Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yatoeni Maisha Yenu kwa Mungu
12 Hivyo, dada na kaka zangu, upokeeni wema mkuu ambao Mungu alituonyesha. Itoeni miili yenu[a] kama sadaka hai kwake. Ishini kwa ajili ya Mungu tu na mweze kumpendeza yeye. Mkizingatia kwa makini yale aliyoyatenda, ni sahihi na inapasa kumwabudu Mungu kwa njia hii. 2 Msifikiri au kuenenda kama watu wa ulimwengu huu, bali mruhusuni Mungu aibadilishe namna yenu ya kufikiri ndani yenu. Ndipo mtaweza kuelewa na kuyathibitisha yale Mungu anayotaka kutoka kwenu; yote yaliyo mema, yanayompendeza yeye na yaliyo makamilifu.
3 Mungu amenipa mimi zawadi maalumu, na ndiyo sababu nina kitu cha kusema na kila mmoja wenu. Msifikiri kuwa ninyi ni bora kuliko jinsi mlivyo kwa asili. Mnapaswa kujiona kadri mlivyo. Mjipime wenyewe jinsi mlivyo kwa imani ambayo Mungu alimpa kila mmoja wetu. 4 Kila mmoja wetu anao mwili mmoja, na mwili huo una viungo vingi. Viungo hivi vyote havifanyi mambo yanayofanana. 5 Kwa jinsi hiyo hiyo, sisi ni watu wengi, lakini kwa sababu ni wa Kristo, sote ni mwili mmoja. Sisi sote ni viungo vya mwili huo, na kila kiungo ni sehemu ya viungo vingine vyote.
6 Sote tunazo karama tofauti tofauti. Kila karama ilikuja kwa sababu ya neema aliyotupa Mungu. Yule aliye na karama ya unabii anapaswa kuitumia karama hiyo kwa namna inayokubalika kiimani. 7 Aliye na karama ya kuhudumia anapaswa kuhudumia. Aliye na karama ya kufundisha anapaswa kufundisha. 8 Aliye na karama ya kufariji wengine anapaswa kufanya hivyo. Aliye na karama ya kuhudumia mahitaji ya wengine anapaswa kutoa kwa moyo mweupe. Aliye na karama ya kuongoza anapaswa kufanya kwa juhudi katika hiyo. Aliye na karama ya kuonesha wema kwa wengine anapaswa kufanya hivyo kwa furaha.
© 2017 Bible League International