Book of Common Prayer
14 Lakini watu watawezaje kumwita Bwana na kupata msaada wake ikiwa hawamwamini yeye? Na watawezaje kumwamini Bwana ikiwa hawajawahi kuzisikia habari zake? Na watawezaje kuzisikia habari zake ikiwa hayupo mtu wa kuwaambia? 15 Na mtu atawezaje kwenda na kuwaambia habari hizo ikiwa hajatumwa? Haya, hii ndiyo sababu Maandiko yanasema, “Ni jambo la kufurahisha kumwona mtu anayepeleka Habari Njema!”(A)
16 Lakini si watu wote walizipokea Habari Njema hizo. Na hii ndiyo sababu Isaya alisema, “Bwana, nani aliyeamini yale tuliyowaeleza?”(B) 17 Kwa hiyo imani hupatikana kutokana na kusikia Habari Njema. Na watu husikia Habari Njema wakati mtu anapowaeleza kuhusu Kristo.
18 Lakini nauliza, “Je, watu hao walizisikia Habari Njema?” Ndio Kwa kweli walizisikia kama Maandiko yanavyosema,
“Sauti zao zilitoka na kuenea duniani kote.
Maneno yao yakaenda kila mahali ulimwenguni.”(C)
19 Lakini tena nauliza, “Je, watu wa Israeli hawakuelewa?” Ndiyo, walielewa. Musa alikuwa wa kwanza kujibu swali hili. Na anasema haya kwa ajili ya Mungu:
“Nitawatumia wale ambao siyo Taifa halisi ili liwafanye muone wivu.
Nitalitumia taifa ambalo halielewi ili mkasirike.”(D)
20 Kisha Isaya ana ujasiri wa kutosha kusema haya kwa ajili ya Mungu:
“Watu walionipata mimi hawakuwa wakinitafuta.
Nilijitambulisha kwa watu ambao hawakuwa wakinitafuta.”(E)
21 Lakini kuhusu watu wa Israeli Mungu anasema,
“Kutwa nzima nilisimama nikiwa tayari kuwakubali watu hawa,
lakini ni wakaidi na wamekataa kunitii.”(F)
Mchungaji na Kondoo Wake
10 Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. 2 Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. 3 Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. 4 Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. 5 Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.”
6 Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
© 2017 Bible League International