Yohana 1-11
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu ni Neno la Mungu la Milele
1 Mwanzoni Kabla ulimwengu haujaumbwa
alikuwepo Neno.[a]
Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu,
na Neno alikuwa Mungu.
2 Alikuwepo pamoja na Mungu
toka mwanzo.
3 Kila kitu kilifanyika kupitia kwake.
Hakuna chochote katika uumbaji wa Mungu
kilichofanyika bila yeye.
4 Ndani yake Neno kulikuwemo na uzima,
na uzima huo ulikuwa nuru
kwa ajili ya watu wa ulimwenguni.
5 Nuru[b] hiyo yamulika gizani,
na giza halikuishinda.[c]
6 Alikuwepo mtu aliyeitwa Yohana, aliyetumwa na Mungu. 7 Alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru. Ili kupitia kwake watu wote waweze kusikia kuhusu yule aliye nuru na wamwamini. 8 Yohana mwenyewe hakuwa nuru. Lakini alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru.
9 Nuru ya kweli,
anayeleta mwangaza kwa watu wote,
alikuwa tayari kuonekana kwa ulimwengu.
10 Huyo Neno alikuwapo tayari ulimwenguni.
Ulimwengu uliumbwa kupitia yeye,
lakini ulimwengu haukumkubali.
11 Alikuja kwa ulimwengu ulio wake,
na watu wake mwenyewe hawakumkubali.
12 Lakini baadhi ya watu walimkubali wakamwamini
na akawapa haki ya kuwa watoto wa Mungu.
13 Ndiyo, walikuwa watoto wa Mungu,
lakini si kwa kuzaliwa kimwili.
Haikuhusisha matamanio
ya kibinadamu.
Mungu mwenyewe aliwafanya
kuwa watoto wake.
14 Neno akafanyika kuwa mwanadamu
na akaishi pamoja nasi.
Tuliouna ukuu wa uungu wake;
utukufu alionao Mwana pekee wa Baba.
15 Yohana alizungumza kuhusu yeye alipopaza sauti na kusema, “Huyu ndiye niliyemzungumzia habari zake niliposema, ‘Anayekuja baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu alikuwepo mwanzoni, zamani kabla sijazaliwa.’”
16 Alikuwa amejaa neema na kweli ya Mungu,
tulipokea kutoka baraka moja
baada ya nyingine[d] kutoka kwake.
17 Hiyo ni kusema kuwa,
sheria ililetwa kwetu kupitia Musa.
Lakini neema na kweli imekuja
kupitia Yesu Kristo.
18 Hakuna aliyewahi kumwona Mungu
isipokuwa Mwana peke yake,
ambaye yeye mwenyewe ni Mungu,
ametuonesha jinsi Mungu alivyo.
Yuko karibu sana na Baba
kiasi kwamba tunapomwona,
tumemwona Mungu.
Yohana Azungumza Juu ya Kristo
(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17)
19 Viongozi wa Kiyahudi kule Yerusalemu walituma baadhi ya makuhani na Walawi kwa Yohana kumwuliza, “Wewe ni nani?” Yohana akawaeleza kweli. 20 Akajibu kwa wazi bila kusitasita, “Mimi siyo Masihi.”
21 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?”
Yohana akawajibu, “Hapana, mimi siye Eliya.”
Wakamwuliza tena, “Je, wewe ni Nabii?”[e]
Naye akawajibu, “Hapana, mimi siyo nabii.”
22 Kisha wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Tueleze habari zako. Tupe jibu la kuwaambia wale waliotutuma. Unajitambulisha mwenyewe kuwa nani?”
23 Yohana akawaambia maneno ya nabii Isaya:
“‘Mimi ni mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
Nyoosheni njia kwa ajili ya Bwana.’”(A)
24 Wale Wayahudi walitoka kwa Mafarisayo. 25 Wakamwambia Yohana, “Unasema kuwa wewe siyo Masihi. Na unasema kuwa wewe siyo Eliya wala nabii. Sasa kwa nini unawabatiza watu?”
26 Yohana akajibu, “Nawabatiza watu kwa maji. Lakini yupo mtu hapa kati yenu ambaye ninyi hamumjui. 27 Yeye ndiye yule anayekuja baada yangu. Nami sina sifa za kuwa mtumwa anayefungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yote yalitokea Bethania iliyokuwa upande mwingine wa Mto Yordani. Hapa ndipo Yohana alipowabatiza watu.
Yesu, Mwanakondoo wa Mungu
29 Siku iliyofuata Yohana akamwona Yesu akija kwake na kusema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu mwenye kuondoa dhambi za ulimwengu.” 30 Huyu ndiye niliyezungumza habari zake niliposema, “Kuna mtu anayekuja baada yangu aliye mkuu zaidi yangu, kwa sababu yeye aliishi muda mrefu kabla ya kuzaliwa kwangu.” 31 Nami sikumjua yeye ni nani. Lakini nilikuja kuwabatiza watu kwa maji ili watu wa Israeli waelewe kuwa huyo ndiye Masihi.
32-34 Kisha Yohana akasema maneno yafuatayo ili kila mtu asikie, “Mimi pia sikujua nani hasa alikuwa Masihi. Lakini yule aliyenituma kubatiza aliniambia, ‘Utamwona Roho akishuka na kutua kwa mtu. Huyo ndiye atakayewabatiza watu kwa Roho Mtakatifu.’ Nami nimeyaona haya yakitokea. Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama njiwa na kutulia juu ya mtu huyu. Hivyo haya ndiyo ninayowaambia watu: ‘Yeye huyo ndiye Mwana wa Mungu.’”[f]
Wafuasi wa Kwanza wa Yesu
35 Siku iliyofuata Yohana alirejea tena mahali hapo pamoja na wafuasi wake wawili. 36 Naye akamwona Yesu akitembea, hivyo akasema, “Angalieni, Mwanakondoo wa Mungu!”
37 Wale wafuasi wake wawili walimsikia Yohana akisema haya, basi wakaondoka na kumfuata Yesu. 38 Yesu aligeuka na kuwaona watu wawili wakimfuata. Akawauliza, “Mnataka nini?” Nao wakajibu wakimwuliza, “Rabi, unakaa wapi?” (Rabi tafsiri yake ni Mwalimu.)
39 Yesu akajibu, “Njooni tufuatane pamoja nanyi mtapaona ninapokaa.” Hivyo wale watu wawili wakaenda pamoja naye. Wakaona mahali alipokuwa anakaa, nao wakashinda huko pamoja naye mchana wote. Hiyo ilikuwa ni saa kumi ya jioni.
40 Watu hawa wakamfuata Yesu baada ya kusikia habari zake kutoka kwa Yohana. Mmoja wao alikuwa Andrea, nduguye Simoni Petro.
41 Kitu cha kwanza alichokifanya Andrea kilikuwa ni kwenda kumtafuta ndugu yake Simoni. Andrea alipompata nduguye akamwambia, “Tumemwona Masihi.” (Masihi tafsiri yake ni Kristo.) 42 Kisha Andrea akamleta Simoni nduguye kwa Yesu. Yesu akamtazama, na kumwambia, “Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yohana. Basi utaitwa Kefa.” (“Kefa” tafsiri yake ni “Petro”.[g])
43 Kesho yake Yesu akaamua kwenda Galilaya. Huko alikutana na Filipo na kumwambia, “Nifuate.” 44 Filipo alikuwa mwenyeji wa mji wa Bethsaida, kama alivyokuwa Andrea na Petro. 45 Filipo akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona mtu ambaye habari zake ziliandikwa na Musa katika sheria. Pia Manabii waliandika habari juu ya mtu huyu. Yeye ni Yesu, mwana wa Yusufu. Naye anatoka mjini Nazareti!”
46 Lakini Nathanaeli akamwambia Filipo, “Nazareti! Je, inawezakana kupata kitu chochote chema kutoka Nazareti?”
Filipo akajibu, “Njoo uone.”
47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na papo hapo akasema, “Mtu huyu anayekuja ni Mwisraeli halisi, ambaye unayeweza kumwamini.”[h]
48 Nathanaeli akamwuliza Yesu, “Umenifahamu kwa namna gani?”
Yesu akamjibu, “Nilikuona pale ulipokuwa chini ya mtini,[i] kabla Filipo hajakueleza habari zangu.”
49 Kisha Nathanaeli akasema, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Nawe ni mfalme wa Israeli.” 50 Yesu akamwambia, “Je, umeyaamini haya kwa sababu nimekwambia kuwa nilikuona chini ya mtini? Utaona mambo makubwa zaidi ya haya.” 51 Kisha akasema, “Mniamini ninapowaambia kwamba mtaziona mbingu zimefunguka. Na mtawaona, ‘Malaika wa Mungu wakipanda juu na kushuka chini’[j] kwa ajili Mwana wa Adamu.”
Arusi Katika Mji wa Kana
2 Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. 2 Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. 3 Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.”
4 Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.”
5 Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.”
6 Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa.[k] Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.[l]
7 Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu.
8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. 9 Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi 10 na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.”
11 Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini.
12 Kisha Yesu akashuka kwenda katika mji wa Kapernaumu. Mama yake, ndugu zake, na wafuasi wake nao walienda pamoja naye. Wote wakakaa huko kwa siku chache.
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-13; Mk 11:15-17; Lk 19:45-46)
13 Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. 14 Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. 15 Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. 16 Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!”
17 Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.”(B)
18 Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.”
19 Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” 20 Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je, ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?”
21 Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu.
23 Yesu alikuwa Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Watu wengi wakamwamini kwa sababu waliona ishara na miujiza alioitenda. 24 Lakini Yesu hakuwaamini wao, kwa sababu alijua jinsi watu wote wanavyofikiri. 25 Hakuhitaji mtu yeyote amwambie jinsi mtu fulani alivyo. Kwa sababu alikwishamjua tayari.
Yesu na Nikodemu
3 Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. 2 Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.”
3 Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya.[m] Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
4 Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je, anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?”
5 Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6 Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. 7 Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ 8 Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.”
9 Nikodemu akauliza, “Je, haya yote yanawezekana namna gani?”
10 Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? 11 Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. 12 Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! 13 Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.”
14 Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani?[n] Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. 15 Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele.[o]
16 Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. 17 Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe. 18 Wote wanaomwamini Mwana wa Mungu hawahukumiwi hatia yoyote. Lakini wale wasiomwamini wamekwisha kuhukumiwa tayari, kwa sababu hawakumwamini Mwana pekee wa Mungu. 19 Wamehukumiwa kutokana na ukweli huu: Kwamba nuru[p] imekuja ulimwenguni, lakini watu hawakuitaka nuru. Bali walilitaka giza, kwa sababu walikuwa wanatenda mambo maovu. 20 Kila anayetenda maovu huichukia nuru. Hawezi kuja kwenye nuru, kwa sababu nuru itayaweka wazi matendo maovu yote aliyotenda.
21 Lakini yeyote anayeifuata njia ya kweli huja kwenye nuru. Nayo nuru itaonesha kuwa Mungu amekuwepo katika matendo yake yote.
Yesu na Yohana Mbatizaji
22 Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. 23 Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. 24 Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani.
25 Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.[q] 26 Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.
27 Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28 Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29 Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30 Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”
Ajaye Kutoka Mbinguni
31 “Anayekuja kutoka juu ni mkubwa kuliko wengine wote. Anayetoka duniani ni wa dunia. Naye huzungumza mambo yaliyo ya duniani. Lakini yeye anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wengine wote. 32 Huyo huyasema aliyoyaona na kuyasikia, lakini watu hawayapokei anayoyasema. 33 Bali yeyote anayepokea anayoyasema basi amethibitisha kwamba Mungu husema kweli. 34 Na kwamba Mungu alimtuma, na yeye huwaeleza watu yale yote Mungu aliyoyasema. Huyo Mungu humpa Roho kwa ujazo kamili. 35 Baba anampenda Mwana na amempa uwezo juu ya kila kitu. 36 Yeyote anayemwamini Mwana anao uzima wa milele. Lakini wale wasiomtii Mwana hawataupata huo uzima. Na hawataweza kuiepuka hasira ya Mungu.”
Yesu Azungumza na Mwanamke Msamaria
4 Yesu akatambua ya kwamba Mafarisayo wamesikia habari kuwa alikuwa anapata wafuasi wengi kuliko Yohana na kuwabatiza. 2 (Lakini kwa hakika, Yesu mwenyewe hakumbatiza mtu yeyote huko; bali wafuasi wake ndiyo waliowabatiza watu kwa niaba yake.) 3 Hivyo akaondoka Uyahudi na kurudi Galilaya.
4 Barabara ya kuelekea Galilaya ilimpitisha Yesu katikati ya nchi ya Samaria. 5 Akiwa Samaria Yesu akafika katika mji wa Sikari, ulio karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. 6 Mahali hapo ndipo kilikuwapo kisima cha Yakobo. Kutokana na safari yake kuwa ndefu Yesu alichoka, hivyo akakaa chini kando ya kisima. Nayo ilikuwa saa sita adhuhuri. 7 Baadaye mwanamke Msamaria akaja kisimani hapo kuchota maji, na Yesu akamwambia, “Tafadhali nipe maji ninywe.” 8 Hili lilitokea wakati wafuasi wake walipokuwa mjini kununua chakula.
9 Mwanamke yule akajibu, “Nimeshangazwa wewe kuniomba maji unywe! Wewe ni Myahudi nami ni mwanamke Msamaria!” (Wayahudi hawana uhusiano na Wasamaria.[r])
10 Yesu akajibu, “Hujui kile Mungu anachoweza kukukirimu. Na hunijui mimi ni nani, niliyekuomba maji ninywe. Kama ungejua, nawe ungekuwa umeniomba tayari, nami ningekupa maji yaletayo uzima.”
11 Mwanamke akasema, “Bwana, utayapata wapi maji yaliyo hai? Kisima hiki kina chake ni kirefu sana, nawe huna kitu cha kuchotea. 12 Je, wewe ni mkuu kumzidi baba yetu Yakobo? Yeye ndiye aliyetupa kisima hiki. Yeye alikunywa kutoka kisima hiki, na wanawe, na wanyama wake wote.”
13 Yesu akajibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14 Bali yeyote anayekunywa maji ninayompa mimi hatapata kiu tena. Maji ninayowapa watu yatakuwa kama chemichemi inayobubujika ndani yao. Hayo yatawaletea uzima wa milele.”
15 Mwanamke akamwambia Yesu, “Bwana, nipe maji hayo. Kisha sitapata kiu na sitapaswa kuja tena hapa kuchota maji.”
16 Yesu akamwambia, “Nenda kamwite mumeo kisha urudi naye hapa.”
17 Mwanamke akajibu, “Lakini mimi sina mume.”
Yesu akamwambia, “Uko sahihi kusema kuwa huna mume. 18 Hiyo ni kwa sababu, hata kama umekuwa na waume watano, mwanaume unayeishi naye sasa sio mume wako. Huo ndiyo ukweli wenyewe.”
19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona ya kuwa wewe ni nabii. 20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu. Lakini ninyi Wayahudi mnasema kuwa Yerusalemu ndipo mahali ambapo watu wanapaswa kuabudia.”
21 Yesu akasema, “Mwanamke! Niamini mimi, wakati unakuja ambapo hamtakwenda Yerusalemu wala kuja kwenye mlima huu kumwabudu Baba. 22 Ninyi Wasamaria hamwelewi mambo mengi kuhusu yule mnayemwabudu. Sisi Wayahudi tunamfahamu vizuri tunayemwabudu, kwa maana njia yake ya kuuokoa ulimwengu imepatikana kupitia Wayahudi. 23 Lakini wakati unakuja wenye nia halisi ya kuabudu watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa hakika, wakati huo sasa umekwishafika. Na hao ndiyo watu ambao Baba anataka wamwabudu. 24 Mungu ni roho. Hivyo wote wanaomwabudu wanapaswa kumwabudu katika roho na kweli.”
25 Mwanamke akasema, “Naelewa kwamba Masihi anakuja.” (Ndiye anayeitwa Kristo.)
“Atakapokuja, atatufafanulia kila kitu.”
26 Kisha Yesu akasema, “Mimi ninayezungumza nawe sasa, ndiye Masihi.”
27 Wakati huo huo wafuasi wa Yesu wakarudi toka mjini. Nao walishangaa kwa sababu walimwona Yesu akiongea na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza yule mwanamke, “Unataka nini?” Wala Yesu, “Kwa nini unaongea naye?”
28 Yule mwanamke akauacha mtungi wake wa maji na kurudi mjini. Akawaambia watu kule, 29 “Mwanaume mmoja amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya. Njooni mkamwone. Inawezekana yeye ndiye Masihi.” 30 Hivyo wale watu wakatoka mjini wakaenda kumwona Yesu!
31 Wakati huyo mwanamke akiwa mjini, wafuasi wa Yesu wakamsihi Bwana wao wakamwambia, “Mwalimu, ule chakula chochote.”
32 Lakini Yesu akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkijui.”
33 Hapo wafuasi wake wakaulizana, “Kwani kuna mtu yeyote hapa aliyemletea chakula mapema?”
34 Yesu akasema, “Chakula changu ni kuimaliza kazi ile ambayo aliyenituma amenipa niifanye. 35 Mnapopanda mimea, huwa mnasema, ‘Bado miezi minne ya kusubiri kabla ya kuvuna mazao.’ Lakini mimi ninawaambia, yafumbueni macho yenu na kuyaangalia mashamba. Sasa yako tayari kuvunwa. 36 Hata sasa, watu wanaovuna mazao wanalipwa. Wanawaleta ndani wale watakaoupata uzima wa milele. Ili kwamba watu wanaopanda waweze kufurahi wakati huu pamoja na wale wanaovuna. 37 Ni kweli tunaposema, ‘Mtu mmoja hupanda, lakini mwingine huvuna mazao.’ 38 Mimi niliwatuma kukusanya mazao ambayo ninyi hamkuyahangaikia. Wengine waliyahangaikia, nanyi mnapata faida kutokana na juhudi na kazi yao.”
39 Wasamaria wengi katika mji huo wakamwamini Yesu. Wakaamini kutokana na yale ambayo walisikia yule mwanamke akiwaambia juu ya Yesu. Aliwaambia, “Yeye amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya.” 40 Wasamaria wakaenda kwa Yesu. Wakamsihi akae pamoja nao. Naye akakaa nao kwa siku mbili. 41 Watu wengi zaidi wakamwamini Yesu kutokana na mambo aliyoyasema.
42 Watu hao wakamwambia mwanamke, “Mwanzoni tulimwamini Yesu kutokana na jinsi ulivyotueleza. Lakini sasa tunaamini kwa sababu tumemsikia sisi wenyewe. Sasa tunajua kwamba hakika Yeye ndiye atakayeuokoa ulimwengu.”
Yesu Amponya Mwana wa Afisa
(Mt 8:5-13; Lk 7:1-10)
43 Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. 44 (Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) 45 Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko.
46 Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47 Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”
49 Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”
50 Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”
Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51 Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”
52 Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”
Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”
53 Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.
54 Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.
Yesu Amponya Mtu Bwawani
5 Baadaye, Yesu akaenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu maalumu ya Wayahudi. 2 Huko Yerusalemu kulikuwa na bwawa lenye mabaraza matano. Kwa Kiaramu liliitwa Bethzatha.[s] Bwawa hili lilikuwa karibu na Lango la Kondoo. 3 Wagonjwa wengi walikuwa wamelala katika mabaraza pembeni mwa bwawa. Baadhi yao walikuwa wasiyeona, wengine walemavu wa viungo, na wengine waliopooza mwili.[t] 4 Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao.[u] 5 Mmoja wa watu waliolala hapo alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. 6 Yesu alimwona akiwa amelala hapo na kutambua kuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu sana. Hivyo akamwuliza, “Je, unataka kuwa mzima?”
7 Yule mgonjwa akajibu, “Bwana, hakuna mtu wa kunisaidia kuingia kwenye bwawa mara maji yanapotibuliwa. Najitahidi kuwa wa kwanza kuingia majini. Lakini ninapojaribu, mtu mwingine huniwahi na kuingia majini kabla yangu.”
8 Kisha Yesu akasema, “Simama juu! Beba kirago chako na utembee.” 9 Mara hiyo, mtu huyo akapona. Akabeba kirago chake na kuanza kutembea.
Siku yalipotokea haya yote ilikuwa ni Siku ya Sabato.[v] 10 Hivyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato. Kulingana na sheria yetu wewe hauruhusiwi kubeba mkeka katika siku ya Sabato!”
11 Lakini yeye akajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Beba mkeka wako uende.’”
12 Wakamwuliza, “Ni nani aliyekuambia kubeba mkeka wako na kutembea?”
13 Lakini yule mtu aliyeponywa hakuwa amemfahamu ni nani. Walikuwepo watu wengi hapo, na Yesu alikwisha kuondoka.
14 Baadaye, Yesu akamwona huyo mtu Hekaluni na akamwambia, “Tazama, umepona sasa. Kwa hivyo uache kutenda dhambi tena, la sivyo jambo baya zaidi laweza kukupata.” 15 Kisha huyo mtu akaondoka na kurudi kwa wale Wayahudi waliomuuliza. Naye aliwaeleza kuwa Yesu ndiye aliyemponya.
16 Yesu alikuwa anayafanya yote haya katika siku ya Sabato. Hivyo Wayahudi hao wakaanza kumsumbua asiendelee. 17 Lakini yeye akawaambia, “Baba yangu hajawahi kuacha kufanya kazi, hivyo nami pia nafanya kazi.” 18 Hili likawafanya waongeze juhudi ya kumwua. Wakasema, “Mwanzoni mtu huyu alikuwa anavunja sheria kuhusu siku ya Sabato. Kisha akasema kwamba Mungu ni Baba yake! Yeye anajifanya kuwa yuko sawa na Mungu.”
Yesu Anayo Mamlaka ya Mungu
19 Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. 20 Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. 21 Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.”
22 “Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. 23 Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana.
24 Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima. 25 Mniamini, wakati muhimu sana unakuja. Wakati huo tayari upo ambapo watu waliokufa wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu. Na hao watakaoisikia watafufuka na kuwa hai. 26 Uzima huja kutoka kwa Baba mwenyewe. Na pia Baba amemruhusu Mwana kutoa uzima. 27 Na Baba amempa Mwana mamlaka ya kuwahukumu watu wote kwa sababu yeye ndiye Mwana wa Adamu.
28 Ninyi msishangazwe na hili. Wakati unakuja ambapo watu wote waliokufa na kuwamo makaburini mwao wataisikia sauti yake. 29 Kisha watatoka nje ya makaburi yao. Wale waliotenda mema watafufuka na kupata uzima wa milele. Lakini wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa kwa kuwa na hatia.
30 Siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninahukumu kama vile ninavyoagizwa. Na hukumu yangu ni halali, kwa sababu sitafuti kujifurahisha mwenyewe. Bali ninataka tu kumfurahisha yeye aliyenituma.”
Yesu Asema Zaidi Na Viongozi wa Kiyahudi
31 “Endapo nitawaeleza watu mambo yangu mwenyewe, watu hawatakuwa na uhakika kama yale ninayosema ni kweli. 32 Lakini yupo mwingine anayewaeleza watu mambo yangu, nami nafahamu kuwa yale anayoyasema juu yangu ni kweli.
33 Mliwatuma watu kwa Yohana, naye akawaambia yaliyo kweli. 34 Hivyo sihitaji mtu yeyote wa kuwaeleza watu juu yangu, isipokuwa nawakumbusha ninyi yale aliyoyasema Yohana ili muweze kuokolewa. 35 Yohana alikuwa kama taa iliyowaka na kutoa mwanga, nanyi mlipata raha mkiufurahia mwanga wake japo kwa muda.
36 Hata hivyo uthibitisho nilionao mwenyewe juu yangu ni mkuu kuliko chochote alichokisema Yohana. Mambo ninayofanya ndiyo yanayonithibitisha. Haya ndiyo Baba aliyonipa kufanya. Nayo yanadhihirisha kuwa Baba alinituma. 37 Na Baba aliyenituma yeye mwenyewe ametoa uthibitisho juu yangu. Lakini hamjawahi kabisa kuisikia sauti yake. Hamjawahi pia kuuona uso wake jinsi ulivyo. 38 Mafundisho ya Baba hayakai ndani yenu, kwa sababu hamumwamini yule aliyetumwa na Baba. 39 Mnajifunza Maandiko kwa makini. Nanyi mnafikiri kuwa yanawapa uzima wa milele. Maandiko haya haya yanaeleza habari zangu! 40 Lakini mnakataa kuja kwangu kuupata huo uzima.
41 Sitaki kutukuzwa nanyi ama na mwanadamu mwingine yeyote. 42 Hata hivyo ninawajua ninyi, na ninajua kwamba hamna upendo kwa Mungu. 43 Nimekuja kutoka kwa Baba yangu nami ni msemaji wake, lakini hamnikubali. Lakini watu wengine wakija wakijisemea mambo yao tu, mnawakubali! 44 Ninyi mnapenda kupeana sifa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini hamjaribu kupata sifa zinazotoka kwa Mungu wa pekee. Hivyo mtawezaje kuamini? 45 Msifikiri kwamba mimi ndiye nitakayesimama mbele za Baba na kuwashtaki. Musa ndiye atakayewashtaki. Na ndiye mliyetegemea angeliwaokoa. 46 Kama kwa hakika mlimwamini Musa, nami mlipaswa kuniamini, kwa sababu yeye aliandika habari juu yangu. 47 Lakini hamuyaamini aliyoyaandika, hivyo hamuwezi kuyaamini ninayoyasema.”
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17)
6 Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). 2 Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. 3 Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. 4 Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5 Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” 6 Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya.
7 Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.”
8 Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, 9 “Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.”
10 Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. 11 Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji.
12 Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” 13 Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano.
14 Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii[w] anayekuja ulimwenguni!”
15 Yesu akajua kwamba watu walipanga kuja kumchukua na kumfanya kuwa mfalme wao baada ya kuona muujiza alioufanya. Hivyo akaondoka na kwenda milimani peke yake.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-27; Mk 6:45-52)
16 Jioni ile wafuasi wake wakashuka kwenda ziwani. 17 Ilikuwa giza sasa, wakati huo Yesu hakuwa pamoja na wafuasi wake. Wakapanda kwenye mashua na kuanza safari kuvuka ziwa kwenda Kapernaumu. 18 Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana. Mawimbi ziwani yakawa makubwa. 19 Wakaiendesha mashua kiasi cha kilomita tano au sita. Kisha wakamwona Yesu. Yeye alikuwa anatembea juu ya maji, akiifuata mashua. Nao wakaogopa. 20 Lakini Yesu akawaambia, “Msiogope. Ni mimi.” 21 Baada ya kusema hivyo, wakamkaribisha kwenye mashua. Kisha mashua ikafika ufukweni katika sehemu waliyotaka kwenda.
Watu Wamtafuta Yesu
22 Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. 23 Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. 24 Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu.
Yesu, Mkate wa Uzima
25 Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?”
26 Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. 27 Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”
28 Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”
29 Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(C)
32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34 Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”
35 Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36 Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,[x] lakini bado hamuniamini. 37 Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38 Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39 Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40 Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”
41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45 Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’(D) Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46 Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.
47 Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. 48 Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49 Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50 Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51 Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”
52 Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?”
53 Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. 54 Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. 55 Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. 56 Wale waulao[y] mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao.
57 Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.”
59 Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu.
Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu
60 Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”
61 Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? 62 Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63 Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64 Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65 Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”
66 Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.
67 Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69 Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”
70 Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71 Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.
Yesu na Ndugu Zake
7 Baada ya hayo, Yesu alitembea kuizunguka miji ya Galilaya. Hakutaka kutembelea Uyahudi, kwa sababu viongozi wa Kiyahudi kule walitaka kumuua. 2 Huu ulikuwa ni wakati wa sherehe za sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. 3 Hivyo ndugu zake wakamwambia, “Unapaswa kuondoka hapa na kwenda kwenye sikukuu Uyahudi. Kisha wafuasi wako kule wataweza kuona ishara unazofanya. 4 Ikiwa unataka kujulikana, basi usiyafiche mambo unayoyafanya. Ikiwa unaweza kufanya mambo ya ajabu hivi, acha ulimwengu wote uone.” 5 Ndugu zake Yesu walisema hivi kwa kuwa hata wao hawakumwamini.
6 Yesu akawaambia, “Wakati unaonifaa kufanya hivyo haujafika, lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa. 7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi. Bali ulimwengu unanichukia mimi kwa sababu nawaambia watu ulimwenguni ya kwamba wanafanya maovu. 8 Hivyo ninyi nendeni kwenye sikukuu. Mimi sitaenda sasa, kwa sababu wakati unaonifaa haujafika.” 9 Baada ya Yesu kusema hayo, akabaki Galilaya.
10 Ndugu zake nao wakaondoka kwenda kwenye sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. Baada ya kuondoka kwao Yesu naye akaenda huko, ingawa hakutaka watu wamwone. 11 Baada ya sikukuu ile kupita viongozi wa Kiyahudi wakawa wanamtafuta Yesu. Wakasema, “Yuko wapi huyo Yesu?”
12 Lilikuwepo kundi la watu wengi mahali pale. Wengi kati yao walikuwa wakizungumza kwa siri kuhusu Yesu. Wengine wakasema, “Huyu ni mtu mzuri.” Lakini wengine wakakataa na kusema, “Hapana, mtu huyo huwadanganya watu.” 13 Pamoja na hayo hakuwepo mtu aliyekuwa na busara zaidi kati yao kusema na Yesu kwa uwazi. Kwani waliwaogopa viongozi wa Wayahudi.
Yesu Afundisha Yerusalemu
14 Sherehe ile ilipokaribia kuisha, Yesu akaenda katika maeneo ya Hekalu na kuanza kufundisha. 15 Viongozi wa Kiyahudi waliomsikiliza walishangazwa na kusema, “Mtu huyu amejifunza wapi mambo haya yote? Yeye hakuwahi kupata mafundisho kama yale tuliyonayo.”
16 Yesu akajibu, “Ninayofundisha siyo yangu. Mafundisho yangu yanatoka kwake Yeye aliyenituma. 17 Watu wanaotaka kufanya kwa uhakika kama anavyotaka Mungu watafahamu kuwa mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu. Watafahamu kwamba mafundisho haya siyo yangu. 18 Kama ningeyafundisha mawazo yangu, ningekuwa najitafutia heshima yangu mwenyewe. Lakini kama najaribu kumletea heshima Yeye aliyenituma, basi naweza kuaminiwa. Yeyote anayefanya kama hivyo hawezi kusema uongo. 19 Musa aliwapa sheria, sivyo? Lakini hamuitii hiyo sheria. Kama mnaitii, kwa nini basi mnataka kuniua?”
20 Watu wakamjibu Yesu, “Pepo amekuchanganya akili! Sisi hatuna mipango ya kukuua!”
21 Yesu akawambia, “Nilitenda ishara moja siku ya Sabato, na wote mkashangaa. 22 Lakini mnatii sheria aliyowapa Musa kuhusu kutahiriwa; nanyi mnatahiri hata siku ya Sabato! (Lakini hakika, Musa siye aliyewatahiri. Tohara Ilitoka kwa baba zenu walioishi kabla ya Musa.) Ndiyo, siku zote mnatahiri wana wenu hata siku ya Sabato. 23 Hii inaonesha kuwa mtu anaweza kutahiriwa siku ya Sabato ili kuitimiza sheria ya Musa. Sasa kwa nini mnanikasirikia mimi kwa kuuponya mwili wote wa mtu siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo ya watu kwa jinsi mnavyoyaona. Muwe makini kutoa kuhukumu kwa njia ya haki kabisa.”
Watu Wajiuliza Ikiwa Yesu Ni Masihi
25 Kisha baadhi ya watu waliokuwepo Yerusalemu wakasema, “Huyo ndiye mtu wanayetaka kumuua. 26 Lakini anafundisha mahali ambapo kila mtu anaweza kumwona na kumsikia. Wala hakuna anayejaribu kumzuia kufundisha. Inawezekana viongozi wamekubali kuwa kweli yeye ni Masihi. 27 Lakini Masihi halisi atakapokuja, hakuna atakayejua anakotoka. Nasi tunajua nyumbani kwake mtu huyu ni wapi.”
28 Yesu alikuwa bado anafundisha katika eneo la Hekalu aliposema kwa sauti, “Ni kweli mnanijua mimi na kule ninakotoka? Niko hapa, lakini siyo kwa matakwa yangu. Nilitumwa na Yeye aliye wa kweli. Lakini ninyi hamumjui. 29 Mimi namfahamu kwa sababu ninatoka kwake. Naye Ndiye aliyenituma.”
30 Yesu aliposema hivi, watu wakajaribu kumkamata. Lakini hakuna aliyethubutu hata kumgusa, kwa sababu wakati unaofaa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika. 31 Hata hivyo watu wengi wakamwamini Yesu. Wakasema, “Je, tunafikiri kuna haja ya kuendelea kumngojea Masihi mwingine aje atakayetenda ishara nyingine zaidi ya zile alizotenda mtu huyu?”
Viongozi wa Kiyahudi Wajaribu Kumkamata Yesu
32 Mafarisayo wakasikia yale ambayo watu walikuwa wakiyasema juu ya Yesu. Kwa sababu hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakawatuma walinzi wa Hekalu kwenda kumkamata. 33 Kisha Yesu akasema, “Nitakuwa nanyi kwa muda mfupi. Kisha nitarudi kwake Yeye aliyenituma. 34 Ninyi mtanitafuta, lakini hamtaniona. Nanyi hamwezi kuja kule nitakapokuwa.”
35 Hawa Wayahudi wakaambiana wao kwa wao, “Huyu mtu atakwenda wapi sisi tusikoweza kufika? Je, anaweza kwenda kwenye miji ya Wayunani wanamoishi watu wetu? Je, atawafundisha Wayunani katika miji hiyo? 36 Anasema, ‘Mtanitafuta, lakini hamtaniona.’ Vile vile anasema, ‘Hamwezi kuja kule nitakapokwenda.’ Maana yake ni nini?”
Yesu Azungumza Juu ya Roho Mtakatifu
37 Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. 38 Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” 39 Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho.
Watu Wanabishana Juu ya Yesu
40 Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.”[z]
41 Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.”
Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. 42 Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” 43 Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. 44 Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo.
Baadhi ya Viongozi wa Kiyahudi Wakataa Kuamini
45 Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?”
46 Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!”
47 Mafarisayo wakajibu, “Kwa hiyo Yesu amewadanganya hata ninyi? 48 Hamuoni kuwa hakuna kiongozi yeyote wala sisi Mafarisayo anayemwamini? 49 Lakini watu hao walio nje wasiojua sheria wamo katika laana ya Mungu.”
50 Lakini Nikodemu alikuwa katika kundi lile. Naye ndiye yule aliyekwenda kumwona Yesu pale mwanzo.[aa] Naye akasema, 51 “Sheria yetu haitaturuhusu kumhukumu mtu na kumtia hatiani kabla ya kumsikiliza kwanza na kuyaona aliyotenda?”
52 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Wewe nawe utakuwa umetoka Galilaya. Jifunze Maandiko. Hutapata lolote kuhusu nabii[ab] anayetoka Galilaya.”
Mwanamke Afumaniwa Akizini
53 Kisha wote wakaondoka na kwenda nyumbani.
8 Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. 2 Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha.
3 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. 4 Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. 5 Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je, Unasema tufanye nini?”
6 Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. 7 Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” 8 Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo.
9 Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10 Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” 11 Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.”[ac]
Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.”
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”
13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”
14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”
19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”
Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”
20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika.
Baadhi ya Wayahudi Hawamwelewi Yesu
21 Kwa mara nyingine, Yesu akawaambia watu, “Mimi nitawaacha. Nanyi mtanitafuta, lakini pamoja na hayo mtakufa katika dhambi zenu. Kwani hamuwezi kuja kule niendako.”
22 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakaulizana wenyewe, “Je, atajiua mwenyewe? Je, ndiyo maana alisema, ‘Hamuwezi kuja kule niendako’?”
23 Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi watu ni wa hapa chini, lakini mimi ni wa kule juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, lakini mimi si wa ulimwengu huu. 24 Niliwaambia kwamba mnaweza kufa katika dhambi zenu. Ndiyo, kama hamtaamini kuwa MIMI NDIYE,[ad] mtakufa katika dhambi zenu.”
25 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani?”
Yesu akajibu, “Mimi ni yule niliyekwisha kuwaambia tangu mwanzo kuwa ni nani. 26 Ninayo mengi zaidi ya kusema na ya kuwahukumu. Lakini nawaambia watu yale tu niliyosikia kutoka kwake aliyenituma, naye daima husema kweli.”
27 Wale watu hawakuelewa alikuwa anazungumza habari za nani. Kwani Yeye alikuwa anawaambia habari za Baba. 28 Naye akawaambia, “Mtamwinua juu[ae] Mwana wa Adamu. Ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE. Mtajua kuwa lo lote nilifanyalo silifanyi kwa mamlaka yangu. Mtajua kuwa nayasema tu yale Baba yangu aliyonifundisha. 29 Yeye aliyenituma yuko pamoja nami. Siku zote nafanya yale yanayompendeza. Naye hajawahi kuniacha peke yangu.” 30 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, watu wengi wakamwamini.
Yesu Azungumzia Uhuru kutokana na Dhambi
31 Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. 32 Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.”
33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”
34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37 Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38 Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”
39 Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.”
Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. 40 Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41 Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”
Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”
42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43 Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44 Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.
45 Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46 Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
Yesu Azungumza Juu yake na Ibrahimu
48 Wayahudi wakajibu, “Sisi tunasema kuwa wewe ni Msamaria na pepo anakufanya uwe mwendawazimu! Je, hatuko sahihi kusema hivyo?”
49 Yesu akajibu, “Sina pepo ndani yangu. Nampa heshima Baba yangu, lakini ninyi hamnipi heshima. 50 Sijaribu kujitukuza mimi mwenyewe. Yupo mmoja anayetaka kunitukuza. Ndiye hakimu. 51 Nawaahidi, yeyote anayeendelea kutii mafundisho yangu, hatakufa milele.”
52 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Sasa tunatambua kuwa una pepo ndani yako! Hata Ibrahimu na manabii walikufa. Lakini unasema, ‘Yeyote anayetii mafundisho yangu, hatakufa kamwe.’ 53 Wewe si mkuu zaidi ya baba yetu Ibrahimu! Yeye alikufa na manabii nao walikufa. Unadhani wewe ni nani?”
54 Yesu akajibu, “Kama ningejipa heshima mwenyewe, heshima hiyo isingelifaa kwa namna yoyote ile. Yule anayenipa mimi heshima ni Baba yangu. Ninyi mnasema kuwa ndiye Mungu wenu. 55 Lakini kwa hakika hamumjui yeye. Mimi namjua. Kama ningesema simjui, basi ningekuwa mwongo kama ninyi. Lakini namjua, na kuyatii anayosema. 56 Baba yenu Ibrahimu alifurahi sana kwamba angeiona siku nilipokuja duniani. Hakika aliiona na akafurahi sana.”
57 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Ati nini? Wawezaje kusema ulimwona Ibrahimu? Wewe bado hujafikisha hata umri wa miaka hamsini!”
58 Yesu akajibu, “Ukweli ni kwamba, kabla Ibrahimu hajazaliwa MIMI NIPO.” 59 Aliposema haya, wakachukua mawe ili wamponde. Lakini Yesu akajificha, na kisha akaondoka katika eneo la Hekalu.
Yesu Amponya Aliyezaliwa Pasipo Kuwa na Uwezo wa Kuona
9 Yesu alipokuwa anatembea, alimwona mtu asiyeona tangu alipozaliwa. 2 Wafuasi wake wakamwuliza, “Mwalimu, kwa nini mtu huyu alizaliwa asiyeona? Dhambi ya nani ilifanya hili litokee? Ilikuwa ni dhambi yake mwenyewe au ya wazazi wake?” 3 Yesu akajibu, “Si dhambi yoyote ya huyo mtu wala ya wazazi wake iliyosababisha awe asiyeona. Alizaliwa asiyeona ili aweze kutumiwa kuonesha mambo makuu ambayo Mungu anaweza kufanya. 4 Kukiwa bado ni mchana, tunapaswa kuendelea kuzifanya kazi zake Yeye aliyenituma. Usiku unakuja, na hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi wakati wa usiku. 5 Nikiwa bado nipo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.”
6 Yesu aliposema haya, akatema mate chini kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka yule asiyeona katika macho yake. 7 Yesu akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni “Aliyetumwa”.) Hivyo mtu yule akaenda katika bwawa lile, akanawa na kurudi akiwa mwenye kuona.
8 Majirani zake na wengine waliomwona akiomba omba wakasema, “Angalieni! Hivi huyu ndiye mtu yule aliyekaa siku zote na kuomba omba?”
9 Wengine wakasema, “Ndiyo! Yeye ndiye.” Lakini wengine wakasema, “Hapana, hawezi kuwa yeye. Huyo anafanana naye tu.”
Kisha yule mtu akasema, “Mimi ndiye mtu huyo.”
10 Wakamwuliza, “Kulitokea nini? Uliwezaje kupata kuona?”
11 Akawajibu, “Mtu yule wanayemwita Yesu alitengeneza tope akayapaka macho yangu. Kisha akaniambia ‘Nenda kanawe kwenye bwawa la Siloamu.’ Hivyo nikaenda kule na kunawa, na ndipo nikaweza kuona.”
12 Wakamwuliza, “Yuko wapi mtu huyo?”
Akajibu, “Mimi sijui aliko.”
Baadhi ya Mafarisayo Wana Maswali
13 Kisha watu wakampeleka huyo mtu kwa Mafarisayo. 14 Siku Yesu alipotengeneza yale matope na kuyaponya macho ya mtu huyo ilikuwa ni Sabato. 15 Hivyo Mafarisayo wakamwuliza huyo mtu, “Uliwezaje kuona?”
Akawajibu, “Alipaka matope katika macho yangu. Nikaenda kunawa, na sasa naweza kuona.”
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyo mtu hatii sheria inayohusu siku ya Sabato. Kwa hiyo hatoki kwa Mungu.”
Wengine wakasema, “Lakini mtu aliye mtenda dhambi hawezi kufanya ishara kama hizi?” Hivyo hawakuelewana wao kwa wao. 17 Wakamuuliza tena huyo mtu, “Kwa vile aliponya macho yako, unasemaje juu ya mtu huyo?”
Akajibu, “Yeye ni nabii.” 18 Viongozi wa Kiyahudi walikuwa bado hawaamini kwamba haya yalimtokea mtu huyo; kwamba alikuwa haoni na sasa ameponywa. Lakini baadaye wakawaita wazazi wake. 19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mwana wenu? Mnasema alizaliwa akiwa haoni. Sasa amewezaje kuona?”
20 Wazazi wake wakajibu, “Tunafahamu kwamba mtu huyu ni mwana wetu. Na tunajua kuwa alizaliwa akiwa asiyeona. 21 Lakini hatujui kwa nini sasa anaweza kuona. Hatumjui aliyeyaponya macho yake. Muulizeni mwenyewe. Yeye ni mtu mzima anaweza kujibu mwenyewe.” 22 Walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Kiyahudi. Viongozi walikwisha azimia kwamba, wangemwadhibu mtu yeyote ambaye angesema Yesu alikuwa Masihi. Wangewazuia hao wasije tena kwenye sinagogi. 23 Ndiyo maana wazazi wake walisema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni yeye!”
24 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakamwita yule aliyekuwa haoni. Wakamwambia aingie ndani tena. Wakasema, “Unapaswa kumheshimu Mungu na kutuambia ukweli. Tunamjua mtu huyu kuwa ni mtenda dhambi.”
25 Yule mtu akajibu, “Mimi sielewi kama yeye ni mtenda dhambi. Lakini nafahamu hili: Nilikuwa sioni, na sasa naweza kuona!”
26 Wakawuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyaponyaje macho yako?”
27 Akajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia hayo. Lakini hamkutaka kunisikiliza. Kwa nini mnataka kusikia tena? Mnataka kuwa wafuasi wake pia?”
28 Kwa hili wakampigia makelele na kumtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake, siyo sisi! Sisi ni wafuasi wa Musa. 29 Tunafahamu kwamba Mungu alisema na Musa. Lakini wala hatujui huyu mtu anatoka wapi!”
30 Yule mtu akajibu, “Hili linashangaza kweli! Hamjui anakotoka, lakini aliyaponya macho yangu. 31 Wote tunajua kuwa Mungu hawasikilizi watenda dhambi, bali atamsikiliza yeyote anayemwabudu na kumtii. 32 Hii ni mara ya kwanza kuwahi kusikia kwamba mtu ameponya macho ya mtu aliyezaliwa asiyeona. 33 Hivyo lazima anatoka kwa Mungu. Kama asingetoka kwa Mungu, asingefanya jambo lolote kama hili.”
34 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ulizaliwa ukiwa umejaa dhambi. Unataka kutufundisha sisi?” Kisha wakamwambia atoke ndani ya sinagogi na kukaa nje.
Kutoona Kiroho
35 Yesu aliposikia kuwa walimlazimisha huyo mtu kuondoka, alikutana naye na kumuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”
36 Yule mtu akajibu, “Niambie ni nani huyo, bwana, ili nimwamini.” 37 Yesu akamwambia, “Umekwisha kumwona tayari. Mwana wa Adamu ndiye anayesema nawe sasa.”
38 Yule mtu akajibu, “Ndiyo, ninaamini, Bwana!” Kisha akainama na kumwabudu Yesu.
39 Yesu akasema, “Nilikuja ulimwenguni ili ulimwengu uweze kuhukumiwa. Nilikuja ili wale wasiyeona waweze kuona. Kisha nilikuja ili wale wanaofikiri wanaona waweze kuwa wasiyeona.”
40 Baadhi ya Mafarisayo walikuwa karibu na Yesu. Wakamsikia akisema haya. Wakamwuliza, “Nini? Unasema sisi pia ni wale wasiyeona?”
41 Yesu akasema, “Kama mngekuwa wasiyeona hakika, msingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini kwa kuwa mnasema mnaona, basi bado mngali na hatia.”
Mchungaji na Kondoo Wake
10 Yesu akawaambia, “Hakika ninawaambia, mtu anapoingia katika zizi la kondoo, hutumia mlango. Kama akiingia kwa kutumia njia nyingine yoyote, huyo ni mwizi. Anajaribu kuwaiba kondoo. 2 Lakini mtu anayewachunga kondoo hupitia mlangoni. Yeye ndiye mchungaji. 3 Mtu anayelinda mlangoni humfungulia mlango mchungaji. Na kondoo huisikiliza sauti ya mchungaji wao. Naye huwaita kondoo wake mwenyewe kwa majina yao, na huwaongoza kwenda nje. 4 Mchungaji huwatoa nje kondoo wake wote. Kisha huwatangulia mbele na kuwaongoza. Kondoo nao humfuata, kwa sababu wanaifahamu sauti yake. 5 Lakini kamwe kondoo hawatamfuata wasiyemfahamu. Bali watamkimbia, kwa sababu hawaifahamu sauti yake.”
6 Yesu aliwaambia watu habari hii, lakini hawakuelewa ilikuwa ina maana gani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[af] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena. 18 Hakuna anayeweza kuuchukua uhai wangu kutoka kwangu. Nautoa uhai wangu kwa hiari yangu. Ninayo haki ya kuutoa, na ninayo haki ya kuuchukua tena. Haya ndiyo aliyoniambia Baba yangu.”
19 Kwa mara nyingine tena Wayahudi wakagawanyika juu ya yale aliyoyasema Yesu. 20 Wengi wao wakasema, “Pepo mchafu amemwingia na kumfanya awe mwendawazimu. Kwa nini sisi tumsikilize?”
21 Lakini wengine wakasema, “Haya siyo maneno ya mtu anayeendeshwa na pepo mchafu. Pepo mchafu hawezi kuponya macho ya mtu asiyeona.”
Viongozi wa Kiyahudi Wasimama Kinyume na Yesu
22 Ulikuwa ni wakati wa baridi, na wakati wa Sikukuu ya Kuweka Wakfu[ag] kule Yerusalemu. 23 Yesu alikuwa katika eneo la Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani. 24 Viongozi wa Kiyahudi wakakusanyika kumzunguka. Wakasema, “Ni mpaka lini utatuacha na mashaka juu yako? Kama wewe ndiwe Masihi, basi tuambie wazi wazi.”
25 Yesu akajibu, “Nilikwisha kuwaambia tayari, lakini hamkuamini. Nafanya miujiza katika jina la Baba yangu. Miujiza hii inaonesha mimi ni nani. 26 Lakini hamuamini, kwa sababu ninyi siyo kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu. Nami nawajua, nao hunifuata. 28 Mimi nawapa kondoo wangu uzima wa milele. Nao hawatakufa kamwe, na tena hakuna atakayemchukua yeyote kutoka mkononi mwangu. 29 Baba yangu ndiye aliyenipa hao, naye ni mkuu kuliko wote.[ah] Hakuna anayeweza kuwaiba kondoo wangu kutoka mkononi mwangu. 30 Mimi na Baba tu umoja.”
31 Kwa mara nyingine Wayahudi pale wakaokota mawe ili wamuue Yesu. 32 Lakini Yeye akawaambia, “Mambo mengi mliyoyaona nikiyatenda yanatoka kwa Baba. Ni kwa mambo gani miongoni mwa hayo mazuri mnataka kuniua?”
33 Wakajibu, “Hatukuui kwa ajili ya jambo lo lote zuri ulilofanya. Lakini wewe unasema mambo yanayomkufuru Mungu! Wewe ni mtu tu, lakini unasema uko sawa na Mungu! Ndiyo sababu tunataka kukuua!”
34 Yesu akajibu, “Imeandikwa katika sheria yenu kuwa Mungu alisema, ‘Nilisema ninyi ni miungu.’(E) 35 Maandiko yaliwaita watu hawa miungu; watu waliopokea ujumbe wa Mungu. Na Maandiko siku zote ni ya kweli. 36 Sasa kwa nini mnanilaumu mimi kwa kumkufuru Mungu kwa kusema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’? 37 Lakini kama sitafanya yale anayoyatenda Baba yangu, basi msiamini ninayosema. 38 Lakini kama nafanya anayofanya Baba, mnapaswa kuyaamini ninayoyafanya. Mnaweza msiniamini mimi, lakini muamini yale ninayotenda. Ndipo mtakapofahamu na kuelewa kwamba Baba yumo ndani yangu nami nimo ndani ya Baba.”
39 Walijaribu kumkamata Yesu tena, lakini yeye akawatoroka.
40 Kisha akarejea tena kwa kuvuka Mto Yordani hadi sehemu ambapo Yohana alipoanzia kazi ya kubatizia watu. Yesu akakaa huko, 41 na watu wengi wakaja kwake. Wakasema, “Yohana hakutenda ishara na miujiza yoyote, lakini kila alichosema kuhusu mtu huyu ni kweli!” 42 Na watu wengi huko wakamwamini Yesu.
Kifo cha Lazaro
11 Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. 2 (Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. 3 Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.”
4 Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” 5 Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. 6 Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, 7 kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.”
8 Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?”
9 Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru[ai] inayomwongoza.”
11 Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.”
12 Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” 13 Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki.
14 Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. 15 Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.”
16 Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.”
Yesu Akiwa Bethania
17 Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. 18 Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu[aj] kutoka Yerusalemu. 19 Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro.
20 Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. 21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. 22 Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.”
23 Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.”
24 Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.”
Footnotes
- 1:1 Neno Kwa Kiyunani neno hili ni logos, lenye maana mawasiliano ya aina yoyote. Linaweza kutafsiriwa “ujumbe”. Hapa lina maana ya Kristo; njia ambayo Mungu alitumia kuueleza ulimwengu kuhusu yeye. Pia katika mstari wa 10,14 na 16.
- 1:5 Nuru Lenye maana ya Kristo, Neno, aliyeleta ulimwenguni uelewa kuhusu Mungu. Pia katika mstari wa 7.
- 1:5 halikuishinda Au “kupotosha ukweli”.
- 1:16 baraka moja baada ya nyingine Kwa maana ya kawaida, “neema juu ya neema”.
- 1:21 Nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19. Pia katika mstari wa 25.
- 1:32-34 Yeye huyo ndiye Mwana wa Mungu Nakala zingine za kale kabisa za Kiyunani zina “Yeye ni mteule wa Mungu.”
- 1:42 Petro Jina la Kiyunani “Petro”, kama jina la Kiaramu “Kefa”, linamaananisha “mwamba”.
- 1:47 unayeweza kumwamini Kwa maana ya kawaida, “Ambaye ndani yake hamna hila.” Katika Agano la Kale, jina lingine la Israeli, Yakobo, linafafanuliwa kwa kutumia maneno kama vile “udanganyifu” au “hila”. Ambayo kwayo alijulikana sana. Tazama Mwa 27:35,36.
- 1:48 mtini Ama “mti wa mtini” aina ya mti wa matunda unaoitwa mtini.
- 1:51 Mwa 28:12, ambayo ni sehemu ya simulizi kuhusu ndoto ya Yakobo ya ngazi iliyokuwa na malaika waliokuwa wakipanda na kushuka kati ya mbinguni na duniani. Tazama Mwa 28:10-17.
- 2:6 desturi yao maalumu ya kunawa Wayahudi walikuwa na sheria za kidini za kunawa maji kwa namna maalumu kabla ya kula, kabla ya kufanya ibada katika Hekalu, na pia nyakati zingine maalumu.
- 2:6 lita 80 au 120 Kwa maana ya kawaida, “metretas 2 au 3”.
- 3:3 azaliwe upya Kuzaliwa tena katika mstari huu na ule wa 7 maneno haya yanaweza kutafsiriwa “kuzaliwa kutoka juu”.
- 3:14 Musa alimwinua … jangwani Wakati watu wa Mungu walikuwa wanakufa kutokana na kuumwa na nyoka, Mungu alimwambia Musa kuweka nyoka wa shaba kwenye mlingoti ili waweze kumwangalia na kuponywa. Tazama Hes 21:4-9.
- 3:15 Wataalamu wengine wanafikiri kwamba maneno ya Yesu kwa Nikodemo yanaendelea hadi mstari wa 21.
- 3:19 nuru Lenye maana ya Kristo, Neno, aliyeleta ulimwenguni uelewa kuhusu Mungu.
- 3:25 ya utakatifu Wayahudi walikuwa na sheria za kidini za kunawa maji kwa namna maalumu kabla ya kula, kabla ya kufanya ibada katika Hekalu, na pia nyakati zingine maalumu.
- 4:9 Wayahudi … Wasamaria Au “Wayahudi hawatumii vitu ambavyo Wasamaria wametumia.”
- 5:2 Bethzatha Pia huitwa Bethsaida au Bethesda. Ama bwawa la maji lililoko kaskazini mwa Hekalu kule.
- 5:3 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza, “na husubiri maji yatibuliwe”.
- 5:4 Nakala zingine za baadaye ziliongeza mstari wa 4, hivyo kutenganisha mstari wa 4 na wa 5: “Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao.”
- 5:9 Siku ya Sabato Ilikuwa siku maalumu kwa Waisraeli na Wayahudi. Kwa amri ya Mungu siku hiyo ilitengwa kama siku ya mapumziko na ya kumheshimu Mungu.
- 6:14 Nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19.
- 6:36 kile ambacho naweza kufanya Au “mimi ninachoweza kufanya”, ambayo ipo katika nakala nyingi za Kiyunani, lakini haipo katika nakala mbili kati ya zile bora zaidi.
- 6:56 waulao Kukaa kula Maana yake, “kutafuna kwa kelele” au “kutafuna kwa nguvu”. Ni neno la kufurahia kula, kunywa na ushirika baada ya mlo mkuu. Sehemu hii ya mlo pia ilijulikana kama “meza ya pili”.
- 7:40 nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19.
- 7:50 Naye ndiye … mwanzo Hadithi juu ya Nikodemo kwenda na kuongea na Yesu katika Yh 3:1-21.
- 7:52 kuhusu nabii Nakala mbili za kale za Kiyunani zina “Nabii”, ambayo ina maana “nabii kama vile Musa” anayetajwa katika Kum 18:15. Katika Mdo 3:22 na 7:37 hii inaeleweka kuwa ni Masihi kama katika mstari wa 40 hapo juu.
- 8:11 Nakala za kale na bora za Kiyunani hazina mistari 7:53-8:11. Nakala zingine zina sehemu hii katika maeneo mbalimbali kitabuni.
- 8:24 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58.
- 8:28 Mtamwinua juu Ina maana kugongomelewa msalabani na “kuinuliwa juu yake ili kufa”. Inaweza kuwa pia kuwa na maana ya pili: “Kuinuliwa juu”.
- 10:16 Yesu ana maana kuwa anao wafuasi ambao si Wayahudi. Tazama Yh 11:52.
- 10:22 Sikukuu ya Kuweka Wakfu Hanukkah, au “Siku Kuu ya Mianga”, ni juma maalumu mwezi wa Disemba lililoadhimisha majira ya mwaka 165 KK wakati Hekalu la Yerusalem lilipotakaswa na kuwa tayari tena kwa ibada ya Wayahudi. Kabla ya hapo lilikuwa chini ya udhibiti wa jeshi la kigeni la Kiyunani na lilitumiwa kwa ibada za kipagani.
- 10:29 Baba yangu … kuliko wote Baadhi ya nakala za zamani za Kiyunani zina, “Kile ambacho Baba amenipa ni kikubwa kuliko vyote.” Kuna tafsiri nyingi katika makala za zamani za Kiyunani. Nakala zingine za baadaye zina “Baba yangu, ambaye amewapa kwangu mimi ni mkuu kuliko wote.”
- 11:10 nuru Hana chanzo cha nuru.
- 11:18 kilomita tatu Kwa maana ya kawaida, “stadia 15” ambazo ni kama umbali wa kilomita tatu hivi.
© 2017 Bible League International