Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
27 Askari waliwaleta mitume na kuwasimamisha mbele ya baraza. Kuhani mkuu akawauliza. 28 Akisema, “Tuliwaambia msifundishe tena kwa kutumia jina lile. Lakini tazameni mlichofanya! Mmeujaza mji wa Yerusalemu kwa mafundisho yenu. Na mnajaribu kutulaumu sisi kwa sababu ya kifo chake.”
29 Petro na mitume wengine wakajibu, “Ni lazima tumtii Mungu, siyo wanadamu! 30 Mlimwua Yesu kwa kumpigilia msalabani. Lakini Mungu, Mungu yule yule wa Baba zetu, alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. 31 Yesu ndiye ambaye Mungu amemtukuza kwa kumpa nafasi upande wake wa kuume. Amemfanya kuwa Kiongozi na Mwokozi wetu. Mungu alifanya hivi ili kuwapa watu wote wa Israeli fursa ya kubadilika na kumgeukia Mungu ili dhambi zao zisamehewe. 32 Tuliona mambo haya yote yakitokea, na tunathibitisha kuwa ni ya kweli. Pia, Roho Mtakatifu anaonesha kuwa mambo haya ni ya kweli. Mungu amemtoa Roho huyu kwa ajili ya wote wanaomtii Yeye.”
Yohana Ayaandikia Makanisa
4 Kutoka kwa Yohana,
Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; 5 na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.
Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. 6 Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.
7 Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma.[a] Watu wote wa dunia watamwombolezea.[b] Ndiyo, hili litatokea! Amina.
8 Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega.[c] Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.”
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Lk 24:36-49)
19 Ilikuwa siku ya Jumapili, na jioni ile wafuasi walikuwa pamoja. Nao walikuwa wamefunga milango kwa kuwa waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ghafla, Yesu akawa amesimama pale katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Mara baada ya kusema haya, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Wafuasi walipomwona Bwana, walifurahi sana.
21 Kisha Yesu akasema tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma, nami sasa nawatuma ninyi vivyo hivyo.” 22 Kisha akawapumulia pumzi na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkisamehe dhambi zake mtu yeyote, dhambi zake hizo zitasamehewa. Kama kuna mtu yeyote ambaye hamtamsamehe dhambi zake, dhambi zake huyo hazitasamehewa.”
Yesu Amtokea Tomaso
24 Tomaso (aliyeitwa Pacha) alikuwa ni mmoja wa wale kumi na mbili, lakini hakuwapo pamoja na wafuasi wengine Yesu alipokuja. 25 Wakamwambia, “Tulimwona Bwana.” Tomaso akasema, “Hiyo ni ngumu kuamini. Ninahitaji kuona makovu ya misumari katika mikono yake, niweke vidole vyangu ubavuni. Ndipo tu nitakapoamini.” 26 Juma moja baadaye wafuasi walikuwemo katika nyumba ile tena, na Tomaso alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja na kusimama katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa. Iangalie mikono yangu. Weka mkono wako hapa ubavuni mwangu. Acha kuwa na mashaka na uamini.”
28 Tomaso akamwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa sababu umeniona. Wana baraka nyingi watu wale wanaoniamini bila kuniona!”
Kwa Nini Yohana Aliandika Kitabu hiki
30 Yesu alifanya ishara nyingine nyingi za miujiza ambazo wafuasi wake waliziona, na ambazo hazikuandikwa kwenye kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili muweze kuamini kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu. Kisha, kwa kuamini, mpate uzima kupitia jina lake.
© 2017 Bible League International