Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
11 Kila siku makuhani husimama na kutekeleza shughuli zao za kidini. Tena na tena hutoa sadaka zilezile, ambazo kamwe haziwezi kuondoa dhambi. 12 Lakini Kristo alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya dhambi, na sadaka hiyo ni nzuri kwa nyakati zote. Kisha akakaa mkono wa kuume wa Mungu. 13 Na sasa Kristo anawasubiria hapo adui zake wawekwe chini ya mamlaka yake.[a] 14 Kwa sadaka moja Kristo akawakamilisha watu wake milele. Ndio wale wanaotakaswa.
15 Roho Mtakatifu pia anatuambia juu ya hili. Kwanza anasema:
16 “Hili ndilo agano[a] nitakaloweka
na watu wangu baadaye, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu ndani ya mioyo yao.
Nitaziandika sheria zangu katika fahamu zao.”(A)
17 Kisha anasema,
“Nitazisahau dhambi zao
na nisikumbuke kamwe uovu walioutenda.”(B)
18 Na baada ya kila kitu kusamehewa, hakuna tena haja ya sadaka ili kuziondoa dhambi.
Mkaribieni Mungu
19 Hivyo ndugu na dada, tuko huru kabisa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu. Tunaweza kufanya hivi bila hofu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Yesu. 20 Tunaingia kwa njia mpya ambayo Yesu alitufungulia. Ni njia iliyo hai inayotuelekeza kupitia pazia; yaani mwili wa Yesu. 21 Na tunaye kuhani mkuu zaidi anayeisimamia nyumba ya Mungu. 22 Ikiwa imenyunyiziwa kwa damu ya Kristo, mioyo yetu imewekwa huru kutokana na dhamiri yenye hukumu, na miili yetu imeoshwa kwa maji safi. Hivyo mkaribieni Mungu kwa moyo safi, mkijaa ujasiri kwa sababu ya imani katika Kristo. 23 Tunapaswa kuling'ang'ania tumaini tulilonalo, bila kusitasita kuwaeleza watu juu yake. Tunaweza kumwamini Mungu kuwa atatimiza aliyoahidi.
Saidianeni Ninyi kwa Ninyi Kuwa Imara
24 Tunahitaji kumfikiria kila mtu kuona jinsi tunavyoweza kuhamasishana kuonesha upendo na kazi njema. 25 Tusiache kukutana pamoja, kama wanavyofanya wengine. Hapana, tunahitaji kuendelea kuhimizana wenyewe. Hili linazidi kuwa muhimu zaidi na zaidi kadri mnavyoona ile Siku inakaribia.
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-25; Lk 21:5-24)
13 Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!”
2 Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.”
3 Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, 4 “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?”
5 Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. 6 Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] nao watawadanganya wengi. 7 Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. 8 Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa.
© 2017 Bible League International