Book of Common Prayer
Ni lazima Tupendane Sisi kwa Sisi
11 Haya ni mafundisho mliyoyasikia toka mwanzo: Ni lazima tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini. Aliyekuwa upande wa Mwovu. Kaini alimwua ndugu yake. Lakini kwa nini alimwua? Ni kwa sababu alichokifanya Kaini kilikuwa cha kiovu, na alichokifanya nduguye kilikuwa cha haki.
13 Kaka zangu na dada zangu, msishangae watu wa dunia hii wakiwachukia. 14 Tunafahamu ya kuwa tumevuka kutoka mautini na kuingia uzimani. Tunafahamu hili kwa sababu tunapendana sisi kwa sisi kama ndugu wa kike na wa kiume. Yeyote asiyewapenda kaka zake na dada zake angali amekufa. 15 Kila anayemchukia nduguye anayeamini ni muuaji. Nanyi mnajua kuwa hakuna muuaji aliye na uzima wa milele.
16 Hivi ndivyo tunavyojua jinsi upendo wa kweli ulivyo: Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hivyo nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu, kwa ajili ya ndugu wa kike na wa kiume katika familia ya Kristo. 17 Itakuwaje pale muumini tajiri mwenye fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote akamwona dada ama kaka yake aliye maskini na asiye na fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote. Endapo muumini huyu tajiri hatamsaidia muumini yule maskini, basi ni wazi kwamba upendo wa Mungu haumo ndani ya muumini yule tajiri. 18 Watoto wangu, upendo wetu usiwe wa maneno na kuongea tu. Hapana, upendo wetu unapaswa kuwa halisi. Hatuna budi kuuonyesha upendo wetu kwa mambo yale tunayofanya.
Yesu Ajaribiwa na Shetani
(Mt 4:1-11; Mk 1:12-13)
4 Akiwa amejaa Roho Mtakatifu, Yesu akarudi kutoka Mto Yordani. Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza mpaka nyikani 2 kwa muda wa siku arobaini, alikojaribiwa na Ibilisi. Katika muda wote huo hakula chakula chochote na baadaye akahisi njaa sana.
3 Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.”
4 Yesu akamjibu, “Maandiko yanasema, ‘Watu hawataishi kwa mkate tu.’”(A)
5 Kisha mwovu akamchukua Yesu na kwa muda mfupi akamwonyesha falme zote za ulimwengu. 6 Mwovu akamwambia, “Nitakufanya uwe mfalme wa sehemu zote hizi. Utakuwa na mamlaka juu yao, na utapata utukufu wote. Yote yametolewa kwangu. Ninaweza kumpa yeyote kadri ninavyopenda. 7 Nitakupa vyote hivi, ikiwa utaniabudu tu.”
8 Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Ni lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’”(B)
9 Ndipo Shetani akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu na kumweka mahali palipo juu katika mnara wa Hekalu. Akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe! 10 Kwani Maandiko yanasema,
‘Mungu atawaamuru
malaika zake wakulinde.’(C)
11 Pia imeandikwa kuwa,
‘Mikono yao itakudaka,
ili usijikwae mguu wako kwenye mwamba.’”(D)
12 Yesu akajibu, “Pia, Maandiko yanasema: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(E)
13 Shetani alipomaliza kumjaribu Yesu katika namna zote, alimwacha akaenda zake hadi wakati mwingine.
© 2017 Bible League International