Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
10 Mungu aliyeumba vitu vyote na ambaye kwa utukufu wake vitu vyote vipo; alitaka watu wengi wawe watoto wake na kuushiriki utukufu wake. Hivyo alifanya yale aliyohitaji kuyafanya. Alimkamilisha yeye anayewaongoza watu hao kuuelekea wokovu. Kwa njia ya mateso yake Mungu alimfanya Yesu kuwa Mwokozi mkamilifu.
11 Yesu, ambaye anawafanya watu kuwa watakatifu, na wale wanaofanywa kuwa watakatifu wanatoka katika familia moja. Hivyo haoni aibu kuwaita kaka na dada zake. 12 Anasema,
“Mungu, nitawaeleza kaka na dada zangu habari zako.
Mbele za watu wako wote nitaziimba sifa zako.”(A)
13 Pia anasema,
“Nitamwamini Mungu.”(B)
Na pia anasema,
“Nipo hapa, na pamoja ni wapo watoto
niliopewa na Mungu.”(C)
14 Watoto hawa ni watu walio na miili ya damu na nyama. Hivyo Yesu mwenyewe akawa kama wao na akapata uzoefu ule ule waliokuwa nao. Yesu alifanya hivi ili, kwa kufa kwake, aweze kumharibu yeye aliye na nguvu ya mauti, Ibilisi. 15 Yesu akawa kama watu hawa na akafa ili aweze kuwaweka huru. Walikuwa kama watumwa maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa kwao kifo. 16 Kwa uwazi, siyo malaika ambao Yesu huwasaidia. Yeye huwasaidia watu waliotoka kwa Ibrahimu. 17 Kwa sababu hii, Yesu alifanyika kama sisi, kaka na dada zake kwa kila namna. Akawa kama sisi ili aweze kuhudumu kwa niaba yetu mbele za Mungu wa kuhani mkuu aliye mwaminifu na mwenye rehema. Ndipo angetoa sadaka ya kuziondoa dhambi za watu. 18 Na sasa anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa. Yuko radhi kuwasaidia kwa sababu yeye mwenyewe aliteseka na alijaribiwa.
Yesu Apelekwa Uhamishoni Misri
13 Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.”
14 Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. 15 Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.”(A)
Herode Aua Watoto wa Kiume Katika Mji wa Bethlehemu
16 Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. 17 Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema:
18 “Sauti imesikika Rama,
sauti ya kilio na huzuni kuu.
Raheli akiwalilia watoto wake,
na amekataa kufarijiwa
kwa sababu watoto wake hawapo tena.”(B)
Yusufu na Familia Yake Warudi Kutoka Misri
19 Wakati Yusufu na familia yake wakiwa Misri, Herode alifariki. Malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto 20 na akamwambia, “Damka! Mchukue mtoto na mama yake urudi Israeli, kwani waliojaribu kumwua mtoto wamekwisha kufa.”
21 Hivyo Yusufu alidamka na kumchukua mtoto Yesu na mama yake na kurudi Israeli. 22 Lakini Yusufu aliposikia kuwa Arkelao alikuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake kufa, aliogopa kwenda huko. Lakini baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto, Yusufu aliondoka pamoja na familia yake akaenda sehemu za Galilaya. 23 Alikwenda katika mji wa Nazareti na kukaa huko. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yale yaliyosemwa na manabii. Mungu alisema Masihi angeitwa Mnazareti.[a]
© 2017 Bible League International