Revised Common Lectionary (Complementary)
Yohana Ayaandikia Makanisa
4 Kutoka kwa Yohana,
Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; 5 na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.
Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. 6 Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.
7 Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma.[a] Watu wote wa dunia watamwombolezea.[b] Ndiyo, hili litatokea! Amina.
8 Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega.[c] Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.”
33 Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”
34 Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”
35 Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?”
36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”
37 Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”
Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”
© 2017 Bible League International