Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
20 Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa. 21 Kifo huja kwa watu kwa sababu ya tendo la mtu mmoja. Lakini sasa kuna ufufuo kutoka kwa wafu kwa sababu ya mtu mwingine. 22 Ndiyo, kwa sababu sisi sote ni wa Adamu, sisi sote tunakufa. Kwa njia hiyo hiyo, sisi sote tulio wa Kristo, tutakuwa hai tena. 23 Lakini kila mmoja atafufuliwa kwa mpango sahihi. Kristo alikuwa wa kwanza kufufuliwa. Kisha atakaporudi, wale walio wake watafufuliwa. 24 Ndipo mwisho utakuja. Kristo atamwangamiza kila mtawala na kila mamlaka na nguvu. Kisha atampa Mungu Baba ufalme.
25 Kristo lazima atawale mpaka Mungu atakapowaweka adui zake wote chini ya udhibiti wake.[a] 26 Adui wa mwisho kuangamizwa ni kifo. 27 Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu ameweka kila kitu chini ya udhibiti wake.”(A) Inaposema “kila kitu” kimewekwa chini yake, hii ni wazi Mungu peke yake ndiye ambaye hayuko chini yake. Mungu ndiye anayeweka kila kitu chini ya udhibiti wa Kristo. 28 Baada ya kuweka kila kitu chini ya Kristo, ndipo yeye mwenyewe, kama Mwana, atawekwa chini ya Mungu. Katika namna hii Mungu atakuwa mtawala mkuu juu ya kila kitu.
29 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao?
30 Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote? 31 Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu. 32 Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.”(B)
33 Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.” 34 Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe.
© 2017 Bible League International