Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mungu Anataka Tumwombee Kila Mtu
2 Kwanza kabisa, ninakuagiza uwaombee watu wote. Uwaombee kwa Mungu ili awabariki na kuwapa mahitaji yao. Kisha umshukuru Yeye. 2 Unapaswa kuwaombea watawala na wote wenye mamlaka. Uwaombee viongozi hawa ili tuweze kuishi maisha yenye utulivu na amani, maisha yaliyojaa utukufu kwa Mungu na yanayostahili heshima. 3 Hili ni jambo jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu.
4 Mungu anataka kila mtu aokolewe na aielewe kweli kikamilifu. 5 Kuna Mungu mmoja tu, na kuna mwanadamu mmoja tu anayeweza kuwaleta pamoja wanadamu wote na Mungu wao. Huyo mtu ni Kristo Yesu kama mwanadamu. 6 Alijitoa mwenyewe kulipa deni ili kila mtu awe huru. Huu ni ujumbe ambao Mungu alitupa wakati unofaa. 7 Nami nilichaguliwa kama mtume kuwaambia watu ujumbe huo. Ninasema kweli. Sidanganyi. Nilichaguliwa kuwafundisha wasio Wayahudi na nimefanya kazi hii kwa imani na ukweli.
Utajiri Halisi
16 Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. 2 Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’
3 Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. 4 Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’
5 Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ 6 Akamjibu, ‘Ananidai mitungi[a] 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’
7 Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo[b] mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’
8 Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu.
9 Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. 10 Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. 11 Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. 12 Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe.
13 Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.”[c]
© 2017 Bible League International