Book of Common Prayer
Mitume wa Kristo Yesu
4 Tuchukulieni sisi kuwa ni watumishi wa Kristo, ambao Mungu ametuamini tufanye kazi ya kuwaambia wengine siri zake za kweli. 2 Wale walioaminiwa kwa kazi muhimu kama hii imewapasa kuonesha ya kuwa wao ni waaminifu. 3 Lakini siichukulii hukumu yenu kuhusu hili kuwa kitu. Hata hukumu yo yote katika mahakama ya kibinadamu isingekuwa na maana yoyote. Sijihukumu hata mimi mwenyewe. 4 Sikumbuki kosa lolote nililofanya, lakini hiyo hainifanyi mimi kujihesabia haki. Bwana pekee ndiye anayepaswa kunihukumu ikiwa nimefanya vyema au la. 5 Hivyo, msimhukumu mtu yeyote sasa. Hukumu itakuwa wakati Bwana atakaporudi. Ataangaza mwanga kwa kila kitu kilichofichwa gizani. Ataziweka wazi nia za siri za mioyo yetu. Ndipo sifa ambayo kila mtu anapaswa kuipata itatoka kwa Mungu.
6 Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.”[a] 7 Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe?
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)
23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”
25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”
27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
3 Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2 Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. 3 Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4 Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5 Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6 Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
© 2017 Bible League International