Book of Common Prayer
Yesu Ni Mkuu Kuliko Musa
3 Hivyo, kaka na dada zangu, ninyi mliochaguliwa na Mungu muwe watu wake watakatifu, mfikirieni Yesu. Yeye ndiye tunayeamini kuwa Mungu alimtuma kuja kutuokoa na awe kuhani wetu mkuu. 2 Mungu akamfanya kuhani wetu mkuu, naye akawa mwaminifu kwa Mungu kama Musa alivyokuwa. Naye alifanya kila kitu ambacho Mungu alimtaka akifanye katika nyumba ya Mungu. 3 Mtu anapojenga nyumba, watu watamheshimu mjenzi zaidi kuliko ile nyumba. Ndivyo ilivyo kwa Yesu. Anastahili heshima kubwa kuliko Musa. 4 Kila nyumba huwa imejengwa na mtu fulani, lakini Mungu alijenga kila kitu. 5 Musa alikuwa mwaminifu kama mtumishi katika nyumba yote ya Mungu. Aliwajulisha watu yale ambayo Mungu angeyasema katika siku zijazo. 6 Lakini Kristo ni mwaminifu katika kuitawala nyumba ya Mungu kama Mwana. Nasi tu nyumba ya Mungu, kama tukibaki wajasiri katika tumaini kuu tunalofurahia kusema kuwa tunalo.
25 Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.[a] 26 Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.
27 Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28 Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29 Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30 Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”
© 2017 Bible League International