Daily Reading for Personal Growth, 40 Days with God
8 Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. 2 Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha.
3 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. 4 Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. 5 Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je, Unasema tufanye nini?”
6 Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. 7 Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” 8 Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo.
9 Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10 Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” 11 Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.”[a]
Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.”
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”
13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”
14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”
19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”
Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”
© 2017 Bible League International