Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Vita ndani Yetu
14 Tunafahamu kuwa sheria ni ya rohoni, lakini mimi si wa rohoni. Mimi ni mwanadamu hasa. Dhambi inanitawala kana kwamba mimi ni mtumwa wake. 15 Sielewi ni kwa nini ninatenda jinsi ninavyotenda. Sitendi mema ninayotaka kuyatenda, bali ninatenda maovu ninayoyachukia. 16 Na ikiwa ninatenda kile nisichotaka kutenda, inamaanisha kuwa ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini kwa hakika siyo mimi mwenyewe ninayetenda maovu. Bali dhambi inayokaa ndani yangu ndiyo inatenda hayo. 18 Ndiyo, ninajua kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu, nina maana kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu kisichokuwa cha rohoni. 19 Sitendi mema ninayotaka nitende. Ninatenda maovu nisiyotaka kutenda. 20 Hivyo ikiwa ninatenda yale nisiyotaka kutenda, hakika si mimi ninayeyatenda hayo. Bali dhambi inayoishi ndani yangu ndiyo inayotenda.
21 Hivyo nimejifunza hivi kuhusu sheria: Ninapotaka kutenda mema ambayo sheria inaamrisha, uovu unakuwa hapo hapo pamoja nami. 22 Moyoni mwangu nafurahi kuifuata sheria ya Mungu. 23 Lakini naiona “sheria” nyingine ikitenda kazi ndani yangu, nayo imo vitani dhidi ya sheria inayokubalika akilini mwangu. “Sheria” hii nyingine ni utawala wa dhambi inayonishinda na inanifanya kuwa mfungwa wake. 24 Mimi ni mtu mwenye taabu kiasi gani! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu unaoniletea kifo? 25 Namshukuru Mungu kwa wokovu wake kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo katika ufahamu wangu mimi ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika udhaifu wangu wa kibinadamu mimi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
© 2017 Bible League International