New Testament in a Year
17 Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. 18 Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. 19 Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. 20 Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Ushauiri Kwa Mke na Mume
21 Mwe radhi kuhudumiana ninyi kwa ninyi kwa kuwa mnamheshimu Kristo.
22 Wake, muwe radhi kuwahudumia waume zenu kama mlivyo radhi kumtumikia Bwana. 23 Mume ni kichwa cha mke wake, kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Kristo ni Mwokozi wa kanisa, ambalo ni mwili wake. 24 Kanisa hutumika chini ya Kristo, hivyo ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi wake. Mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu katika kila jambo.
25 Waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuyatoa maisha yake kwa ajili yake. 26 Alikufa ili alitakase kanisa lake. Alitumia ujumbe wa Habari Njema kulisafisha kanisa kwa kuliosha katika maji. 27 Kristo alikufa ili aweze kujiletea mwenyewe kanisa lililo kama bibi harusi katika uzuri wake wote. Alikufa ili kanisa liweze kuwa takatifu na lisilo na dosari, lisilokuwa na uovu au dhambi au chochote kilicho kibaya ndani yake.
28 Na waume wawapende hivyo wake zao. Wawapende wake zao kama vile ni miili yao wenyewe. Mtu anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe, 29 kwa sababu kamwe hakuna anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza. Na hivyo ndivyo Kristo anavyolifanyia kanisa 30 kwa sababu sisi sote ni viungo vya mwili wake. 31 Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mkewe, nao hao wawili watafanyika mwili mmoja.”(A) 32 Siri hiyo ya kweli ni ya muhimu sana, ninazungumza juu ya Kristo na kanisa. 33 Lakini kila mmoja wenu anapaswa kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwenyewe. Na mke anapaswa kumheshimu mume wake.
© 2017 Bible League International