Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
68 “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amekuja kuwasaidia
watu wake na kuwaweka huru.
69 Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70 Hivi ndivyo alivyoahidi
kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71 Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
na milki za wote wanaotuchukia.
72 Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73 Agano hili ni kiapo alichomwapia
baba yetu Ibrahimu.
74 Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75 Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
mbele zake siku zote za maisha yetu.
76 Sasa wewe, mtoto mdogo,
utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
kuandaa njia yake.
77 Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
kwa kusamehewa dhambi zao.
78 Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
siku mpya[a] itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79 Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
katika njia ya amani.”
Yesu Kristo ni Dhabihu yetu kwa Ajili ya Dhambi
23 Mambo haya ni nakala ya mambo halisi yaliyoko mbinguni. Nakala hizi zinapaswa kutakaswa kwa sadaka ya wanyama. Lakini mambo halisi yaliyoko mbinguni yanapaswa kuwa na sadaka zilizo bora zaidi. 24 Kristo alienda katika Patakatifu pa Patakatifu. Lakini hapakuwa mahali palipotengenezwa na mwanadamu, ambapo ni nakala tu ya ile iliyo halisi. Alienda katika mbingu, na yuko huko sasa mbele za Mungu ili atusaidie sisi.
25 Kuhani mkuu huingia katika Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kila mwaka. Huchukua pamoja naye damu ya sadaka. Lakini hatoi damu yake kama alivyofanya Kristo. Kristo alienda mbinguni, lakini siyo kujitoa mwenyewe mara nyingi kama ambavyo kuhani mkuu hutoa damu tena na tena. 26 Kama Kristo alijitoa mwenyewe mara nyingi, basi angehitaji kuteseka mara nyingi tangu wakati dunia ilipoumbwa. Lakini alikuja kujitoa mwenyewe mara moja tu. Na mara hiyo moja inatosha kwa nyakati zote. Alikuja katika wakati ambao ulimwengu unakaribia mwisho. Alikuja kuchukua dhambi zote kwa kujitoa mwenyewe kama sadaka.
27 Kila mtu atakufa mara moja tu. Baada ya hapo ni kuhukumiwa. 28 Hivyo Kristo alitolewa kama sadaka mara moja kuchukua dhambi za watu wengi. Na atakuja mara ya pili, lakini siyo kujitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi. Atakuja mara ya pili kuleta wokovu kwa wale wanaomngojea.
© 2017 Bible League International