Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu atupaye tumaini.
2 Ninakuandikia wewe, Timotheo. Wewe ni kama mwanangu halisi kwa sababu ya imani yetu.
Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu ziwe pamoja nawe.
Maonyo kuhusu Mafundisho ya Uongo
3 Nilipokwenda Makedonia, nilikuomba ubaki Efeso. Baadhi ya watu huko wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, nami ninataka uwaonye waache. 4 Uwaambie wasitumie muda wao kusimulia simulizi zisizo na maana za mambo ya kale na kutengeneza orodha ndefu ya mababu. Mambo hayo husababisha mabishano tu na hayaisaidii katika kuikamilisha kazi ya Mungu tuliyopewa, ambayo ni lazima tuikamilishe kwa imani. 5 Kusudi langu la kukueleza ufanye jambo hili ni kutaka kukuza upendo; aina ya upendo unaooneshwa na wale ambao mawazo yao ni safi; watu ambao hufanya yale wanayojua kuwa ni sahihi na ambao imani yao kwa Mungu ni ya kweli. 6 Lakini wengine wamekosa jambo hili la msingi katika mafundisho yao na wamepoteza mwelekeo. Sasa wanazungumza juu ya mambo yasiyo na msaada kwa mtu yeyote. 7 Wanataka kuwa walimu wa sheria,[b] lakini hawafahamu mambo wanayosema, wanasema kwa ujasiri wote juu ya mambo wasiyoyaelewa wenyewe.
8 Tunajua kwamba sheria ni nzuri ikiwa mtu anaitumia kwa usahihi. 9 Pia tunajua kwamba sheria haikutengenezwa kwa ajili ya wale wanaotenda haki. Imetengenezwa kwa ajili ya wale wanayoipinga na kukataa kuifuata. Sheria ipo kwa ajili ya wenye dhambi wanaompinga Mungu na mambo yote yanayompendeza. Ipo kwa ajili ya wale wasio na hamu ya mambo ya kiroho na kwa ajili ya wale wanaowaua baba au mama zao au mtu yeyote yule. 10 Ipo kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi ya uasherati, kwa wanaume wanaolala na wanaume wenzao au wavulana, kwa wote wanaoteka watu na kuwauza kama watumwa, kwa wote wanaodanganya au wale wasiosema ukweli wakiwa katika kiapo, na kwa ajili ya wale walio kinyume na mafundisho ya kweli ya Mungu. 11 Mafundisho hayo ni sehemu ya Habari Njema ambayo Mungu wetu wa utukufu alinipa kuhubiri na ndani yake tunauona utukufu wake.
© 2017 Bible League International