Book of Common Prayer
13 Maandiko yanasema, “Niliamini, hivyo nikasema.”(A) Tuna Roho huyo huyo anayetupa imani kama hiyo. Tunaamini, na hivyo tunasema pia. 14 Mungu alimfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, nasi tunajua kuwa atatufufua pamoja na Yesu. Mungu atatukusanya pamoja nanyi, na tutasimama mbele zake. 15 Mambo yote haya ni kwa ajili yenu. Na hivyo neema ya Mungu inatolewa kwa watu wengi zaidi na zaidi. Hili litaleta shukrani nyingi zaidi na utukufu kwa Mungu.
Kuishi kwa Imani
16 Hii ndiyo sababu hatukati tamaa. Miili yetu inazidi kuzeeka na kuchoka, lakini roho zetu ndani zinafanywa upya kila siku. 17 Tuna masumbufu, lakini ni madogo na ni ya muda mfupi. Na masumbufu haya yanatusaidia kuupata utukufu wa milele ulio mkuu kuliko masumbufu yetu. 18 Hivyo twafikiri juu ya mambo tusiyoweza kuyaona, si tunayoona. Tunayoyaona ni ya kitambo tu, na yale tusiyoyaona yanadumu milele.
5 Tunafahamu kuwa miili yetu, ambayo ni hema tunaloishi ndani yake hapa duniani itaharibiwa. Hilo litakapotokea, Mungu atakuwa na nyumba tayari kwa ajili yetu kuishi ndani yake. Haitakuwa nyumba kama ambayo watu hujenga hapa duniani. Itakuwa nyumba ya mbinguni itakayodumu milele. 2 Lakini wakati bado tunaishi katika miili hii, tunaugua kwa sababu tuna shauku kubwa mbele za Mungu ya kutupa mwili wetu mpya wa mbinguni ili tuweze kujivika. 3 Tutauvaa mwili wa mbinguni kama vazi jipya na hatutakuwa uchi. 4 Tunapoishi katika “hema” hili la kidunia, tunaugua na kuelemewa na mizigo. Lakini, hiyo si kwa sababu tunataka kuivua miili hii ya zamani. Hapana, ni kwa sababu tunataka kuivaa miili yetu mipya. Kisha mwili huu unao kufa utafunikwa na uzima. 5 Hii ndiyo sababu Mungu mwenyewe ndiye aliyetuandaa kwa kusudi hili hasa. Na ametupata Roho kama malipo ya awali kutuhakikishia maisha yajayo.
6 Hivyo tuna ujasiri daima. Tunafahamu kuwa tunapoendelea kuishi katika mwili huu, tunakuwa mbali na makao yetu pamoja na Bwana. 7 Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona. 8 Hivyo ninasema tuna ujasiri. Na tungependa kuondoka na kutokuwa katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana. 9 Lengo letu pekee ni kumpendeza Bwana, kwamba tupo nyumbani au mbali. 10 Tutasimama sote mbele za Kristo ili tuhukumiwe. Kila mtu atalipwa anachostahili. Kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake, mazuri au mabaya, alipoishi katika mwili huu wa kidunia.
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
6 Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2 Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3 Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] 4 Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5 Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6 Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
7 Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. 8 Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. 9 Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako lipewe utukufu.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11 Utupe leo chakula tunachohitaji.
12 Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13 Usiruhusu tukajaribiwa,
lakini utuokoe na Yule Mwovu.’[c]
14 Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15 Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote.
© 2017 Bible League International