Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
5 Hatuwaambii watu habari zetu wenyewe. Lakini tunawaambia habari za Kristo Yesu kuwa ni Bwana, na tunawaambia kuwa sisi ni watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kuna wakati Mungu alisema, “Na nuru ing'ae gizani”[a] na huyu ni Mungu yule yule anayesababisha nuru ing'ae katika mioyo yetu ili tutambue utukufu wa uungu wake mkuu unaongaa katika sura ya Kristo.
7 Tuna hazina hii kutoka kwa Mungu, lakini sisi ni kama vyombo vya udongo tu vinavyobeba hazina. Hii ni kuonesha kuwa nguvu ya kustaajabisha tuliyo nayo inatoka kwa Mungu, si kwetu. 8 Tunasumbuliwa kila upande, lakini hatushindwi. Mara kwa mara hatujui tufanye nini, lakini hatukati tamaa. 9 Tunateswa, lakini Mungu hatuachi. Tunaangushwa chini wa nyakati zingine, laki hatuangamizwi. 10 Hivyo tunashiriki kifo cha Yesu katika miili yetu kila wakati, lakini haya yanatokea ili uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu. 11 Tuko hai, lakini kwa ajili ya Yesu tupo katika hatari ya kifo kila wakati, ili kwamba uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu ya kufa. 12 Kwa hiyo kifo kinafanya kazi ndani yetu, lakini matokeo yake ni kwamba uzima unafanya kazi ndani yenu.
Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato
(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)
23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”
25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”
27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
3 Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2 Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. 3 Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4 Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5 Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6 Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
© 2017 Bible League International