M’Cheyne Bible Reading Plan
22 Malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, ulikuwa anga'avu kama kioo. Mto hutiririka kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2 Hutiririka kupitia katika mtaa mkuu wa mji. Mti wa uzima[a] uko kila upande wa mto, na huzaa tunda kila mwezi, mara kumi na mbili kwa mwaka. Majani ya mti ni kwa ajili ya kutibu mataifa.
3 Katika mji ule hakuna mtu au kitu kitakachokuwa chini ya laana ya Mungu tena. Kiti cha ufalme cha Mungu na Mwanakondoo vitakuwa ndani ya mji. Watumishi wa Mungu watamwabudu yeye. 4 Watauona uso wake. Jina la Mungu litaandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Hakutakuwa usiku tena. Watu hawatahitaji mwanga wa taa au mwanga wa jua. Bwana Mungu atawapa mwanga. Watatawala kama wafalme milele na milele.
6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminiwa. Bwana, Mungu awavuviaye manabii, amemtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni: 7 ‘Sikiliza, Naja upesi! Heri anayetii maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.’”
8 Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. 9 Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. 11 Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri walioosha kanzu zao.[b] Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake. 15 Nje ya mji ni kwa ajili wale waishio kama mbwa; wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wapendao kudanganya na kujifanya wema.
16 Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.”
17 Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka.
18 Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.
Yesu Awatokea wafuasi Wake Saba
21 Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: 2 Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. 3 Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.”
Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu.
4 Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. 5 Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?”
Wao wakajibu, “Hapana.”
6 Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua.
7 Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. 8 Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100[a] tu. 9 Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. 10 Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua.
11 Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. 13 Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia.
14 Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
Yesu Azungumza na Petro
15 Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo[b] wangu.”
16 Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.”
17 Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!”
Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. 18 Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako,[c] na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” 19 (Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka na kumwona yule mfuasi mwingine aliyependwa sana na Yesu akitembea nyuma yao. (Huyu alikuwa ni mfuasi aliyejilaza kwa Yesu wakati wa chakula cha jioni na kusema, “Bwana, ni nani atakayekusaliti kwa maadui zako?”) 21 Petro alipomwona nyuma yao, akamwuliza Yesu, “Bwana, vipi kuhusu yeye?”
22 Yesu akajibu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali. Wewe nifuate!”
23 Kwa hiyo habari ikaenea miongoni mwa wafuasi wa Yesu. Wao walikuwa wakisema kuwa mfuasi huyo asingekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa asingekufa. Yeye alisema tu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali.”
24 Huyo mfuasi ndiye yeye anayesimulia habari hizi. Ndiye ambaye sasa ameziandika habari zote hizi. Nasi tunajua kuwa anayoyasema ni kweli.
25 Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu. Kama kila moja ya hayo yote yangeandikwa, nafikiri ulimwengu wote usingevitosha vitabu ambavyo vingeandikwa.
© 2017 Bible League International