Old/New Testament
Kuhusu Ndoa
7 Sasa nitazungumza kuhusu mambo yale mliyoniandikia. Mliuliza ikiwa ni bora mwanaume asimguse mwanamke kabisa. 2 Lakini dhambi ya uzinzi ni ya hatari, hivyo kila mwanaume anapaswa kumfurahia mke wake, na kila mwanamke anapaswa kumfurahia mume wake. 3 Mume anapaswa kumtosheleza mkewe, vivyo hivyo mke amtosheleze mume wake. 4 Mke hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe. Mume hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. 5 Msinyimane miili yenu. Lakini mnaweza kukubaliana kutojamiiana kwa muda ili mtumie muda huo katika maombi. Kisha mkutane tena ili Shetani asiwajaribu kutokana na kushindwa kujizuia tamaa zenu. 6 Ninasema hivi ili kuwaruhusu mtengane kwa muda tu. Lakini hii siyo amri. 7 Mimi ningependa kila mtu angekuwa kama mimi nilivyo. Lakini Mungu amempa kila mtu uwezo tofauti. Huwafanya wengine kuwa hivi na wengine kuwa vile.
8 Sasa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa ama hawajaolewa na kwa ajili ya wajane ninawaambia ya kwamba ni vizuri mkae bila kuoa au kuolewa kama mimi. 9 Lakini ikiwa mtashindwa kudhibiti tamaa zenu, basi mwoe au muolewe. Ni vyema kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
10 Na sasa ninawaamuru wale walio katika ndoa. Si amri kutoka kwangu, lakini ndivyo Bwana aliamuru. Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake. 11 Lakini ikiwa mke anaondoka, anapaswa kukaa bila kuolewa au arudi kwa mume wake. Na mume hapaswi kumtaliki mke wake.
12 Ushauri nilionao kwa wengine unatoka kwangu. Bwana hajatupa mafundisho mengine kuhusu hili. Ukiwa na mke asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 13 Na kama una mume asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 14 Mume asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mke wake anayeamini. Na mke asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mume wake anayeamini. Ikiwa hii si sahihi basi watoto wenu wasingefaa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Lakini sasa wametengwa kwa ajili yake.
15 Lakini mume au mke asiyemwamini akiamua kuondoka katika ndoa. Hili linapotokea, ndugu aliye katika Kristo anakuwa huru. Mungu aliwachagua ili muwe na maisha ya amani. 16 Inawezekana ninyi wake mtawaokoa waume zenu; nanyi waume mtawaokoa wake zenu kwani bado hamjui kitakachotokea baadaye.
Ishini Kama Mlivyokuwa Mungu Alivyowaita
17 Kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuishi katika namna ambayo Bwana Mungu amewapa, kuishi kama mlivyoishi Mungu alipowaita. Ninawaambia watu katika makanisa yote kufuata kanuni hii. 18 Mwanaume asibadili tohara yake ikiwa alikuwa ametahiriwa alipoitwa. Ikiwa hakuwa ametahiriwa alipoitwa, asitahiriwe. 19 Kutahiriwa au kutotahiriwa si muhimu. Kilicho muhimu ni kutii amri za Mungu.
© 2017 Bible League International