Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Adamu na Kristo
12 Dhambi ilikuja ulimwenguni kwa sababu ya kile alichofanya mtu mmoja. Na dhambi ikaleta kifo. Kwa sababu hiyo ni lazima watu wote wafe, kwa kuwa watu wote wametenda dhambi. 13 Dhambi ilikuwepo ulimwenguni kabla ya Sheria ya Musa. Lakini Mungu hakutunza kumbukumbu ya dhambi ya watu wakati sheria haikuwepo. 14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Musa, mauti ilitawala juu ya kila mtu. Adamu alikufa kwa sababu alitenda dhambi kwa kutokutii amri ya Mungu. Lakini hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa njia hiyo hiyo walipaswa kufa.
Hivyo mtu mmoja Adamu anaweza kufananishwa na Kristo, Yeye ambaye angekuja baadaye. 15 Lakini kipawa cha Mungu hakifanani na dhambi ya Adamu. Watu wengi walikufa kwa sababu ya dhambi ya mtu huyo mmoja. Lakini neema waliyopokea watu kutoka kwa Mungu ilikuwa kuu zaidi. Wengi walikipokea kipawa cha Mungu cha uzima kwa neema ya huyu mtu mwingine, Yesu Kristo. 16 Baada ya Adamu kutenda dhambi mara moja, alihukumiwa kuwa na hatia. Lakini kipawa cha Mungu ni tofauti. Kipawa chake cha bure kilikuja baada ya dhambi nyingi, nacho kinawafanya watu wahesabiwe haki mbele za Mungu. 17 Mtu mmoja alitenda dhambi, hivyo kifo kikawatawala watu wote kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Lakini sasa watu wengi wanaipokea neema ya Mungu iliyo nyingi sana na karama yake ya ajabu ya kufanyika wenye haki. Hakika watakuwa na uzima wa kweli na kutawala kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo.
18 Hivyo dhambi hiyo moja ya Adamu ilileta adhabu ya kifo kwa watu wote. Lakini kwa njia hiyo hiyo, Kristo alifanya kitu chema zaidi kilichowezesha watu kufanyika wenye haki mbele za Mungu. Na hicho huwaletea uzima wa kweli. 19 Mtu mmoja hakumtiii Mungu na wengi wakafanyika wenye dhambi. Lakini kwa namna hiyo hiyo, mtu mmoja alipotii, wengi wamefanyika kuwa wenye haki.
Yesu Ajaribiwa na Shetani
(Mk 1:12-13; Lk 4:1-13)
4 Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu hadi nyikani ili akajaribiwe na Shetani. 2 Baada ya Yesu kufunga kwa siku arobaini mchana na usiku, akaumwa njaa sana. 3 Mjaribu[a] akamwendea na akasema, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, basi yaamuru mawe haya yawe mikate.”
4 Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu.’”(A)
5 Kisha Shetani alimwongoza Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na akamweka juu ya mnara wa Hekalu. 6 Akamwambia Yesu, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe mpaka chini! Kwani Maandiko yanasema,
‘Mungu atawaamuru malaika zake wakusaidie,
na mikono yao itakupokea,
ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’”(B)
7 Yesu akamjibu, “Pia, Maandiko yanasema, ‘usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(C)
8 Kisha Shetani akamwongoza Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima ulio mrefu sana na kumwonyesha falme zote za ulimwengu na vitu vya kupendeza vilivyomo ndani. 9 Shetani akamwambia Yesu, “Ukiinama na kuniabudu, nitakupa vitu hivi vyote.”
10 Yesu akamjibu Shetani akamwambia, “Ondoka kwangu Shetani! Kwani Maandiko yanasema, ‘Umwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake!’”(D)
11 Baada ya hayo, Shetani akamwacha. Ndipo malaika wakaja kumhudumia.
© 2017 Bible League International