Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tuishi kwa Kusaidiana Sisi kwa Sisi
6 Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi. 2 Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya. 3 Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe. 4 Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote. 5 Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya.
Msiache Kutenda Mema
6 Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo.
7 Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda. 8 Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele. 9 Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa. 10 Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini.
Paulo Amalizia Barua Yake
11 Huu ni mwandiko wa mkono wangu mwenyewe. Mnaweza kuona jinsi herufi zilivyo kubwa.[a] 12 Watu wale wanaojaribu kuwalazimisha ninyi kutahiriwa wanafanya hivyo ili wawaridhishe Wayahudi wenzao. Wanaogopa wasije wakateswa kwa sababu ya msalaba[b] wa Kristo. 13 Maana hata wale waliotahiriwa hawaitii sheria. Na bado wanawataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujisifu kwa ajili ya yale waliyowatendea ninyi.
14 Mimi nisijisifu kwa ajili ya mambo kama haya. Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo sababu pekee ya kujivuna kwangu. Kupitia kifo cha Yesu msalabani ulimwengu ukafa[c] kwangu, nami nimeufia ulimwengu. 15 Haijalishi kwamba mtu ametahiriwa au hajatahiriwa. Kinachojalisha ni uumbaji mpya wa Mungu katika Kristo.[d] 16 Amani iwe kwa wale wote wanaoifuata njia hii mpya. Na rehema za Mungu ziwe juu ya watu wake Israeli.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake 72
10 Baada ya hili, Bwana alichagua wafuasi sabini na wawili[a] zaidi. Aliwatuma watangulie katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda wakiwa wawili wawili. 2 Aliwaambia, “Kuna mavuno mengi ya watu wa kuwaingiza katika Ufalme wa Mungu. Lakini watenda kazi wa kuwaingiza katika ufalme wa Mungu ni wachache. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni ili atume watenda kazi wengi ili wasaidie kuyaingiza mavuno yake.
3 Mnaweza kwenda sasa. Lakini sikilizeni! Ninawatuma na mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. 4 Msibebe mfuko wowote, wala pesa au viatu. Msisimame kusalimiana na watu njiani. 5 Kabla ya kuingia katika nyumba, mseme, ‘Amani iwemo katika nyumba hii.’ 6 Ikiwa watu wanaoishi katika nyumba hiyo wanapenda amani, baraka yenu ya amani itakaa nao. Lakini kama siyo, baraka yenu ya amani itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba inayopenda amani. Kuleni na kunywa chochote watakachowapa kwa maana mfanyakazi anastahili ujira. Msihame kutoka katika nyumba hiyo na kwenda kukaa katika nyumba nyingine.
8 Mkiingia katika mji wowote na watu wakawakaribisha, kuleni vyakula watakavyowapa. 9 Waponyeni wagonjwa wanaoishi katika mji huo, na waambieni Ufalme wa Mungu umewafikia![b]
10 Lakini mkiingia katika mji wowote na watu wasiwakaribishe, nendeni katika mitaa ya mji huo na mseme, 11 ‘Tunafuta mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana katika miguu yetu! Lakini kumbukeni kwamba: Ufalme wa Mungu umewafikia!’
16 Mtu yeyote akiwasikiliza ninyi wafuasi wangu, hakika ananisikiliza mimi. Lakini mtu yeyote akiwakataa ninyi, hakika ananikataa mimi. Na mtu yeyote akinikataa mimi anamkataa Yule aliyenituma.”
Shetani Aangushwa
17 Wale wafuasi sabini na wawili waliporudi kutoka katika safari yao, walikuwa na furaha sana. Walisema, “Bwana, hata pepo walitutii tulipotumia jina lako!”
18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kama mwanga wa radi kutoka mbinguni! 19 Yeye ndiye adui, lakini tambueni kuwa nimewapa mamlaka zaidi yake. Nimewapa mamlaka ya kuponda nyoka na nge zake kwa miguu yenu. Hakuna kitakachowadhuru. 20 Ndiyo, hata pepo wanawatii. Na mnaweza kufurahi, lakini si kwa sababu mna mamlaka hii. Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
© 2017 Bible League International