M’Cheyne Bible Reading Plan
Mnyama kutoka Baharini
13 Kisha niliona mnyama mwenye pembe kumi na vichwa saba akipanda kutoka baharini. Kila pembe yake ilikuwa na taji. Alikuwa na kumkufuru Mungu lililoandikwa kwenye kila kichwa. 2 Mnyama huyu alionekana kama chui, miguu yake ilikuwa kama ya dubu. Mdomo wake ulikuwa kama wa simba. Joka akampa huyo mnyama uweza wake wote, kiti chake cha enzi na mamlaka kuu.
3 Kichwa kimoja cha mnyama kilionekana kama kimejeruhiwa na kuuawa, lakini kidonda cha mauti kilipona. Watu wote ulimwenguni walishangaa, na wote walimfuata mnyama. 4 Watu waliliabudu joka kwa sababu limempa nguvu mnyama, na pia walimwabudu mnyama. Waliuliza, “Nani ana nguvu kama mnyama? Nani anaweza kufanya vita dhidi yake?”
5 Mnyama aliruhusiwa kujigamba na kumtukana Mungu na kutumia nguvu zake kwa miezi arobaini na mbili. 6 Mnyama alifungua kinywa chake ili amtukane Mungu, alitukane jina lake, mahali anapoishi, na wale wote wanaoishi mbinguni. 7 Alipewa uwezo wa kufanya vita na watakatifu wa Mungu na kuwashinda. Alipewa uwezo juu ya kila kabila, asili, lugha na taifa. 8 Kila anayeishi duniani angemwabudu mnyama. Hawa ni watu wote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tangu mwanzo wa ulimwengu. Mwanakondoo ndiye yule aliyeuawa.
9 Kila mtu anayesikia mambo haya azingatie hili:
10 Yeyote ambaye ni lazima awe mfungwa,
atakuwa mfungwa.
Yeyote ambaye ni wa kuuawa kwa upanga,
atauawa kwa upanga.
Hii inamaanisha kwamba watakatifu wa Mungu lazima wawe na subira na imani.
Mnyama Kutoka Nchi Kavu
11 Pia nikaona mnyama mwingine akija kutoka katika nchi. Alikuwa na pembe mbili kama kondoo, lakini anaongea kama joka. 12 Mnyama huyu alisimama mbele ya mnyama wa kwanza na kutumia nguvu ile ile ya mnyama wa kwanza. Alitumia nguvu hii kumfanya kila mtu aishiye duniani amwabudu mnyama wa kwanza. Mnyama wa kwanza ndiye mwenye jeraha la mauti lililopona. 13 Mnyama wa pili alifanya miujiza[a] mikuu. Alitengeneza hata moto ushuke kutoka mbinguni kuja duniani watu wakiangalia.
14 Mnyama huyu wa pili aliwadanganya watu wanaoishi duniani kwa kutumia miujiza ambayo amepewa uwezo wa kuifanya kwa ajili ya mnyama wa kwanza. Aliwaamuru watu kutengeneza sanamu ili kumheshimu mnyama wa kwanza, aliyejeruhiwa kwa upanga lakini hakufa bali akawa hai tena. 15 Mnyama wa pili alipewa uwezo wa kuipa uzima sanamu ya mnyama wa kwanza. Kisha kinyago kiliweza kuongea na kuamuru watu wote ambao hawakukiabudu wauawe. 16 Pia mnyama wa pili aliwaamuru watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na maskini, walio huru au watumwa, wawekewe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. 17 Hakuna ambaye angeweza kununua au kuuza bila ya kuwa na alama hii. (Alama hii ni jina la mnyama au namba ya jina lake.)
18 Kila mwenye uelewa anaweza kujua maana ya namba ya mnyama. Hili linahitaji hekima. Namba hii ni namba ya mtu. Nayo ni 666.
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)
12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. 2 Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. 3 Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita[a] hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. 5 Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka[b] wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” 6 Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.
7 Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. 8 Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini.[c] Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”
Mpango Dhidi ya Lazaro
9 Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. 10 Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro. 11 Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu.
Yesu Anaingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Lk 19:28-40)
12 Siku iliyofuata watu waliokuwamo Yerusalemu walisikia kwamba Yesu alikuwa anakuja huko. Hili ni kundi la watu waliokuja kusherehekea sikukuu ya Pasaka. 13 Hawa walibeba matawi ya miti ya mitende na kwenda kumlaki Yesu. Pia walipiga kelele wakisema,
“‘Msifuni[d] Yeye!’
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
ajaye kwa jina la Bwana!’(A)
Mungu ambariki Mfalme wa Israeli!”
14 Yesu akamkuta punda njiani naye akampanda, kama vile Maandiko yanavyosema,
16 Wafuasi wa Yesu hawakuyaelewa yale yaliyokuwa yanatokea wakati huo. Lakini Yesu alipoinuliwa juu kwenye utukufu, ndipo walipoelewa kuwa haya yalitokea kama ilivyoandikwa juu yake. Kisha wakakumbuka kwamba walifanya mambo haya kwa ajili ya Yesu.
17 Siku Yesu alipomfufua Lazaro kutoka wafu na kumwambia atoke kaburini walikuwepo watu wengi pamoja naye. Hawa walikuwa wakiwaeleza wengine yale aliyoyafanya Yesu. 18 Ndiyo sababu watu wengi walienda ili kumlaki Yesu; kwa kuwa walikuwa wamesikia habari za ishara hii aliyoifanya. 19 Mafarisayo nao wakasemezana wao kwa wao, “Tazameni! Mpango wetu haufanyi kazi. Watu wote wanamfuata Yesu!”
Yesu Azungumza Juu Uzima na Kifo
20 Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka. 21 Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.” 22 Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake. 24 Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja. 25 Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele. 26 Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
27 Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je, niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso. 28 Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!”
Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.”
29 Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!”
30 Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu. 31 Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu[f] huu atatupwa nje. 32 Nami nitainuliwa juu[g] kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa.
34 Watu wakasema, “Lakini sheria yetu inasema kwamba Masihi ataishi milele. Sasa kwa nini unasema, ‘Ni lazima Mwana wa Adamu ainuliwe juu’? Ni nani huyu ‘Mwana wa Adamu’?”
35 Kisha Yesu akasema, “Nuru[h] itabaki pamoja nanyi kwa muda mfupi tu. Kwa hiyo mtembee mkiwa bado na hiyo nuru. Hapo giza[i] halitaweza kuwakamata. Watu wanaotembea gizani hawajui kule wanakoenda. 36 Hivyo wekeni matumaini yenu katika nuru wakati bado mkiwa nayo. Jinsi hiyo mtakuwa watoto wa nuru.” Yesu alipomaliza kusema mambo hayo, aliondoka na kwenda mahali ambapo watu wasingeweza kumwona.
Baadhi ya Wayahudi Wakataa Kumwamini Yesu
37 Watu wakaona ishara[j] hizi zote alizozifanya Yesu, lakini bado hawakumwamini. 38 Haya yalikuwa hivyo ili kuthibitisha yale aliyoyasema nabii Isaya kuwa:
“Bwana, ni nani aliyeamini yale tuliyowaambia?
Ni nani aliyeziona nguvu za Bwana?”(C)
39 Hii ndiyo sababu watu hawakuweza kuamini. Kwani Isaya alisema pia,
40 “Mungu aliwafanya baadhi ya watu wasione.
Aliufunga ufahamu wao.
Alifanya hivi ili wasiweze kuona kwa macho yao
na kuelewa kwa ufahamu wao.
Alifanya hivyo ili wasiweze kugeuka
na kuponywa.”(D)
41 Isaya alisema hivi kwa sababu aliuona ukuu wa Mungu[k] ndani ya Yesu. Naye alizungumza habari zake Yesu.
42 Lakini watu wengi wakamwamini Yesu. Hata wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi wakamwamini, lakini walikuwa na hofu juu ya Mafarisayo, hivyo hawakusema kwa uwazi kwamba wameamini. Hao walikuwa na hofu kwamba wangeamriwa watoke na kukaa nje ya sinagogi. 43 Wao walipenda kusifiwa na watu zaidi kuliko kupata sifa zinazotoka kwa Mungu.
Mafundisho ya Yesu Yatawahukumu Watu
44 Kisha Yesu akapaza sauti, “Mtu yeyote anayeniamini basi kwa hakika anamwamini yule aliyenituma. 45 Yeyote anayeniona mimi hakika anamwona yeye aliyenituma. 46 Nimekuja katika ulimwengu huu kama mwanga. Nimekuja ili kila mmoja atakayeniamini asiendelee kuishi katika giza.
47 Sikuja ulimwenguni humu kuwahukumu watu. Nimekuja ili kuwaokoa watu wa ulimwengu huu. Hivyo mimi siye ninayewahukumu wale wanaosikia mafundisho yangu bila kuyafuata. 48 Isipokuwa yupo hakimu wa kuwahukumu wote wanaokataa kuniamini na wasiokubaliana na yale ninayoyasema. Ujumbe ninaousema utawahukumu ninyi siku ya mwisho. 49 Hiyo ni kwa sababu yale niliyofundisha hayakutoka kwangu. Baba aliyenituma ndiye aliyeniambia yale nitakayosema na kuyafundisha. 50 Nami najua amri za Mungu kwamba lolote alisemalo na kutenda litawaletea watu uzima wa milele, kama watazifanya. Hivyo mambo ninayosema ni yale ambayo Baba yangu ameniambia niyaseme.”
© 2017 Bible League International