Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

M’Cheyne Bible Reading Plan

The classic M'Cheyne plan--read the Old Testament, New Testament, and Psalms or Gospels every day.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Judg for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Matendo 7

Hotuba ya Stefano

Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Ibrahimu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’(A)

Hivyo Ibrahimu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo[a] na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. Lakini Mungu hakumpa Ibrahimu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Ibrahimu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Ibrahimu hajapata watoto.

Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’(B) Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’(C)

Mungu aliweka agano na Ibrahimu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Ibrahimu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu.

Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10 akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. 11 Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote.

12 Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. 13 Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. 14 Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. 15 Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. 16 Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori.

17 Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Ibrahimu ilikuwa karibu kutimia. 18 Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. 19 Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe.

20 Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. 21 Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. 22 Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.

23 Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24 Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25 Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.

26 Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27 Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28 Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’(D) 29 Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.

30 Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31 Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32 Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(E) Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.

33 Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34 Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’(F)

35 Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’(G) Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,[b] ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36 Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.

37 Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’(H) 38 Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.

39 Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40 Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’(I) 41 Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.[c] Kitabu cha manabii[d] kinasema hivi:

‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
    jangwani kwa miaka arobaini.
43 Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
    na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
    Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’(J)

44 Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. 45 Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. 46 Mungu alimpenda Daudi.[e] Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli[f] 47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu.

48 Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi:

49 ‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi,
    na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu.
Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba?
    Je, ninahitaji mahali pa kupumzika?
50 Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’”(K)

51 Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52 Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53 Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,[g] aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”

Stefano Auawa

54 Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”

57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.

Error: Book name not found: Jer for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Marko 2

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mt 9:1-8; Lk 5:17-26)

Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini[a] kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.”

Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? 10 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? 11 Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’”

12 Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!”

Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu

(Mt 9:9-13; Lk 5:27-32)

13 Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. 14 Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata.

15 Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. 16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?”

17 Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mt 9:14-17; Lk 5:33-39)

18 Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.”

19 Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga.

21 Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. 22 Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani[b] vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.”

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)

23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”

25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”

27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International