Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Ushindi Dhidi ya Ulimwengu
25 Nimewaambia mambo haya kwa kutumia maneno yenye mafumbo. Isipokuwa utakuja wakati ambapo sitatumia tena maneno ya jinsi hiyo kuwaeleza mambo. Nami nitasema nanyi kwa maneno ya wazi wazi juu ya Baba. 26 Kisha, mtaweza kumwomba Baba vitu kwa jina langu. Sisemi kwamba nitapaswa kumwomba Baba kwa ajili yenu. 27 Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu ninyi mmenipenda mimi. Naye anawapenda kwa sababu mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28 Mimi nimetoka kwa Baba kuja ulimwenguni. Sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29 Kisha wafuasi wake wakasema, “Tayari unaongea nasi wazi wazi. Hutumii tena maneno yanayoficha maana. 30 Sasa tunatambua kuwa unajua mambo yote. Wewe unajibu maswali yetu hata kabla hatujayauliza. Hii inatufanya tuamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31 Yesu akasema, “Kwa hiyo sasa mnaamini? 32 Basi nisikilizeni! Wakati unakuja mtakapotawanywa, kila mmoja nyumbani kwake. Kwa hakika, wakati huo tayari umekwisha fika. Ninyi mtaniacha, nami nitabaki peke yangu. Lakini kamwe mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami.
33 Nimewaambia mambo haya ili muwe na amani ndani yangu. Katika ulimwengu huu mtapata mateso. Lakini muwe jasiri! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
© 2017 Bible League International