Book of Common Prayer
Petro akiwa Lida na Yafa
32 Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini[a] walioishi Lida. 33 Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35 Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[b] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
56 Kisha wakaenda kuandaa manukato yanayonukia vizuri ili kuupaka mwili wa Yesu.
Siku ya Sabato walipumzika, kama ilivyoamriwa katika Sheria ya Musa.
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Yh 20:1-10)
24 Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. 2 Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. 3 Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4 Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. 5 Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. 6 Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? 7 Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” 8 Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema.
9 Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. 10 Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. 11 Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi.
© 2017 Bible League International