Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Tajiri na Lazaro
19 Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. 20 Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. 21 Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake.
22 Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Ibrahimu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. 23 Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti[a] na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’
25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. 26 Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’
27 Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, 28 Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 Lakini Ibrahimu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’
30 Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Ibrahimu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’
31 Lakini Ibrahimu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’”
© 2017 Bible League International