Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Ufunuo 1-2

Yohana Aeleza Kuhusu Kitabu Hiki

Huu ni ufunuo[a] kutoka kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa ili awaoneshe watumishi wake yale ambayo ni lazima yatokee muda mfupi ujao. Yesu Kristo alimtuma malaika wake ili amwonyeshe Yohana, mtumishi wake, ambaye amesema kila kitu alichokiona. Ni ukweli alioambiwa na Yesu Kristo; ni ujumbe kutoka kwa Mungu. Ana heri anayesoma maneno ya ujumbe huu kutoka kwa Mungu kwa kupaza sauti na wale wanaousikia ujumbe huu na kuyatendea kazi yaliyoandikwa ndani yake. Wakati uliosalia ni mfupi.

Yohana Ayaandikia Makanisa

Kutoka kwa Yohana,

Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:

Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.

Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.

Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma.[b] Watu wote wa dunia watamwombolezea.[c] Ndiyo, hili litatokea! Amina.

Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega.[d] Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.” Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo[e] kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. 10 Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. 11 Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

12 Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. 13 Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. 15 Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. 16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.

17 Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu. 19 Hivyo andika unachokiona. Yaandike mambo yanayotokea sasa na mambo yatakayotokea baadaye. 20 Hii ni maana iliyofichwa ya nyota na vinara saba vya taa vya dhahabu ulivyoviona: Vinara saba ni makanisa saba. Nyota saba ni malaika wa makanisa saba.”

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Efeso

“Andika hivi kwa malaika[f] wa kanisa lililoko Efeso:

Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu.

Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo. Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa.

Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo. Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake. Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai.[g] Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda.

Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna

Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:

“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.

Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu.[h] Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi[i] la Shetani. 10 Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu[j] ya uzima wa milele.

11 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo

12 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:

Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.

13 Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu[k] aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.

14 Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15 Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16 Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.

17 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!

Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira

18 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:

Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.

19 Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. 20 Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii,[l] lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.

22 Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. 23 Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.

24 Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. 25 Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.

26 Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. 27 Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.[m] 28 Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. 29 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International