Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
7 Kristo alimpa kila mmoja wetu karama. Kila mmoja alipokea kwa jinsi alivyopenda yeye kuwapa. 8 Ndiyo maana Maandiko yanasema,
“Alipaa kwenda mahali pa juu sana;
aliwachukua wafungwa pamoja naye,
na akawapa watu vipawa.”(A)
9 Inaposema, “Alipaa juu,” inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa kwanza alikuja chini duniani. 10 Hivyo Kristo alishuka chini, na ndiye aliyekwenda juu. Alikwenda juu ya mbingu za juu zaidi ili avijaze vitu vyote pamoja naye. 11 Na Kristo huyo huyo aliwapa watu hawa vipawa: aliwafanya wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kwenda na kuhubiri Habari Njema, na wengine kuwa wachungaji[a] ili wawafundishe watu wa Mungu. 12 Mungu aliwapa hao ili kuwaandaa watakatifu wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma, kuufanya imara mwili wa Kristo. 13 Kazi hii inabidi iendelee hadi wote tutakapounganishwa pamoja katika lile tunaloliamini na tunalolijua kuhusu Mwana wa Mungu. Lengo letu ni kufanana na mtu mzima aliyekomaa na kuwa kama Kristo tukiufikia ukamilifu wake wote.
14 Ndipo tutakapokuwa si kama watoto wachanga. Hatutakuwa watu ambao nyakati zote hubadilika kama meli inayochukuliwa na mawimbi huku na kule. Hatutaweza kuathiriwa na fundisho lolote jipya tutakalosikia kutoka kwa watu wanaojaribu kutudanganya. Hao ni wale wanaoweka mipango ya ujanja na kutumia kila aina ya mbinu kuwadanganya wengine waifuate njia iliyopotoka. 15 Hapana, tunapaswa kusema ukweli kwa upendo. Tutakua na kuwa kama Kristo katika kila njia. Yeye ni kichwa, 16 na mwili wote unamtegemea yeye. Viungo vyote vya mwili vimeunganishwa na kushikanishwa pamoja, huku kila kiungo kikitenda kazi yake. Hili huufanya mwili wote ukue na kujengeka katika upendo.
© 2017 Bible League International