M’Cheyne Bible Reading Plan
Ukoo wa Yesu
(Lk 3:23-38)
1 Hii ni historia ya ukoo wa Yesu, Masihi.[a] Alitoka katika ukoo wa Daudi, aliyetoka katika ukoo wa Ibrahimu.
2 Ibrahimu alikuwa baba yake Isaka.
Isaka alikuwa baba yake Yakobo.
Yakobo alikuwa baba wa Yuda na ndugu zake.
3 Yuda alikuwa baba wa Peresi na Zera. (Mama yao alikuwa Tamari.)
Peresi alikuwa baba yake Hezroni.
Hezroni alikuwa baba yake Ramu.
4 Ramu alikuwa baba yake Aminadabu.
Aminadabu alikuwa baba yake Nashoni.
Nashoni alikuwa baba yake Salmoni.
5 Salmoni alikuwa baba yake Boazi. (Mama yake Boazi alikuwa Rahabu.)
Boazi alikuwa baba yake Obedi. (Mama yake Obedi alikuwa Ruthu.)
Obedi alikuwa baba yake Yese.
6 Yese alikuwa baba yake Mfalme Daudi.
Daudi alikuwa baba yake Sulemani. (Mama yake Sulemani alikuwa mke wa Uria.)
7 Sulemani alikuwa baba yake Rehoboamu.
Rehoboamu alikuwa baba yake Abiya.
Abiya alikuwa baba yake Asa.
8 Asa alikuwa baba yake Yehoshafati.
Yehoshafati alikuwa baba yake Yoramu.
Yoramu alikuwa baba yake Uzia.
9 Uzia alikuwa baba yake Yothamu.
Yothamu alikuwa baba yake Ahazi.
Ahazi alikuwa baba yake Hezekia.
10 Hezekia alikuwa baba yake Manase.
Manase alikuwa baba yake Amoni.
Amoni alikuwa baba yake Yosia.
11 Yosia alikuwa baba wa Yekonia[b] na ndugu zake.
Walioishi wakati ambao watu walipelekwa utumwani Babeli.
12 Baada ya uhamisho wa Babeli,
Yekonia akawa baba yake Shealtieli.
Shealtieli alikuwa babu wa Zerubabeli.
13 Zerubabeli alikuwa baba yake Abiudi.
Abiudi alikuwa baba yake Eliakimu.
Eliakimu alikuwa baba yake Azori.
14 Azori alikuwa baba yake Sadoki.
Sadoki alikuwa baba yake Akimu.
Akimu alikuwa baba yake Eliudi.
15 Eliudi alikuwa baba yake Eliazari.
Eliazari alikuwa baba yake Matani.
Matani alikuwa baba yake Yakobo.
16 Yakobo alikuwa baba yake Yusufu,
Yusufu alikuwa mume wa Mariamu.
Na Mariamu alimzaa Yesu, anayeitwa Masihi.
17 Kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Ibrahimu mpaka kwa Daudi. Na kulikuwa na vizazi kumi na nne kuanzia kwa Daudi mpaka wakati wa uhamisho wa Babeli. Na palikuwa na vizazi kumi na nne tangu uhamisho wa Babeli mpaka wakati alipozaliwa Yesu, Masihi.
Kuzaliwa kwa Yesu, Masihi
(Lk 2:1-7)
18 Kuzaliwa kwa Yesu Masihi, kulikuwa hivi: Mariamu mama yake alikuwa amechumbiwa na Yusufu. Kabla hawajaoana, Yusufu aligundua kuwa Mariamu alikuwa mja mzito. (Yeye alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.) 19 Kwa kuwa Yusufu alitaka kufanya kile kilichokuwa, alikusudia kumwacha Mariamu kwa siri bila ya kumvunjia heshima.
20 Lakini baada ya Yusufu kuliwazia jambo hili, Malaika wa Bwana alimjia katika ndoto na akamwambia, “Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako. Mimba aliyonayo ameipata kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Atamzaa mwana, nawe utamwita Yesu.[c] Utampa jina hilo Yesu kwa sababu yeye atawaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
22 Haya yote yalitokea ili kutimiza maneno ambayo Bwana aliyasema kupitia kwa nabii aliposema:
23 “Sikiliza! Msichana bikira atapata mimba
na atazaa mtoto wa kiume.
Mtoto huyo ataitwa Emanueli.”(A)
(Yaani “Mungu yu pamoja nasi”.)
24 Yusufu alipoamka alifanya kama alivyoelekezwa na Malaika wa Bwana. Alimuoa Mariamu. 25 Lakini hakukutana naye kimwili mpaka Mariamu alipomzaa mwana. Na Yusufu akamwita Yesu.
Luka Aandika Kitabu Kingine
1 Mpendwa Theofilo:
Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo 2 mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. 3 Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. 4 Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. 5 Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Yesu Achukuliwa Juu Mbinguni
6 Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?”
7 Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. 8 Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.”
9 Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. 10 Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. 11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.”
Mtume Mpya Achaguliwa
12 Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja[a] kutoka Yerusalemu. 13 Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo).
14 Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume.
15 Baada ya siku chache waamini waliokuwa kama mia moja na ishirini walikutana pamoja. Petro alisimama na kusema, 16-17 “Kaka na dada zangu, katika Maandiko Roho Mtakatifu alisema kupitia Daudi kwamba jambo fulani lazima litatokea. Alizungumza kuhusu Yuda, yule aliyekuwa katika kundi letu wenyewe. Yuda alihudumu pamoja nasi. Roho alisema Yuda atawaongoza watu kumkamata Yesu.”
18 (Kwa kufanya hili Yuda alilipwa pesa. Alinunulia shamba pesa hizo. Lakini aliangukia kichwa chake, mwili wake ukapasuka, na matumbo yake yote yakamwagika nje. 19 Na watu wote wa Yerusalemu wanalijua hili. Ndiyo maana waliliita shamba hilo Akeldama, ambalo maana yake kwa Kiaramu ni “Shamba la Damu”.)
20 Petro akasema, “Katika kitabu cha Zaburi, jambo hili limeandikwa kuhusu Yuda:
‘Watu wasipakaribie mahali pake;
Yeyote asiishi hapo.’(A)
Pia imeandikwa kuwa:
‘Mtu mwingine achukue kazi yake.’(B)
21-22 Hivyo ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi ili awe shahidi wa ufufuo wa Bwana Yesu. Ni lazima awe mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana Yesu alipokuwa pamoja nasi. Ni lazima awe yule ambaye amekuwa pamoja nasi tangu Yohana alipokuwa anabatiza watu mpaka siku ambayo Bwana Yesu alichukuliwa kutoka kwetu na kwenda mbinguni.”
23 Kisha waliwasimamisha watu wawili mbele ya kundi. Mmoja aliitwa Yusufu Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto. Mwingine aliitwa Mathiasi. 24-25 Wakaomba wakisema, “Bwana unajua mioyo ya watu wote. Tuonyeshe kati ya watu hawa wawili uliyemchagua kufanya kazi hii. Yuda aliiacha na kuifuata njia yake. Bwana tuonyeshe ni nani achukue sehemu yake kama mtume!” 26 Kisha wakapiga kura kumchagua mmoja kati ya watu hao wawili. Kura ikaonesha Mathiasi ndiye Bwana anamtaka. Hivyo akawa mtume pamoja na wale wengine kumi na moja.
© 2017 Bible League International