M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Awatokea wafuasi Wake Saba
21 Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: 2 Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. 3 Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.”
Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu.
4 Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. 5 Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?”
Wao wakajibu, “Hapana.”
6 Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua.
7 Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. 8 Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100[a] tu. 9 Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. 10 Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua.
11 Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. 13 Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia.
14 Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
Yesu Azungumza na Petro
15 Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo[b] wangu.”
16 Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.”
17 Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!”
Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. 18 Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako,[c] na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” 19 (Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka na kumwona yule mfuasi mwingine aliyependwa sana na Yesu akitembea nyuma yao. (Huyu alikuwa ni mfuasi aliyejilaza kwa Yesu wakati wa chakula cha jioni na kusema, “Bwana, ni nani atakayekusaliti kwa maadui zako?”) 21 Petro alipomwona nyuma yao, akamwuliza Yesu, “Bwana, vipi kuhusu yeye?”
22 Yesu akajibu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali. Wewe nifuate!”
23 Kwa hiyo habari ikaenea miongoni mwa wafuasi wa Yesu. Wao walikuwa wakisema kuwa mfuasi huyo asingekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa asingekufa. Yeye alisema tu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali.”
24 Huyo mfuasi ndiye yeye anayesimulia habari hizi. Ndiye ambaye sasa ameziandika habari zote hizi. Nasi tunajua kuwa anayoyasema ni kweli.
25 Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu. Kama kila moja ya hayo yote yangeandikwa, nafikiri ulimwengu wote usingevitosha vitabu ambavyo vingeandikwa.
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka niwe. Salamu pia kutoka kwa Timotheo ndugu yetu katika Kristo.
2 Salamu kwenu kaka na dada zetu watakatifu na walio waaminifu katika Kristo mlioko Kolosai.
Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu ziwe pamoja nanyi.
3 Katika maombi yetu tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Yeye ndiye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. 4 Nasi tunamshukuru Yeye kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu na upendo wenu kwa watu wa Mungu wote. 5 Imani yenu na upendo wenu vinatokana na ufahamu kwamba mtapokea kile mnachotumaini. Hicho ambacho Mungu amekihifadhi salama mbinguni kwa ajili yenu. Hilo ni tumaini lile lile ambalo mmekuwa nalo tangu mliposikia kwa mara ya kwanza ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema. 6 Habari Njema hii imezaa matunda na imeenea ulimwenguni kote. Na hicho ndicho kilichokuwa kikitokea tangu siku mliposikia kwa mara ya kwanza na kuelewa ukweli wa neema ya Mungu. 7 Kweli hiyo mliisikia kutoka kwa Epafra, aliye mtumwa wa Bwana pamoja nasi. Yeye anatusaidia sisi[b] kama mtumishi mwaminifu wa Kristo. 8 Naye ametueleza pia kuhusu upendo mlioupokea kutoka kwa Roho Mtakatifu.
9 Ndugu zangu tangu siku tuliposikia mambo haya juu yenu, tumeendelea kuwaombea, na haya ndiyo maombi yetu kwa ajili yenu:
Kwamba Mungu awajaze ufahamu wa mapenzi yake kwa kuwapa hekima na ufahamu wote wa kiroho mnaohitaji; 10 ili hayo yawasaidie kuishi maisha yanayomletea Bwana heshima na kumpendeza yeye katika hali zote; ili maisha yenu yazae matunda mema ya aina mbalimbali na mpate kuongezeka katika maarifa yenu ya Mungu;[c] 11 ili Mungu mwenyewe awaimarishe kwa uwezo wake mkuu, ili muwe na uvumilivu pasipo kukata tamaa mnapokutana na shida.
Ndipo nanyi mtakapofurahi, 12 na kumshukuru Mungu Baba. Kwani yeye amewastahilisha kupokea kile alichowaahidi watakatifu wake, wanaoishi katika nuru. 13 Mungu ametuweka huru kutoka katika nguvu za giza. Naye ametuingiza katika ufalme wa Mwanaye mpendwa. 14 Na huyo Mwana amelipa gharama ya kutuweka huru, kwani ndani yake tuna msamaha wa dhambi zetu.
Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu
15 Hakuna anayeweza kumwona Mungu,
lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.
Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.
16 Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:
vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,
watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.
Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.
17 Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,
na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili,
yaani kanisa.
Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,
ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.[d]
Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.
19 Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake
uishi ndani ya Mwana.
20 Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi
kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;
vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.
Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.
21 Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye. 22 Lakini sasa amewafanya kuwa marafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake; 23 na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya.
Kazi ya Paulo kwa Ajili ya Kanisa
24 Nina furaha kwa sababu ya mateso ninayopata kwa manufaa yenu. Yapo mambo mengi ambayo kupitia hayo Kristo bado anateseka. Nami ninayapokea mateso haya kwa furaha katika mwili wangu kwa ajili ya mwili wake, yaani Kanisa. 25 Nilifanyika kuwa mtumishi wa kanisa kwa sababu Mungu alinipa kazi maalum ya kufanya. Kazi hii inawasaidia ninyi, nayo ni kuuhubiri ujumbe kamili wa Mungu. 26 Ujumbe huu ni ukweli wenye siri uliofichwa tangu mwanzo wa nyakati. Nao ulifichwa kutoka kwa kila mtu kwa muda mrefu, lakini sasa umedhihirishwa kwa watakatifu wa Mungu. 27 Mungu aliamua kuwajulisha watu wake namna Kweli hii ilivyo na utajiri na utukufu. Siri hii ya kweli hii, ambayo ni kwa ajili ya watu wote, ni kwamba Kristo anaishi ndani yenu. Yeye ndiye tumaini la kushiriki katika utukufu wake. 28 Hivyo tunaendelea kuwaambia watu juu ya Kristo. Tunatumia hekima yote kumshauri na kumfundisha kila mtu. Tunajaribu kumleta kila mtu mbele za Mungu kama watu waliokomaa kiroho katika uhusiano wao na Kristo. 29 Kwa kufanya hivi, ninafanya kazi kwa bidii, nikijitahidi na kutumia nguvu kubwa aliyonipa Kristo. Nguvu hiyo inafanya kazi katika maisha yangu.
© 2017 Bible League International