Revised Common Lectionary (Complementary)
Endeleeni Kumfuata Kristo Yesu
6 Mlimpokea Kristo Yesu kama Bwana, hivyo mwendelee kumfuata yeye. 7 Na mizizi yenu ikue hata ndani ya Kristo, na maisha yenu yajengwe juu yake. Kama mlivyofundishwa imani ya kweli mwendelee kuwa imara katika ufahamu wenu katika hilo. Na msiache kumshukuru Mungu.
8 Angalieni msichukuliwe mateka na mafundisho ya uongo kutoka kwa watu wasio na chochote cha maana kusema, bali kuwadanganya tu. Mafundisho yao hayatoki kwa Kristo bali ni desturi za kibinadamu tu na zinatoka katika nguvu za uovu zinazotawala maisha ya watu. 9 Nasema hili kwa sababu Mungu mwenyewe kama alivyo, ukamilifu wa uungu wake unaishi ndani ya Kristo. Hii ni hata wakati wa maisha yake hapa duniani. 10 Na kwa sababu ninyi ni wa Kristo basi mmekamilika, na mna kila kitu mnachohitaji. Kristo ni mtawala juu ya kila nguvu na mamlaka zingine zote.
11 Mlitahiriwa katika Kristo kwa namna tofauti, si kwa mikono ya kibinadamu. Hii ni kusema ya kwamba, mlishiriki katika kifo cha Kristo, ambacho kilikuwa aina ya tohara kwa namna ya kuuvua mwili wake wa kibinadamu.[a] 12 Na mlipobatizwa, mlizikwa na kufufuka pamoja naye kutokana na imani yenu kwa nguvu za Mungu aliyemfufua Kristo kutoka katika kifo.
13 Mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi zenu na kwa sababu hamkuwa sehemu ya watu wa Mungu.[b] Lakini Mungu amewapa ninyi uhai mpya pamoja na Kristo na amewasamehe dhambi zenu zote. 14 Kwa sababu tulizivunja sheria za Mungu, tunalo deni. Kumbukumbu ya deni hilo imeorodhesha amri zote tulizoshindwa kuzifuata. Lakini Mungu ametusamehe deni hilo. Ameiondoa kumbukumbu yake na kuipigilia msalabani. 15 Pale msalabani, aliwanyang'anya watawala wa ulimwengu wa roho nguvu na mamlaka. Aliwashinda pale. Na akawafukuza kama wafungwa ili ulimwengu wote uone.
Msizifuate Sheria Zilizowekwa na Watu
16 Hivyo msimruhusu mtu yeyote awahukumu katika masuala yanayohusu kula au kunywa au kwa kutofuata desturi za Kiyahudi (kusherehekea siku takatifu, sikukuu za Mwandamo wa Mwezi,[a] au siku za Sabato). 17 Zamani mambo hayo yalikuwa kama kivuli cha yale yaliyotarajiwa kuja. Lakini mambo mapya yaliyotarajiwa kuja yanapatikana katika Kristo. 18 Watu wengine hufurahia kutenda mambo yanayowafanya wajisikie kuwa ni wanyenyekevu na kisha kushirikiana na malaika katika ibada.[b] Nao wanazungumza juu ya kuyaona mambo hayo katika maono. Msiwasikilize wanapowaambia kuwa mnakosea kwa sababu hamfanyi mambo haya. Ni ujinga kwao kujisikia fahari kwa kufanya hivyo, kwa sababu mambo hayo yote yanatokana na namna mwanadamu anavyofikiri. 19 Hawajafungamanishwa na kichwa; Kristo ndiye kichwa, na mwili wote humtegemea Yeye. Kwa sababu ya Kristo viungo vyote vya mwili vinatunzana na kusaidiana kila kimoja na kingine. Hivyo mwili hupata nguvu zaidi na kufungamana pamoja kadri Mungu anavyouwezesha kukua.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Mt 6:9-15)
11 Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.”
2 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima.
Tunaomba Ufalme wako uje.
3 Utupe chakula tunachohitaji kila siku.
4 Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea.
Na usiruhusu tukajaribiwa.’”
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Mt 7:7-11)
5-6 Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ 7 Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ 8 Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. 9 Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. 10 Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. 11 Je, kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je, kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? 12 Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. 13 Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?”
© 2017 Bible League International