Beginning
Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu
(Mt 3:1-12; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)
1 Mwanzo wa Habari Njema za Yesu Masihi,[a] Mwana wa Mungu,[b] 2 zilianza kama vile Nabii Isaya alivyosema zitaanza, aliandika,
“Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.”(A)
3 “Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(B)
4 Naye Yohana akaja, akiwabatiza watu huko nyikani huku akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. 5 Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.
6 Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi.
7 Yeye alitangaza yafuatayo: “Yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.[c] 8 Mimi nawabatiza katika maji, lakini yeye huyo atawabatiza katika Roho Mtakatifu.”
Yohana Ambatiza Yesu
(Mt 3:13-17; Lk 3:21-22)
9 Ikatokea katika siku hizo Yesu alikuja toka Nazareti uliokuwa mji wa Galilaya akabatizwa na Yohana katika mto Yordani. 10 Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, Yesu aliona mpasuko ukitokea angani, akamwona Roho akishuka chini kuja kwake kama njiwa. 11 Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”
Yesu Ajaribiwa na Shetani
(Mt 4:1-11; Lk 4:1-13)
12 Kisha baada ya kutokea mambo haya Roho Mtakatifu alimchukua Yesu na kumpeleka nyikani,[d] 13 naye akawa huko kwa siku arobaini, ambapo alijaribiwa na Shetani. Yesu alikuwa nyikani pamoja na wanyama wa porini, na malaika walimhudumia.
Yesu Aanza Kazi yake Galilaya
(Mt 4:12-17; Lk 4:14-15)
14 Baada ya Yohana kuwekwa gerezani, Yesu akaja katika wilaya karibu na Ziwa Galilaya, huko aliwatangazia watu Habari Njema kutoka kwa Mungu. 15 Akasema, “Wakati umefika. Ufalme wa Mungu umewafikia.[e] Mbadili mioyo yenu na maisha yenu, na kuiamini habari njema!”
Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi
(Mt 4:18-22; Lk 5:1-11)
16 Alipokuwa akitembea kando kando ya Ziwa Galilaya, Yesu alimwona Simoni[f] na Andrea ndugu yake. Hao walikuwa wavuvi na walikuwa wakizitupa nyavu zao ziwani kukamata samaki. 17 Yesu akawaambia, “njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine, nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 18 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata.
19 Kisha Yesu akaendelea mbele kidogo na akawaona ndugu wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na kaka yake Yohana. Yesu aliwaona wakiwa kwenye mashua wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. 20 Naye akawaita mara moja. Hivyo wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua na watu waliowaajiri na kumfuata Yesu.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu
(Lk 4:31-37)
21 Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. 22 Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[g] 23 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, 24 “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”
25 Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” 26 Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka.
27 Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)
29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.
32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[h]
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Lk 4:42-44)
35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)
40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”
41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[i] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.
43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[j] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[k] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mt 9:1-8; Lk 5:17-26)
2 Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. 2 Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, 3 baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. 4 Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini[l] kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. 5 Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.”
6 Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, 7 “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.”
8 Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? 9 Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? 10 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? 11 Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’”
12 Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!”
Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu
(Mt 9:9-13; Lk 5:27-32)
13 Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. 14 Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata.
15 Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. 16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?”
17 Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mt 9:14-17; Lk 5:33-39)
18 Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.”
19 Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga.
21 Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. 22 Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani[m] vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.”
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)
23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”
25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”
27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
3 Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2 Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[n] ili wapate sababu ya kumshitaki. 3 Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4 Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5 Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6 Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
Wengi Wamfuata Yesu
7 Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, 8 Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.
9 Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10 Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12 Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.
Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili
(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)
13 Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15 Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16 Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:
Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,
17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,
18 Andrea,
Filipo,
Bartholomayo,
Mathayo,
Thomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Thadayo,
Simoni Mzelote
19 na Yuda Iskariote,[o] ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)
20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.
22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[p] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”
23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.
27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.
28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”
30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)
31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[q] nje wanakusubiri.”
33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”
© 2017 Bible League International