Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Petro 3:8-5:14

Kuteseka kwa kutenda haki

Hivyo ninyi nyote mnapaswa kuishi pamoja kwa amani. Mjitahidi kuelewana ninyi wenyewe. Mpendane kama kaka na dada na muwe wanyenyekevu na wema. Msimfanyie uovu mtu yeyote ili kulipa kisasi kwa uovu aliowatendea. Msimtukane mtu yeyote ili kulipiza matusi aliyowatukana. Lakini mwombeni Mungu awabariki watu hao. Fanyeni hivyo kwa sababu ninyi wenyewe mliteuliwa kupokea baraka, 10 Maandiko yanasema:

“Anayetaka kufurahia maisha ya kweli
    na kuwa na siku nyingi njema tu,
aepuke kusema chochote kinachoumiza,
    na asiruhusu uongo utoke kwenye kinywa yake.
11 Aache kutenda uovu, na atende mema.
    Atafute amani, na fanya kila analoweza ili kuwasaidia watu kuishi kwa amani.
12 Bwana huwaangalia wale watendao haki,
    na husikia maombi yao.
Lakini yu kinyume cha wale watendao uovu.”(A)

13 Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru? 14 Lakini hata ukiteseka kwa sababu kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu. “Msimwogope mtu yeyote, wala msiruhusu watu wawasumbue.”(B) 15 Lakini mjitoe kikamilifu kwa Kristo ambaye ni Bwana wenu pekee. Na daima iweni tayari kumjibu mtu yeyote anayetaka ufafanuzi kuhusu tumaini linaloyaongoza maisha yenu.[a] 16 Lakini wajibuni kwa upole na heshima kwa ajili ya Mungu, mkizitunza dhamiri zenu mbele zake. Ndipo watu watakapoona namna njema mnayoishi kama wafuasi wa Kristo. Na wataaibika kwa kuwanenea mabaya.

17 Ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya. Ndiyo, ni bora ikiwa hivyo ndivyo Mungu anavyotaka.

18 Kristo mwenyewe aliteseka alipokufa kwa ajili yenu,
    na kwa kifo hicho kimoja alilipa fidia kwa ajili ya dhambi.
Hakuwa na hatia,
    lakini alikufa kwa ajili ya watu waliokuwa na hatia.
    Alifanya hivyo ili awalete ninyi nyote kwa Mungu.
Kama mwanadamu, aliuawa,
    lakini uhai wake ulifanywa hai na Roho.[b]

19 Na kwa Roho alikwenda akazihubiri roho zilizo kifungoni. 20 Hizo ndizo roho zilizokataa kumtii Mungu hapo zamani wakati wa Nuhu. Mungu alisubiri kwa uvumilivu Nuhu alipokuwa anaunda safina. Na watu wachache tu, yaani wanane kwa jumla ndiyo walioingia katika safina na kuokolewa kwa kuvushwa salama katika gharika hiyo. 21 Na maji yale ni kama ubatizo, unaowaokoa ninyi sasa kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka katika wafu na siyo kuondoa uchafu mwilini kwa kuoga. Ni ahadi ya dhati ya kuishi kwa kumcha Mungu. 22 Sasa yupo mbinguni upande wa kuume wa Mungu, na anatawala juu ya malaika, mamlaka na nguvu.

Maisha Mapya

Kristo aliteseka alipokuwa katika mwili wake. Hivyo mjitayarishe kwa fikra ile ile aliyokuwa nayo Kristo. Yeyote anayekubali kuteseka katika maisha haya hakika ameamua kuacha kutenda dhambi. Jiimarishe wenyewe ili mweze kuishi maisha yenu yaliyosalia hapa duniani kwa kutenda yale anayotaka Mungu, siyo maovu ambayo watu wanataka kufanya. Huko nyuma mmepoteza muda mwingi mkitenda yale ambayo wasiyomjua Mungu wanapenda kutenda. Mliishi kwa kutojali maadili, mkitenda maovu mliyotaka kutenda. Daima mlikuwa mnalewa, mlifanya sherehe mbaya za ulevi, na mlitenda mambo ya aibu katika ibada zenu za sanamu.

Na sasa “marafiki” zenu wa zamani wanaona ni ajabu kwamba ninyi hamshirikiani nao katika njia za maisha zilizo mbaya na zisizofaa wanazozifuata. Na hivyo wanasema mabaya juu yenu. Lakini itawalazimu kukutana na Mungu na kutoa maelezo juu ya yale waliyoyatenda. Yeye ndiye atakaye hukumu watu wote muda si mrefu, walio hai sasa na wale waliokwisha kufa. Walikosolewa na wengine katika maisha yao hapa duniani. Lakini ulikuwa mpango wa Mungu kwamba wasikie Habari Njema kabla hawajafa ili wawe na maisha mapya katika Roho.

Vitumieni vizuri vipawa vya Mungu

Wakati wa kila kitu kufikia mwisho wake umekaribia. Hivyo iweni waangalifu katika akili zenu na mjizuie kwa kila jambo. Hii itawasaidia katika maombi yenu. Jambo lililo muhimu kuliko yote, daima mpendane ninyi kwa ninyi kikamilifu, kwa sababu upendo huwawezesha kusamehe dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi katika nyumba zenu na kushiriki chakula kwa pamoja pasipo manunguniko. 10 Mungu amewapa neema yake kwa namna nyingi mbalimbali. Hivyo muwe watumishi wema na kila mmoja wenu atumie kipawa chochote alichopewa kwa njia iliyo bora katika kuhudumiana ninyi kwa ninyi. 11 Ikiwa kipawa chako ni kuhubiri, maneno yako yawe kama yanayotoka kwa Mungu. Ikiwa kipawa chako ni kuhudumu, unatakiwa kuhudumu kwa nguvu anazokupa Mungu. Ndipo Mungu atakaposifiwa kwa kila jambo katika Yesu Kristo. Uwezo na utukufu ni wake milele na milele. Amina.

Kuteseka kama mfuasi wa Kristo

12 Rafiki zangu, msishangae kwa sababu ya mateso mnayoyapata sasa, mateso hayo yanaijaribu imani yenu. Msidhani kuwa linalotokea kwenu ni jambo la ajabu. 13 Lakini mnapaswa kufurahi kwa kuwa mnayashiriki mateso ya Kristo. Mtafurahi na kujawa na raha wakati uweza wake mkuu utapodhihirishwa kwa ulimwengu. 14 Mhesabu kuwa ni heshima watu wanapowanenea mabaya kwa sababu mnamwakilisha Kristo. Linapotokea hilo inaonesha kuwa Roho wa Mungu, aliye Roho wa utukufu, yupo pamoja nanyi. 15 Mnaweza kupata mateso; lakini msiteseke kwa sababu mmeua, mmeiba, mmesababisha ghasia, au mmejaribu kutawala maisha ya watu wengine. 16 Lakini endapo utateswa kwa kuwa ni “Mkristo” basi usione haya. Bali umshukuru Mungu kwa kuwa unalibeba jina hilo. 17 Wakati wa kuanza hukumu umewadia. Hukumu hiyo itaanza na familia ya Mungu. Ikiwa itaanzia kwetu, nini kitawatokea wale wasioikubali Habari Njema ya Mungu?

18 “Iwapo ni vigumu hata kwa mtu mwema kuokolewa,
    nini kitatokea kwa yule aliye kinyume na Mungu na amejaa dhambi?”(C)

19 Hivyo kama mnateseka kwa sababu ya kutii mapenzi ya Mungu, yakabidhini maisha yenu kwake maana Yeye ndiye aliyewaumba, na hivyo mnapaswa kumwamini. Na anastahili kuthaminiwa na kuaminiwa.

Kondoo wa Mungu

Sasa nina jambo la kuwaambia wazee walio katika kundi lenu. Mimi pia ni mzee nami mwenyewe nimeyaona mateso ya Kristo. Na nitashiriki katika utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Hivyo ninawasihi, mlitunze kundi la watu mnalowajibika kwalo. Ni kundi lake Mungu.[c] Basi lichungeni kwa moyo wa kupenda na si kwa kulazimishwa. Hivi ndivyo Mungu anavyotaka. Fanyeni hivyo kwa sababu mnafurahi kutumika, na si kwa sababu mnataka pesa. Msiwaongoze wale mnaowasimamia kwa kuwaamrisha. Lakini muwe mfano mzuri wa kuiga kwao. Ili Kristo aliye Mchungaji Mkuu atakapokuja, mpate taji yenye utukufu na isiyopoteza uzuri wake.

Vijana, nina jambo la kuwaambia ninyi pia. Mnapaswa kutii mamlaka ya wazee. Na ninyi nyote mnapaswa kuwa wanyenyekevu ninyi kwa ninyi.

“Mungu yu kinyume na wanaojivuna,
    lakini ni mwema kwa wanyenyekevu.”(D)

Hivyo mjinyenyekeze chini ya mkono wa Mungu wenye nguvu. Kisha, wakati sahihi utakapofika, atawalipa kwa kuwainua. Mpeni Mungu masumbufu yenu yote, kwa sababu Yeye anawajali.

Iweni na kiasi na muwe waangalifu! Shetani ni adui yenu naye huzunguka zunguka kama simba anayeunguruma akimtafuta yeyote wa kumshambulia na kumla. Mpingeni ibilisi. Kisha msimame imara katika imani yenu. Mnafahamu kwamba ndugu zenu ulimwenguni kote wanapitia mateso sawa na hayo mliyonayo.

10 Ndiyo, mtateseka kwa muda mfupi. Lakini baada ya hapo, Mungu ataweka kila kitu sawa. Atawatia nguvu, atawasaidia na kuwashika msianguke. Yeye ni Mungu ndiye chanzo cha neema yote. Aliwachagua mshiriki katika utukufu wake ndani ya Kristo. Utukufu huo utadumu milele. 11 Uwezo wote ni wake milele. Amina.

Salamu za Mwisho

12 Sila ataileta barua hii kwenu. Nafahamu kwamba ni ndugu mwaminifu katika familia ya Mungu. Niliandika barua hii fupi kuwatia moyo na kuwaambia kuwa hii ni neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

13 Kanisa lililoko Babeli[d] linatuma salamu kwenu. Wameteuliwa kama ninyi. Marko, ambaye ni kama mwanangu kwangu katika Kristo, anawasalimu pia. 14 Mpeni kila mmoja wenu salamu maalumu[e] mnapokutana.

Amani iwe kwenu ninyi nyote mlio katika Kristo.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International