Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
10 Mungu aliyeumba vitu vyote na ambaye kwa utukufu wake vitu vyote vipo; alitaka watu wengi wawe watoto wake na kuushiriki utukufu wake. Hivyo alifanya yale aliyohitaji kuyafanya. Alimkamilisha yeye anayewaongoza watu hao kuuelekea wokovu. Kwa njia ya mateso yake Mungu alimfanya Yesu kuwa Mwokozi mkamilifu.
11 Yesu, ambaye anawafanya watu kuwa watakatifu, na wale wanaofanywa kuwa watakatifu wanatoka katika familia moja. Hivyo haoni aibu kuwaita kaka na dada zake. 12 Anasema,
“Mungu, nitawaeleza kaka na dada zangu habari zako.
Mbele za watu wako wote nitaziimba sifa zako.”(A)
13 Pia anasema,
“Nitamwamini Mungu.”(B)
Na pia anasema,
“Nipo hapa, na pamoja ni wapo watoto
niliopewa na Mungu.”(C)
14 Watoto hawa ni watu walio na miili ya damu na nyama. Hivyo Yesu mwenyewe akawa kama wao na akapata uzoefu ule ule waliokuwa nao. Yesu alifanya hivi ili, kwa kufa kwake, aweze kumharibu yeye aliye na nguvu ya mauti, Ibilisi. 15 Yesu akawa kama watu hawa na akafa ili aweze kuwaweka huru. Walikuwa kama watumwa maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa kwao kifo. 16 Kwa uwazi, siyo malaika ambao Yesu huwasaidia. Yeye huwasaidia watu waliotoka kwa Ibrahimu. 17 Kwa sababu hii, Yesu alifanyika kama sisi, kaka na dada zake kwa kila namna. Akawa kama sisi ili aweze kuhudumu kwa niaba yetu mbele za Mungu wa kuhani mkuu aliye mwaminifu na mwenye rehema. Ndipo angetoa sadaka ya kuziondoa dhambi za watu. 18 Na sasa anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa. Yuko radhi kuwasaidia kwa sababu yeye mwenyewe aliteseka na alijaribiwa.
© 2017 Bible League International