Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yohana 11-12

Kifo cha Lazaro

11 Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. (Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.”

Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.”

Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?”

Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru[a] inayomwongoza.”

11 Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.”

12 Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” 13 Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki.

14 Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. 15 Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.”

16 Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.”

Yesu Akiwa Bethania

17 Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. 18 Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu[b] kutoka Yerusalemu. 19 Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro.

20 Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. 21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. 22 Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.”

23 Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.”

24 Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.”

25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo. Mimi ndiye uzima. Kila anayeniamini atakuwa na uzima, hata kama atakufa. 26 Kila atakayeniamini hatakufa kiroho hata kama atakufa kimwili. Je, Martha, unaliamini jambo hili?”

27 Martha akajibu, “Ndiyo Bwana naliamini. Nakuamini kwamba wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu. Ndiwe unayekuja ulimwenguni.”

Yesu Alia

28 Baada ya Martha kusema maneno haya, alirejea kwa Mariamu dada yake. Aliongea naye peke yake na kusema, “Mwalimu yupo hapa. Anakutafuta.” 29 Mariamu aliposikia hivyo, aliinuka na kwenda haraka kwa Yesu. 30 Yesu hakuwa amefika kijijini. Alikuwa bado yupo pale pale Martha alipomkuta. 31 Wayahudi waliokuwepo nyumbani hapo wakimfariji Mariamu walimwona akiinuka na kuondoka ghafla. Walifikiri alikuwa anaenda kaburini kuomboleza. Hivyo wakamfuata. 32 Mariamu alienda pale Yesu alipokuwa. Naye baada ya kumwona, aliinama miguuni pake Yesu na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, kaka yangu asingekufa.”

33 Ndipo Yesu alipomwona Mariamu na watu waliokuwa pamoja naye wakilia, akahuzunika na kusikitika sana. 34 Akawauliza, “Mmemweka wapi?”

Wakasema, “Bwana, njoo uone.”

35 Yesu akalia na kutoa machozi.

36 Na Wayahudi wakasema, “Angalia! Alikuwa anampenda sana Lazaro!”

37 Lakini wengine wao wakasema, “Yesu aliyeyaponya macho ya yule mtu asiyeona kwa nini hakumsaidia Lazaro na kumzuia asife?”

Yesu Amfufua Lazaro Kutoka Mautini

38 Akiwa bado ana uchungu na kusikitika sana, Yesu akaenda kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa ni pango lenye jiwe kubwa lililofunika pa kuingilia. 39 Yesu akasema, “Lisogezeni pembeni hilo jiwe.”

Martha akasema, “Lakini, Bwana, ni siku nne[c] sasa tangu Lazaro alipofariki. Kutakuwa na harufu mbaya.” Martha alikuwa ni dada wa marehemu.

40 Kisha Yesu akamwambia Martha, “Unakumbuka jinsi nilivyokuambia? Je, sikukuambia kwamba kama ukiamini, ungeuona utukufu wa Mungu?”

41 Kwa hiyo wakalisogeza lile jiwe kutoka kwenye sehemu ya kuingilia. Kisha Yesu akatazama juu na kusema, “Baba, Nakushukuru kwa kuwa ulinisikia. 42 Najua kuwa siku zote unanisikia. Lakini nimeyasema mambo haya kwa ajili ya watu walioko hapa. Nataka kwamba waweze kuamini kuwa ni wewe uliyenituma.” 43 Baada ya Yesu kusema hivi akaita kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!” 44 Yule mtu aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa sanda. Uso wake ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa.

Yesu akawaambia watu, “Mfungueni hizo sanda na kumwacha aende.”

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Lk 22:1-2)

45 Walikuwepo Wayahudi wengi waliokuja kumtembelea Mariamu. Hawa walipoona aliyotenda Yesu, wengi wao wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwapa habari ya mambo aliyofanya Yesu. 47 Kisha viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaitisha kikao cha baraza kuu. Wakasema, “Tutafanyaje? Mtu huyu anafanya ishara nyingi sana. 48 Tukimwacha aendelee kufanya hivi, kila mtu atamwamini. Ndipo Warumi watakuja na kulichukua Hekalu na Taifa letu pia.”

49 Mmoja wa watu wale alikuwa ni Kayafa. Yeye alikuwa kuhani mkuu kwa mwaka ule. Akasema, “Ninyi hamjui lo lote! 50 Ni bora mtu mmoja akafa kwa ajili ya watu wengine badala ya taifa zima kuangamia. Ninyi bado hamjalitambua hili.”

51 Kayafa hakufikiri hivi peke yake. Hakika kama kuhani mkuu kwa mwaka ule, alikuwa akitabiri kwamba Yesu angekufa kwa ajili ya Wayahudi. 52 Kweli, angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Lakini pia angekufa kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika ulimwenguni pote. Angekufa ili awakusanye na kuwaweka katika kundi moja.

53 Siku ile viongozi wa Wayahudi wakaanza kupanga jinsi ya kumuua Yesu. 54 Hivyo Yesu akaacha kusafiri wazi wazi katikati ya Wayahudi. Akaelekea katika mji ulioitwa Efraimu uliokuwa kwenye eneo karibu na jangwa. Akakaa huko pamoja na wafuasi wake.

55 Wakati huo Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Watu wengi kutoka katika nchi yote ya Uyahudi wakaenda Yerusalemu siku chache kabla. Walienda kujitakasa tayari kwa ajili ya sikukuu hiyo. 56 Watu wakamtafuta Yesu. Nao walisimama katika maeneo ya Hekalu na kuulizana, “Je, naye atakuja kwenye sikukuu? Unafikirije wewe?” 57 Lakini viongozi wa makuhani na Mafarisayo walitoa agizo maalumu kuhusu Yesu. Walisema kuwa mtu yeyote anayejua mahali alipo Yesu awaambie ili waweze kumkamata.

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)

12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita[d] hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.

Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka[e] wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.

Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini.[f] Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”

Mpango Dhidi ya Lazaro

Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. 10 Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro. 11 Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu.

Yesu Anaingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Lk 19:28-40)

12 Siku iliyofuata watu waliokuwamo Yerusalemu walisikia kwamba Yesu alikuwa anakuja huko. Hili ni kundi la watu waliokuja kusherehekea sikukuu ya Pasaka. 13 Hawa walibeba matawi ya miti ya mitende na kwenda kumlaki Yesu. Pia walipiga kelele wakisema,

“‘Msifuni[g] Yeye!’
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
    ajaye kwa jina la Bwana!’(A)
Mungu ambariki Mfalme wa Israeli!”

14 Yesu akamkuta punda njiani naye akampanda, kama vile Maandiko yanavyosema,

15 “Msiogope, enyi watu wa Sayuni![h]
Tazameni! Mfalme wenu anakuja.
    Naye amepanda mwana punda.”(B)

16 Wafuasi wa Yesu hawakuyaelewa yale yaliyokuwa yanatokea wakati huo. Lakini Yesu alipoinuliwa juu kwenye utukufu, ndipo walipoelewa kuwa haya yalitokea kama ilivyoandikwa juu yake. Kisha wakakumbuka kwamba walifanya mambo haya kwa ajili ya Yesu.

17 Siku Yesu alipomfufua Lazaro kutoka wafu na kumwambia atoke kaburini walikuwepo watu wengi pamoja naye. Hawa walikuwa wakiwaeleza wengine yale aliyoyafanya Yesu. 18 Ndiyo sababu watu wengi walienda ili kumlaki Yesu; kwa kuwa walikuwa wamesikia habari za ishara hii aliyoifanya. 19 Mafarisayo nao wakasemezana wao kwa wao, “Tazameni! Mpango wetu haufanyi kazi. Watu wote wanamfuata Yesu!”

Yesu Azungumza Juu Uzima na Kifo

20 Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka. 21 Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.” 22 Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu.

23 Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake. 24 Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja. 25 Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele. 26 Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu.

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

27 Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je, niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso. 28 Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!”

Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.”

29 Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!”

30 Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu. 31 Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu[i] huu atatupwa nje. 32 Nami nitainuliwa juu[j] kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa.

34 Watu wakasema, “Lakini sheria yetu inasema kwamba Masihi ataishi milele. Sasa kwa nini unasema, ‘Ni lazima Mwana wa Adamu ainuliwe juu’? Ni nani huyu ‘Mwana wa Adamu’?”

35 Kisha Yesu akasema, “Nuru[k] itabaki pamoja nanyi kwa muda mfupi tu. Kwa hiyo mtembee mkiwa bado na hiyo nuru. Hapo giza[l] halitaweza kuwakamata. Watu wanaotembea gizani hawajui kule wanakoenda. 36 Hivyo wekeni matumaini yenu katika nuru wakati bado mkiwa nayo. Jinsi hiyo mtakuwa watoto wa nuru.” Yesu alipomaliza kusema mambo hayo, aliondoka na kwenda mahali ambapo watu wasingeweza kumwona.

Baadhi ya Wayahudi Wakataa Kumwamini Yesu

37 Watu wakaona ishara[m] hizi zote alizozifanya Yesu, lakini bado hawakumwamini. 38 Haya yalikuwa hivyo ili kuthibitisha yale aliyoyasema nabii Isaya kuwa:

“Bwana, ni nani aliyeamini yale tuliyowaambia?
    Ni nani aliyeziona nguvu za Bwana?”(C)

39 Hii ndiyo sababu watu hawakuweza kuamini. Kwani Isaya alisema pia,

40 “Mungu aliwafanya baadhi ya watu wasione.
    Aliufunga ufahamu wao.
Alifanya hivi ili wasiweze kuona kwa macho yao
    na kuelewa kwa ufahamu wao.
Alifanya hivyo ili wasiweze kugeuka
    na kuponywa.”(D)

41 Isaya alisema hivi kwa sababu aliuona ukuu wa Mungu[n] ndani ya Yesu. Naye alizungumza habari zake Yesu.

42 Lakini watu wengi wakamwamini Yesu. Hata wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi wakamwamini, lakini walikuwa na hofu juu ya Mafarisayo, hivyo hawakusema kwa uwazi kwamba wameamini. Hao walikuwa na hofu kwamba wangeamriwa watoke na kukaa nje ya sinagogi. 43 Wao walipenda kusifiwa na watu zaidi kuliko kupata sifa zinazotoka kwa Mungu.

Mafundisho ya Yesu Yatawahukumu Watu

44 Kisha Yesu akapaza sauti, “Mtu yeyote anayeniamini basi kwa hakika anamwamini yule aliyenituma. 45 Yeyote anayeniona mimi hakika anamwona yeye aliyenituma. 46 Nimekuja katika ulimwengu huu kama mwanga. Nimekuja ili kila mmoja atakayeniamini asiendelee kuishi katika giza.

47 Sikuja ulimwenguni humu kuwahukumu watu. Nimekuja ili kuwaokoa watu wa ulimwengu huu. Hivyo mimi siye ninayewahukumu wale wanaosikia mafundisho yangu bila kuyafuata. 48 Isipokuwa yupo hakimu wa kuwahukumu wote wanaokataa kuniamini na wasiokubaliana na yale ninayoyasema. Ujumbe ninaousema utawahukumu ninyi siku ya mwisho. 49 Hiyo ni kwa sababu yale niliyofundisha hayakutoka kwangu. Baba aliyenituma ndiye aliyeniambia yale nitakayosema na kuyafundisha. 50 Nami najua amri za Mungu kwamba lolote alisemalo na kutenda litawaletea watu uzima wa milele, kama watazifanya. Hivyo mambo ninayosema ni yale ambayo Baba yangu ameniambia niyaseme.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International