Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 1

Luka Aandika Kitabu Kingine

Mpendwa Theofilo:

Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu Achukuliwa Juu Mbinguni

Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?”

Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.”

Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. 10 Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. 11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.”

Mtume Mpya Achaguliwa

12 Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja[a] kutoka Yerusalemu. 13 Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo).

14 Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume.

15 Baada ya siku chache waamini waliokuwa kama mia moja na ishirini walikutana pamoja. Petro alisimama na kusema, 16-17 “Kaka na dada zangu, katika Maandiko Roho Mtakatifu alisema kupitia Daudi kwamba jambo fulani lazima litatokea. Alizungumza kuhusu Yuda, yule aliyekuwa katika kundi letu wenyewe. Yuda alihudumu pamoja nasi. Roho alisema Yuda atawaongoza watu kumkamata Yesu.”

18 (Kwa kufanya hili Yuda alilipwa pesa. Alinunulia shamba pesa hizo. Lakini aliangukia kichwa chake, mwili wake ukapasuka, na matumbo yake yote yakamwagika nje. 19 Na watu wote wa Yerusalemu wanalijua hili. Ndiyo maana waliliita shamba hilo Akeldama, ambalo maana yake kwa Kiaramu ni “Shamba la Damu”.)

20 Petro akasema, “Katika kitabu cha Zaburi, jambo hili limeandikwa kuhusu Yuda:

‘Watu wasipakaribie mahali pake;
    Yeyote asiishi hapo.’(A)

Pia imeandikwa kuwa:

‘Mtu mwingine achukue kazi yake.’(B)

21-22 Hivyo ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi ili awe shahidi wa ufufuo wa Bwana Yesu. Ni lazima awe mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana Yesu alipokuwa pamoja nasi. Ni lazima awe yule ambaye amekuwa pamoja nasi tangu Yohana alipokuwa anabatiza watu mpaka siku ambayo Bwana Yesu alichukuliwa kutoka kwetu na kwenda mbinguni.”

23 Kisha waliwasimamisha watu wawili mbele ya kundi. Mmoja aliitwa Yusufu Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto. Mwingine aliitwa Mathiasi. 24-25 Wakaomba wakisema, “Bwana unajua mioyo ya watu wote. Tuonyeshe kati ya watu hawa wawili uliyemchagua kufanya kazi hii. Yuda aliiacha na kuifuata njia yake. Bwana tuonyeshe ni nani achukue sehemu yake kama mtume!” 26 Kisha wakapiga kura kumchagua mmoja kati ya watu hao wawili. Kura ikaonesha Mathiasi ndiye Bwana anamtaka. Hivyo akawa mtume pamoja na wale wengine kumi na moja.

Kuja kwa Roho Mtakatifu

Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.

Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.

Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[b] Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”

12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.

Petro Azungumza na Watu

14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:

17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
    nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
    Vijana wenu wataona maono,
    na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
    yangu kwa watumishi wangu,
    wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
    Nitasababisha ishara chini duniani.
    Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
    na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
    kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[c] ataokolewa.(C)

22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:

‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
    Yupo hapa pembeni yangu,
    hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
    na ninaimba kwa furaha!
    Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[d]
    Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[e] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
    Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(D)

29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[f] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:

‘Hakuachwa kaburini.
    Mwili wake haukuozea humo.’[g]

Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. 32 Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. 33 Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia 34 Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kuume
35     hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’[h](E)

36 Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!”

37 Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?”

38 Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.”

40 Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” 41 Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile.

Ushirika wa Waamini

42 Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula[i] na kuomba pamoja. 43 Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44 Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45 Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46 Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47 Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International