Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Siri ya Maisha Yetu
14 Ninatarajia kuja kwenu hivi karibuni. Lakini ninakuandikia maneno haya sasa, 15 ili kwamba, hata kama sitakuja mapema, utafahamu jinsi ambavyo watu wanapaswa kuishi katika familia[a] ya Mungu. Familia hiyo ni kanisa la Mungu aliye hai. Na Kanisa la Mungu ni msaada na msingi wa ukweli. 16 Ndiyo, Mungu ametuonesha siri ya maisha yanayompa heshima na kumpendeza Yeye. Siri hii ya ajabu ni ukweli ambao wote tunakubaliana nao:
Kristo[b] alijulikana kwetu katika umbile la kibinadamu;
alioneshwa na Roho[c] kuwa kama alivyojitambulisha;
alionwa na malaika.
Ujumbe kuhusu Yeye ulitangazwa kwa mataifa;
watu ulimwenguni walimwamini;
alichukuliwa juu mbinguni katika utukufu.
Maonyo juu ya Walimu wa uongo
4 Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. 3 Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. 4 Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. 5 Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi.
© 2017 Bible League International