Add parallel Print Page Options

Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya

(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)

17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.

Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[a] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”

Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”

Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.

Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”

10 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje[b] kabla ya Masihi kuja?”

11 Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. 12 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” 13 Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji.

Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu

(Mk 9:14-29; Lk 9:37-43a)

14 Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. 15 Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. 16 Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.”

17 Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” 18 Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona.

19 Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?”

20 Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” 21 [c]

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

(Mk 9:30-32; Lk 9:43b-45)

22 Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, 23 watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana.

Yesu Afundisha Kuhusu Kulipa Kodi

24 Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu[d] wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?”

25 Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.”

Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?”

26 Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.”

Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. 27 Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.”

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)

18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”

Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.

Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.

Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi

(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)

Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.

Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.

Yesu Atumia Simulizi ya Kondoo Aliyepotea

(Lk 15:3-7)

10 Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. 11 [e]

12 Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? 13 Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, 14 Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee.

Mrekebishe Kila Anayekosea

(Lk 17:3)

15 Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako,[f] umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. 16 Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea.[g] 17 Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru.

18 Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu.[h] 19 Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. 20 Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.”

Simulizi Kuhusu Msamaha

21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”

22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[i]

23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[j] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.

26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.

28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’

29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’

30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.

32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.

35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Mk 10:1-12)

19 Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko.

Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?”

Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’(A) Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’(B) Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.”

Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?”[k]

Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.”

10 Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.”

11 Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. 12 Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi.[l] Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.”

Yesu Awakaribisha Watoto

(Mk 10:13-16; Lk 18:15-17)

13 Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. 14 Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” 15 Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko.

Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu

(Mk 10:17-31; Lk 18:18-30)

16 Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?”

17 Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.”

18 Yule mtu akauliza, “Amri zipi?”

Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, 19 mheshimu baba na mama yako,’(C) na ‘mpende jirani yako[m] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(D)

20 Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?”

21 Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!”

22 Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka.

23 Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 24 Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

25 Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?”

26 Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.”

27 Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?”

28 Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. 30 Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo.

Yesu Atumia Mfano wa Wakulima Katika Shamba la Mizabibu

20 Ufalme wa Mungu umefanana na mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Asubuhi mmoja akatoka kwenda kuajiri watu ili walime katika shamba lake la mizabibu. Alikubaliana nao kuwa atawalipa sarafu moja ya fedha ikiwa watafanya kazi siku ile. Kisha akawapeleka kwenye shamba la mizabibu kulima.

Ilipofika saa tatu asubuhi mtu huyo alitoka na kwenda sokoni ambako aliwaona baadhi ya watu wamesimama na hawafanyi kazi yo yote. Akawaambia, ‘Ikiwa mtakwenda kufanya kazi shambani kwangu, nitawalipa kutokana na kazi yenu.’ Hivyo walikwenda kufanya kazi kwenye shamba lake la mizabibu.

Ilipofika saa sita mchana na saa tisa alasiri alitoka tena. Na nyakati zote mbili aliwaajiri watu wengine waende kufanya kazi shambani mwake. Ilipofika saa kumi na moja alikwenda sokoni tena. Akawaona watu wengine wamesimama pale. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa siku nzima na hamfanyi kazi?’

Wakasema, ‘Hakuna aliyetupa kazi.’

Mwenye shamba akawaambia, ‘Basi mnaweza kwenda kufanya kazi katika shamba langu la mizabibu.’

Mwishoni mwa siku, mwenye shamba akamwambia msimamizi wa wafanyakazi wote, ‘Waite wafanyakazi na uwalipe wote. Anza kwa kulipa watu niliowaajiri mwishoni, na malizia kwa wale niliowaajiri mwanzoni.’

Wafanyakazi walioajiriwa saa kumi na moja jioni walipata malipo yao. Kila mfanyakazi alipata sarafu moja ya fedha. 10 Ndipo wafanyakazi walioajiriwa kwanza wakaja kupokea malipo yao. Walidhani wangelipwa zaidi ya wengine. Lakini kila mmoja wao alipokea sarafu moja ya fedha. 11 Walipopata sarafu ya fedha, walimlalamikia mmiliki wa shamba. 12 Walisema, ‘Watu hao walioajiriwa mwishoni wamefanya kazi saa moja tu. Lakini umewalipa sawa na sisi. Na tumefanya kazi siku nzima kwenye jua kali.’

13 Lakini mmiliki wa shamba akamwambia mmoja wao, ‘Rafiki, nimekulipa kama tulivyopatana, ulikubali kufanya kazi kwa malipo ya sarafu moja ya fedha. Sawa? 14 Hivyo chukua malipo yako na uende. Ninataka kumlipa mtu niliyemwajiri mwishoni sawa na kiasi nilichokulipa. 15 Ninaweza kufanya chochote ninachotaka na pesa yangu. Wewe unao wivu[n] na unataka kuwadhuru wengine kwa kuwa mimi ni mkarimu?’

16 Hivyo walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo. Na walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo.”

Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake

(Mk 10:32-34; Lk 18:31-34)

17 Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, 18 “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. 19 Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.”

Mama Ataka Upendeleo Maalum kwa Wanaye

(Mk 10:35-45)

20 Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu.

21 Yesu akasema, “Unataka nini?”

Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.”

22 Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe[o] ambacho ni lazima nikinywee?”

Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!”

23 Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.”

24 Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. 25 Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi[p] wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. 26 Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. 28 Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.”

Yesu Awaponya Watu Wawili Wasiyeona

(Mk 10:46-52; Lk 18:35-43)

29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wanaondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Walikuwepo wasiyeona wawili wamekaa kando ya njia. Waliposikia kuwa Yesu anapita pale walipaza sauti wakasema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

31 Watu waliwakemea wale wasiyeona, wakawaambia wanyamaze. Lakini waliendelea kupaza sauti zao zaidi na zaidi, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali tusaidie!”

32 Yesu alisimama na kuwaambia, “Mnataka niwafanyie nini?”

33 Wakajibu, “Bwana, tunataka tuweze kuona.”

34 Yesu aliwahurumia wale wasiyeona. Akayagusa macho yao, na mara hiyo hiyo wakaanza kuona. Wakawa wafuasi wa Yesu.

Footnotes

  1. 17:4 vibanda vitatu Au “mahema matatu.” Neno hilo limetafsiriwa “hema takatifu” katika Agano la Kale. Hapa limetumika kwa maana ya mahali pa ibada.
  2. 17:10 lazima Eliya aje Tazama Mal 4:5-6.
  3. 17:21 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 21: “Lakini pepo wa aina hii hutoka kwa kufunga na kuomba.”
  4. 17:24 ushuru wa Hekalu Sarafu za kiyunani, drakma Mbili (pia katika mstari wa 27).
  5. 18:11 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 11: “Mwana wa Adamu amekuja kuokoa waliopotea.” Tazama Lk 19:10.
  6. 18:15 kwako Nakala bora za kale za Kiyunani hazina neno “kwako”.
  7. 18:16 Ndipo watakuwepo … kile kilichotokea Tazama Kum 19:15.
  8. 18:18 mnapotoa msamaha … wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “chochote mtakachokifunga hapa duniani kitakuwa kimefungwa mbinguni, na chochote mtakachokifungua kitakuwa kimefunguliwa mbinguni”.
  9. 18:22 saba mara sabini Ni idadi kubwa sana ya makosa, ikiwa na maana kuwa msamaha haupaswi kuwekewa kiwango.
  10. 18:24 tani 300 Kwa maana ya kawaida, “talanta 10,000”. Talanta 1 ilikuwa kama kilo 27 hadi 36 za sarafu za dhahabu, fedha, ama za shaba.
  11. 19:7 amri ya … ya talaka Tazama Kum 24:1.
  12. 19:12 wanaume hawaoi Kwa maana ya kawaida, “Maana wapo walio matowashi”.
  13. 19:19 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  14. 20:15 wivu Kwa maana ya kawaida, “Jicho lako lina uovu.” Kwa maana ya akasema mtu aliye na wivu anaweza kuleta madhara kwa mtu kwa kumkodolea macho tu. Imani hii ipo katika ukanda wa Bahari ya Kati hapo kale na hata leo.
  15. 20:22 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao. Pia katika mstari wa 23.
  16. 20:25 Watu Wasio Wayahudi Au “Mataifa”.