Beginning
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Lk 7:18-35)
11 Yesu alipomaliza maelekezo haya kwa wafuasi wake kumi na wawili wa karibu, aliondoka mahali pale. Akaenda katika miji ya Galilaya kuwafundisha watu na kuwaeleza ujumbe wa Mungu.
2 Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. 3 Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”
4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: 5 Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. 6 Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”
7 Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? 8 Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. 9 Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)
11 Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. 12 Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu.[a] 13 Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. 14 Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. 15 Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!
16 Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine,
17 ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliimba wimbo wa maziko,
lakini hamkuhuzunika.’
18 Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 19 Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.”
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Lk 10:13-15)
20 Kisha Yesu akaanza kuikosoa miji ambako alifanya miujiza yake mingi. Aliikosoa miji hii kwa sababu watu katika miji hii hawakubadili maisha yao na kuacha kutenda dhambi. 21 Yesu alisema, “Itakuwa vibaya kwako Korazini! Itakuwa vibaya kwako Bethsaida![b] Ikiwa miujiza hii hii ingetokea Tiro na Sidoni,[c] watu huko wangeshabadili maisha yao kitambo. Wangekwishavaa magunia na kujimwagia majivu kuonesha kuwa wanasikitikia dhambi zao. 22 Lakini ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya zaidi kwako kuliko Tiro na Sidoni.
23 Nawe Kapernaumu, utakwezwa mpaka mbinguni? Hapana! Utatupwa chini mpaka Kuzimu. Nimetenda miujiza mingi ndani yako. Iwapo miujiza hii ingetokea Sodoma,[d] watu huko wangeacha kutenda dhambi na ungekuwa bado ni mji hata leo. 24 Lakini ninakuambia, itakuwa vibaya kwako siku ya hukumu kuliko Sodoma.”
Yesu Awapa Pumziko Watu Wake
(Lk 10:21-22)
25 Kisha Yesu akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbinguni na duniani. Ninashukuru kwa sababu umeyaficha mambo haya kwa wale wanaofikiri kuwa ni wenye hekima na werevu sana. Lakini umeyaonesha haya kwa watu walio kama watoto wadogo.[e] 26 Ndiyo, Baba, ulifanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulivyotaka kufanya.
27 Baba yangu amenipa kila kitu. Hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba peke yake. Na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana ndiye anayemjua Baba. Na watu pekee watakaomjua Baba ni wale ambao Mwana atachagua kuwaonesha.
28 Njooni kwangu ninyi nyote mliochoka kutokana na mizigo mizito mnayolazimishwa kubeba. Nitawapa pumziko. 29 Chukueni nira yangu,[f] jifunzeni kutoka kwangu. Mimi ni mwema na mnyenyekevu katika roho. Nanyi mtaweza kupumzika. 30 Ndiyo, nira yangu ni rahisi. Mzigo ninaowapa muubebe ni mwepesi.”
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mk 2:23-28; Lk 6:1-5)
12 Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. 2 Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.”
3 Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. 4 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. 5 Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. 6 Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. 7 Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’(B) Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya.
8 Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mk 3:1-6; Lk 6:6-11)
9 Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. 10 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11 Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. 12 Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.”
13 Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. 14 Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu.
Yesu ni Mtumishi Aliyechaguliwa na Mungu
15 Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, 16 lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. 17 Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu:
18 “Hapa ni mtumishi wangu,
niliyemchagua.
Ndiye ninayempenda,
na ninapendezwa naye.
Nitamjaza Roho yangu,
naye ataleta haki kwa mataifa.
19 Hatabishana au kupiga kelele;
hakuna atakayesikia sauti yake mitaani.
20 Hatavunja wala kupindisha unyasi.
Hatazimisha hata mwanga hafifu.
Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi.
21 Watu wote watatumaini katika yeye.”(C)
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mk 3:20-30; Lk 11:14-23; 12:10)
22 Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. 23 Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!”
24 Mafarisayo waliposikia hili, walisema, “Mtu huyu anatumia nguvu za Shetani[g] kufukuza mashetani kutoka kwa watu. Beelzebuli ni mtawala wa mashetani.”
25 Yesu alijua kile Mafarisayo walikuwa wanafikiri. Hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe utateketezwa. Na kila mji au familia iliyogawanyika haiwezi kuishi. 26 Hivyo ikiwa Shetani anayafukuza mashetani[h] yake mwenyewe, anapigana kinyume chake yeye mwenyewe, na ufalme wake hautaishi. 27 Mnasema kuwa ninatumia nguvu za Shetani kuyatoa mashetani. Ikiwa hiyo ni kweli, sasa ni nguvu gani watu wenu hutumia wanapoyafukuza mashetani? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa mmekosea. 28 Lakini ninatumia nguvu ya Roho wa Mungu kuyafukuza mashetani, na hili linaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu. 29 Watu wowote wanaotaka kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake lazima wamfunge kwanza. Kisha wanaweza kuiba vitu kutoka katika nyumba yake. 30 Yeyote ambaye hayuko pamoja nami yu kinyume nami. Na yeyote ambaye hakusanyi pamoja nami hutawanya.
31 Hivyo ninawaambia, Mungu atawasamehe watu kila dhambi wanayotenda au kila jambo baya wanalosema kinyume naye. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Unaweza kusema kinyume na Mwana wa Adamu na ukasamehewa. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa; si sasa au baadaye.
Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo
(Lk 6:43-45)
33 Ikiwa unataka matunda mazuri, ni lazima uutunze mti vizuri. Ikiwa mti wako siyo mzuri, utakuwa na matunda mabaya. Mti unajulikana kutokana na aina ya matunda inaozalisha. 34 Ninyi nyoka! Ni waovu sana. Mnawezaje mkasema chochote kilicho chema? Kile ambacho watu husema kwa midomo yao kinatoka katika yale yaliyojaa katika mioyo yao. 35 Walio wema wana vitu vizuri vilivyotunzwa katika mioyo yao. Ndiyo maana husema mambo mazuri. Lakini wale walio waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu husema mambo maovu. 36 Ninawaambia kuwa kila mmoja atajibu kwa ajili ya mambo yasiyo ya maana waliyosema. Hili litatokea siku ya hukumu. 37 Maneno yenu yatatumika kuwahukumu ninyi. Uliyosema yataamua ikiwa una haki mbele za Mungu au unahukumiwa na Mungu.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-12; Lk 11:29-32)
38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjibu Yesu. Wakasema, “Mwalimu, tunataka kukuona ukifanya miujiza kama ishara kuwa unatoka kwa Mungu.”
39 Yesu akajibu, “Watu wenye dhambi na wasio na imani hutafuta kuona muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika kudhibitisha chochote kwao. Yona[i] ni ishara pekee itakayotolewa kwenu ninyi mlio wa kizazi kiovu cha leo. 40 Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu, mchana na usiku. Vivyo hivyo, Mwana wa Adamu atakuwa kaburini kwa siku tatu, mchana na usiku. 41 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi leo mtalinganishwa na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha namna mlivyokosea. Kwa nini ninasema hivi? Kwa sababu Yona alipowahubiri watu hao, walibadili maisha yao. Na aliye mkuu kuliko Yona, yupo hapa lakini mnakataa kubadilika!
42 Pia, siku ya hukumu, Malkia wa Kusini[j] atasimama pamoja na wale wanaoishi sasa, atasababisha mhukumiwe kuwa na makosa. Ninasema hivi kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana kuja kusikiliza mafundisho yenye hekima ya Sulemani. Nami Ninawaambia aliye mkuu zaidi ya Sulemani yuko hapa, lakini hamnisikii!
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Lk 11:24-26)
43 Roho chafu inapotoka kwa mtu, husafiri katika sehemu kavu ikitafuta mahali pa kupumzika, lakini haipati mahali pa kupumzika. 44 Inapokosa mahali pa kupumzika, husema, ‘Nitarudi katika nyumba niliyotoka.’ Inaporudi, ikakuta nyumba hiyo bado ni tupu, ikiwa safi na nadhifu, 45 hutoka nje na kuleta roho zingine saba zilizo chafu zaidi yake. Huingia na kuishi humo, na mtu huyo anakuwa na matatizo mengi kuliko mwanzo wakati roho chafu moja iliishi ndani yake. Ndivyo ilivyo kwa kizazi hiki cha watu wanaoishi leo.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mk 3:31-35; Lk 8:19-21)
46 Yesu alipokuwa akiongea na watu, mama yake na ndugu zake walikuwa nje. Walitaka kuongea naye. 47 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na wadogo zako wanakusubiri nje. Wanataka kuongea nawe.”
48 Yesu akajibu, “Mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni nani?” 49 Kisha akanyoosha kidole kwa wafuasi wake na akasema, “Unaona! Watu hawa ni mama yangu na ndugu zangu. 50 Kaka yangu, dada yangu na mama yangu halisi ni yule afanyaye yale Baba yangu wa mbinguni anataka.”
© 2017 Bible League International