Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
6 1-2 Hivyo tusiendelee tena na masomo ya msingi juu ya Kristo. Tusiendelee kurudia kule tulikoanzia. Tuliyaanza maisha yetu mapya kwa kugeuka kutoka katika uovu tuliotenda zamani na kwa kumwamini Mungu. Hapo ndipo tulipofundishwa kuhusu mabatizo,[a] kuwawekea watu mikono,[b] ufufuo wa wale waliokwisha kufa, na hukumu ya mwisho. Sasa tunahitajika kuendelea mbele hadi kwenye mafundisho ya ukomavu zaidi. 3 Na hayo ndiyo tutayafanya Mungu akitupa kibali.
4-6 Baada ya watu kuiacha njia ya Kristo, je unaweza kuwafanya wabadilike tena katika maisha yao? Ninazungumzia wale watu ambao mwanzo walijifunza kweli, wakapokea karama za Mungu, na kushiriki katika Roho Mtakatifu. Walibarikiwa kusikia ujumbe mzuri wa Mungu na kuziona nguvu kuu za ulimwengu wake mpya. Lakini baadaye waliziacha zote, na siyo rahisi kuwafanya wabadilike tena. Ndiyo sababu wale watu wanaomwacha Kristo wanamsulibisha msalabani kwa mara nyingine, wakimwaibisha yeye mbele ya kila mtu.
7 Watu wengine wako kama ardhi inayopata mvua nyingi na kuzaa mazao mazuri kwa wale wanaoilima. Aina hiyo ya ardhi inazo baraka za Mungu. 8 Lakini watu wengine wako kama ardhi ambayo huzalisha miiba na magugu tu. Haifai na iko katika hatari ya kulaaniwa na Mungu. Itateketezwa kwa moto.
9 Rafiki zangu, sisemi haya kwa sababu nafikiri kuwa yanawatokea ninyi. Kwa hakika tunatarajia kuwa mtafanya vizuri zaidi; kwamba mtayafanya mambo mema yatakayotokea katika wokovu wenu. 10 Mungu ni wa haki, na ataikumbuka kila kazi mliyoifanya. Atakumbuka kuwa mliuonesha upendo wenu kwake kwa kuwasaidia watu wake na kwamba mnaendelea kuwasaidia. 11 Tunamtaka kila mmoja wenu awe radhi na mwenye shauku ya kuuonyesha upendo kama huo katika maisha yenu yote. Ndipo mtakapokuwa na uhakika wa kupata kile mnachokitumaini. 12 Hatupendi muwe wavivu. Tunapenda muwe kama wale, kwa sababu ya imani yao na uvumilivu, watapokea kile Mungu alichoahidi.
© 2017 Bible League International