Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waebrania 6-7

1-2 Hivyo tusiendelee tena na masomo ya msingi juu ya Kristo. Tusiendelee kurudia kule tulikoanzia. Tuliyaanza maisha yetu mapya kwa kugeuka kutoka katika uovu tuliotenda zamani na kwa kumwamini Mungu. Hapo ndipo tulipofundishwa kuhusu mabatizo,[a] kuwawekea watu mikono,[b] ufufuo wa wale waliokwisha kufa, na hukumu ya mwisho. Sasa tunahitajika kuendelea mbele hadi kwenye mafundisho ya ukomavu zaidi. Na hayo ndiyo tutayafanya Mungu akitupa kibali.

4-6 Baada ya watu kuiacha njia ya Kristo, je unaweza kuwafanya wabadilike tena katika maisha yao? Ninazungumzia wale watu ambao mwanzo walijifunza kweli, wakapokea karama za Mungu, na kushiriki katika Roho Mtakatifu. Walibarikiwa kusikia ujumbe mzuri wa Mungu na kuziona nguvu kuu za ulimwengu wake mpya. Lakini baadaye waliziacha zote, na siyo rahisi kuwafanya wabadilike tena. Ndiyo sababu wale watu wanaomwacha Kristo wanamsulibisha msalabani kwa mara nyingine, wakimwaibisha yeye mbele ya kila mtu.

Watu wengine wako kama ardhi inayopata mvua nyingi na kuzaa mazao mazuri kwa wale wanaoilima. Aina hiyo ya ardhi inazo baraka za Mungu. Lakini watu wengine wako kama ardhi ambayo huzalisha miiba na magugu tu. Haifai na iko katika hatari ya kulaaniwa na Mungu. Itateketezwa kwa moto.

Rafiki zangu, sisemi haya kwa sababu nafikiri kuwa yanawatokea ninyi. Kwa hakika tunatarajia kuwa mtafanya vizuri zaidi; kwamba mtayafanya mambo mema yatakayotokea katika wokovu wenu. 10 Mungu ni wa haki, na ataikumbuka kila kazi mliyoifanya. Atakumbuka kuwa mliuonesha upendo wenu kwake kwa kuwasaidia watu wake na kwamba mnaendelea kuwasaidia. 11 Tunamtaka kila mmoja wenu awe radhi na mwenye shauku ya kuuonyesha upendo kama huo katika maisha yenu yote. Ndipo mtakapokuwa na uhakika wa kupata kile mnachokitumaini. 12 Hatupendi muwe wavivu. Tunapenda muwe kama wale, kwa sababu ya imani yao na uvumilivu, watapokea kile Mungu alichoahidi.

13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu. Na hayuko yeyote aliye mkuu kuliko Mungu, hivyo akaweka ahadi yenye kiapo kwa jina lake mwenyewe; kiapo ambacho atatimiza alichoahidi. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki. Nitakupa wewe wazaliwa wengi.”(A) 15 Ibrahimu akangoja kwa uvumilivu hili litimie, na baadaye akapokea kile Mungu alichoahidi.

16 Mara nyingi watu hutumia jina la mtu aliye mkuu zaidi yao ili kuweka ahadi yenye kiapo. Kiapo huthibitisha kwamba walichokisema ni kweli, na hakuna haja ya kubishana juu ya hilo. 17 Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. 18 Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo.

Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. 19 Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia[c] katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. 20 Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.

Kuhani Melkizedeki

Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu. Alikutana na Ibrahimu wakati Ibrahimu alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme. Siku hiyo Melkizedeki alimbariki Ibrahimu. Kisha Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya kila kitu alichokuwa nacho.

Jina Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lilikuwa na maana mbili. Kwanza, Melkizedeki inamaanisha “mfalme wa haki.” Na “mfalme wa Salemu” inamaanisha “mfalme wa amani.” Hakuna ajuaye baba na mama yake walikuwa ni kina nani au walitokea wapi.[d] Na hakuna ajuaye alizaliwa lini au alikufa lini. Melkizedeki ni kama Mwana wa Mungu kwa vile siku zote atakuwa kuhani.

Unaweza kuona kuwa Melkizedeki alikuwa mkuu sana. Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa yeye sehemu ya kumi ya kila alichoshinda kule vitani. Sasa sheria inasema kwamba wale wa ukoo wa Lawi waliokuja kuwa makuhani wanastahili kupata sehemu ya kumi kutoka kwa watu wao, hata kama wao na watu wao ni wa familia ya Ibrahimu. Melkizedeki wala hakutoka katika kabila la Lawi, lakini Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya alivyokuwa navyo. Na Melkizedeki akambariki Ibrahimu yule aliyekuwa na ahadi za Mungu. Na kila mtu anajua kwamba mtu aliye wa muhimu zaidi humbariki mtu yule ambaye ana umuhimu mdogo.

Makuhani hawa hupata sehemu ya kumi, lakini wao ni binadamu tu wanaoishi kisha hufa. Lakini Melkizedeki, aliyepata sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu, anaendelea kuishi, kama Maandiko yanavyosema. Sasa wale wa kutoka ukoo wa Lawi ndiyo wanaopata sehemu ya kumi kutoka kwa watu. Lakini tunaweza kusema kuwa Ibrahimu alipompa Melkizedeki sehemu ya kumi, kisha Lawi naye akatoa. 10 Lawi alikuwa bado hajazaliwa, lakini alikuwepo katika baba yake Ibrahimu wakati Melkizedeki alipokutana naye.

11 Watu walipewa sheria chini ya mfumo wa makuhani waliotoka katika ukoo wa Lawi. Lakini hayupo awezaye kufanywa mkamilifu kiroho kwa njia ya mfumo wa makuhani. Hivyo lilikuwepo hitaji la kuhani mwingine kuja. Namaanisha kama Melkizedeki, siyo Haruni. 12 Na anapokuja kuhani wa aina nyingine, basi sheria pia inabidi ibadilishwe. 13-14 Tunazungumza juu ya Bwana Yesu, aliyetoka katika kabila lingine. Hakuwepo yeyote kutoka katika kabila hilo kamwe aliyeweza kutumika kama kuhani madhabahuni. Ni dhahiri kwamba Bwana Yesu alitoka katika kabila la Yuda. Na Musa hakusema chochote kuhusu makuhani waliyetokana na kabila hilo.

Yesu Ni Kuhani Mfano wa Melkizedeki

15 Na mambo haya yalizidi kuwa wazi zaidi tunapomwona kuhani mwingine aliye kama Melkizedeki. 16 Alifanywa kuhani, lakini siyo kwa sababu alikamilisha mahitaji ya kuzaliwa katika familia sahihi. Alifanyika kuhani kwa nguvu ya uhai ambayo haitakwisha. 17 Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema kumhusu yeye: “Wewe ni kuhani milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.”(B)

18 Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia. 19 Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu.

20 Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo. 21 Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia:

“Bwana anaweka ahadi kwa kiapo
    naye hatabadili mawazo yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’”(C)

22 Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake.

23 Pia, mmoja wa hawa makuhani wengine alipofariki, asingeendelea kuwa kuhani. Hivyo walikuwepo makuhani wengi wa jinsi hii. 24 Lakini Yesu anaishi milele. Hatakoma kufanya kazi kama kuhani. 25 Hivyo anaweza kuwaokoa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake. Yesu anaweza kufanya hivi milele, kwa sababu anaishi siku zote na yuko tayari kuwasaidia watu wanapomjia Mungu.

26 Hivyo Yesu ni aina ya kuhani mkuu tunayemhitaji. Yeye ni mkamilifu. Hana dhambi ndani yake. Hana kasoro na havutwi na watenda dhambi. Naye amepandishwa juu ya mbingu. 27 Hayuko sawa na hawa makuhani wengine. Walitakiwa kutoa sadaka kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Lakini Yesu hahitaji kufanya hivyo. Alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya nyakati zote. Alijitoa mwenyewe. 28 Sheria huchagua makuhani wakuu ambao ni watu na wanao udhaifu ule ule ambao watu wote wanao. Lakini baada ya sheria, Mungu alisema kiapo ambacho kilimfanya Mwana awe kuhani mkuu. Na Mwana huyo, aliyekamilishwa kwa njia ya mateso, atatumika kama kuhani mkuu milele yote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International