Book of Common Prayer
1 Tunataka tuwaambie juu ya Neno[a] linalo toa uzima. Yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Huyu ndiye yule tuliyemsikia na kumwona kwa macho yetu. Tuliyaona mambo aliyeyafanya, na mikono yetu ilimgusa. 2 Ndiyo, yeye aliye uzima alidhihirishwa kwetu. Tulimwona, na hivyo tunaweza kuwaeleza wengine juu yake. Sasa tunawaeleza habari kwamba yeye ndiye uzima wa milele aliyekuwa pamoja na Mungu Baba na alidhihirishwa kwetu. 3 Tuna wasimulia mambo tuliyoyaona na kuyasikia kwa sababu tunawataka muwe na ushirika pamoja nasi. Ushirika tulionao ni pamoja na Mungu Baba na mwanaye Yesu Kristo. 4 Tunawaandikia mambo haya ili furaha yetu iwe kamili.
Mungu Anatusamehe Dhambi Zetu
5 Tulisikia mafundisho ya kweli toka kwa Mungu. Na sasa tunayasimulia kwenu. Mungu ni nuru, na ndani yake hamna giza. 6 Kwa hiyo kama tukisema kuwa tunashirikiana na Mungu, lakini tukaendelea kuishi katika giza, tunakuwa ni waongo, tusioifuata kweli. 7 Tunapaswa kuishi katika nuru, ambamo Mungu yupo. Kama tunaishi katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na sadaka ya damu yake Yesu, Mwana wa Mungu, inatutakasa kila dhambi.
8 Kama tukisema kuwa hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na tumeikataa kweli. 9 Lakini kama tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe. Tunaweza kumwamini Mungu kufanya hili. Kwa sababu Mungu daima hufanya lililo haki. Atatufanya tuwe safi toka kila dhambi tuliyofanya. 10 Kama tukisema kuwa hatujafanya dhambi, tunasema kuwa Mungu ni mwongo na tumeyakana mafundisho yake.
Yesu Amponya Aliyezaliwa Pasipo Kuwa na Uwezo wa Kuona
9 Yesu alipokuwa anatembea, alimwona mtu asiyeona tangu alipozaliwa. 2 Wafuasi wake wakamwuliza, “Mwalimu, kwa nini mtu huyu alizaliwa asiyeona? Dhambi ya nani ilifanya hili litokee? Ilikuwa ni dhambi yake mwenyewe au ya wazazi wake?” 3 Yesu akajibu, “Si dhambi yoyote ya huyo mtu wala ya wazazi wake iliyosababisha awe asiyeona. Alizaliwa asiyeona ili aweze kutumiwa kuonesha mambo makuu ambayo Mungu anaweza kufanya. 4 Kukiwa bado ni mchana, tunapaswa kuendelea kuzifanya kazi zake Yeye aliyenituma. Usiku unakuja, na hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi wakati wa usiku. 5 Nikiwa bado nipo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.”
6 Yesu aliposema haya, akatema mate chini kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka yule asiyeona katika macho yake. 7 Yesu akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni “Aliyetumwa”.) Hivyo mtu yule akaenda katika bwawa lile, akanawa na kurudi akiwa mwenye kuona.
8 Majirani zake na wengine waliomwona akiomba omba wakasema, “Angalieni! Hivi huyu ndiye mtu yule aliyekaa siku zote na kuomba omba?”
9 Wengine wakasema, “Ndiyo! Yeye ndiye.” Lakini wengine wakasema, “Hapana, hawezi kuwa yeye. Huyo anafanana naye tu.”
Kisha yule mtu akasema, “Mimi ndiye mtu huyo.”
10 Wakamwuliza, “Kulitokea nini? Uliwezaje kupata kuona?”
11 Akawajibu, “Mtu yule wanayemwita Yesu alitengeneza tope akayapaka macho yangu. Kisha akaniambia ‘Nenda kanawe kwenye bwawa la Siloamu.’ Hivyo nikaenda kule na kunawa, na ndipo nikaweza kuona.”
12 Wakamwuliza, “Yuko wapi mtu huyo?”
Akajibu, “Mimi sijui aliko.”
Baadhi ya Mafarisayo Wana Maswali
13 Kisha watu wakampeleka huyo mtu kwa Mafarisayo. 14 Siku Yesu alipotengeneza yale matope na kuyaponya macho ya mtu huyo ilikuwa ni Sabato. 15 Hivyo Mafarisayo wakamwuliza huyo mtu, “Uliwezaje kuona?”
Akawajibu, “Alipaka matope katika macho yangu. Nikaenda kunawa, na sasa naweza kuona.”
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyo mtu hatii sheria inayohusu siku ya Sabato. Kwa hiyo hatoki kwa Mungu.”
Wengine wakasema, “Lakini mtu aliye mtenda dhambi hawezi kufanya ishara kama hizi?” Hivyo hawakuelewana wao kwa wao. 17 Wakamuuliza tena huyo mtu, “Kwa vile aliponya macho yako, unasemaje juu ya mtu huyo?”
Akajibu, “Yeye ni nabii.”
© 2017 Bible League International