Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tutafufuliwa Kutoka kwa Wafu
12 Tunamwambia kila mtu kuwa Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo kwa nini baadhi yenu mnasema watu hawatafufuliwa kutoka kwa wafu? 13 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu. 14 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa, ujumbe tunaowahubiri ni bure. Na imani yenu ni bure. 15 Nasi tutakuwa na hatia ya kutoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumewahubiri watu kuhusu Yeye, kwa kusema kuwa alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Na ikiwa hakuna anayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Mungu hakumfufua Kristo. 16 Ikiwa wale waliokufa hawatafufuliwa, basi Kristo hakufufuliwa pia. 17 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, basi imani yenu ni bure; bado mngali watumwa wa dhambi zenu. 18 Na watu wa Kristo waliokwisha kufa wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu katika Kristo ni kwa ajili tu ya maisha haya hapa duniani, basi watu watuhurumie sisi kuliko mtu mwingine yeyote.
20 Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa.
Yesu Afundisha na Kuponya Watu
(Mt 4:23-25; 5:1-12)
17 Yesu na mitume wakatelemka kutoka mlimani. Yesu akasimama mahali tambarare. Kundi kubwa la wafuasi wake lilikuwa pale. Walikuwepo pia watu wengi waliotoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu, na maeneo ya pwani karibu na Tiro na Sidoni. 18 Wote walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya watu waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo. 19 Kila mtu alijaribu kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa unamtoka. Yesu aliwaponya wote.
20 Yesu akawatazama wafuasi wake na kusema,
“Heri ninyi mlio maskini.
Maana Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri ninyi mlio na njaa sasa.
Maana mtashibishwa.
Heri ninyi mnaolia sasa.
Maana mtafurahi na kucheka.
22 Watu watawachukia kwa sababu ninyi ni wa milki ya Mwana wa Adamu. Watawabagua na watawatukana. Watajisikia vibaya hata kutamka majina yenu. Mambo haya yatakapotukia, mjue kuwa baraka kuu ni zenu. 23 Ndipo mfurahi na kurukaruka kwa furaha, kwa sababu mna thawabu kuu mbinguni. Baba zao waliwafanyia manabii vivyo hivyo.
24 Lakini ole wenu ninyi matajiri,
kwa kuwa mmekwishapata maisha yenye raha.
25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
kwa kuwa mtasikia njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
kwa kuwa mtalia na kuhuzunika.
26 Ole wenu watu wote wanapowasifu ninyi. Maana mababu zao waliwasifu manabii wa uongo vivyo hivyo daima.
© 2017 Bible League International