Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tahadhari Kutokana na Yaliyotokea Zamani
10 Ndugu zangu, sitaki mshindwe kutambua umuhimu wa kile kilichowatokea baba zetu waliokuwa na Musa. Walifunikwa na wingu,[a] na walipita katika bahari. 2 Walibatizwa[b] wote katika Musa katika wingu na katika bahari. 3 Wote walikula chakula kilichotolewa na Roho wa Mungu, 4 na wote walikunywa kinywaji kinachotolewa na Roho wa Mungu. Kinywaji walichokunywa kilitoka katika mwamba wa roho uliokuwa pamoja nao, na mwamba huo ni Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, na hivyo waliangamizwa jangwani.
6 Mambo haya yaliyotokea ni tahadhali kwa ajili yetu. Mifano hii itufanye tuache kutamani maovu kama baadhi yao walivyofanya. 7 Msiabudu sanamu kama ambavyo baadhi yao walifanya. Na kama Maandiko yanavyosema, “Waliketi chini kula na kunywa kisha wakasimama kucheza.”(A) 8 Tusifanye dhambi ya uzinzi kama baadhi yao walivyofanya na watu ishirini na tatu elfu miongoni mwao wakafa. 9 Tusimjaribu Kristo[c] kama vile baadhi yao walivyofanya. Kwa sababu hiyo, waliuawa na nyoka. 10 Na msinung'unike kama baadhi yao walivyofanya na wakauawa na malaika anayeangamiza.
11 Mambo yaliyowapata wale watu ni mifano na yaliandikwa ili kututahadharisha sisi tunaoishi nyakati hizi za mwisho. 12 Hivyo kila anayedhani kuwa yuko imara katika imani yake, basi awe mwangalifu asianguke. 13 Majaribu mliyonayo ni yale yale waliyonayo watu wote. Lakini Mungu ni mwaminifu maana hataacha mjaribiwe kwa kiwango msichoweza kustahimili. Mnapojaribiwa, Mungu atawapa mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Ndipo mtaweza kustahimili.
Badilisheni Namna Mnavyoishi
13 Sehemu ya watu waliokuwa pamoja na Yesu pale, walimweleza kilichowapata baadhi ya waabuduo kutoka Galilaya. Pilato alikuwa ameamuru wauawe. Damu zao zilichanganywa na damu za wanyama waliowaleta kwa ajili ya kutoa dhabihu. 2 Yesu alijibu akasema, “Mnadhani hili liliwapata watu hao kwa sababu walikuwa wenye dhambi kuliko watu wengine wote wa Galilaya? 3 Hapana, hawakuwa hivyo. Lakini ikiwa hamtaamua kubadili maisha yenu sasa, ninyi nyote mtaangamizwa kama wao! 4 Na vipi kuhusu wale watu kumi na wanane waliokufa pale mnara wa Siloamu ulipowaangukia? Mnadhani walikuwa na dhambi kuliko watu wengine katika mji wa Yerusalemu? 5 Hawakuwa hivyo. Lakini ninawaambia, ikiwa hamtaamua kubadilika sasa, hata ninyi mtaangamizwa pia!”
Mti Usiozaa Matunda
6 Yesu akawasimulia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa amepanda mtini katika shamba lake. Alipokuja kutafuta matunda kwenye mtini huo hakupata tunda lolote. 7 Alikuwa na mtumishi aliyekuwa akilitunza shamba. Hivyo alimwambia mtumishi wake, ‘Nimekuwa nikitafuta matunda kwenye mti huu kwa miaka mitatu, lakini sijawahi kupata tunda lolote. Ukate mti huu! Kwa maana unaiharibu ardhi.’ 8 Lakini mtumishi alijibu, ‘Mkuu, tuuache mti huu mwaka mmoja zaidi ili tuone ikiwa utazaa matunda. Nitakusanya samadi kuuzunguka ili kuupa mbolea. 9 Unaweza kuzaa matunda mwaka ujao. Ikiwa hautazaa, ndipo utaweza kuukata.’”
© 2017 Bible League International