Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Ninyi ni Kama Chumvi na Nuru
(Mk 9:50; 4:21; Lk 14:34-35; 8:16)
13 Mnahitajika kama chumvi inavyohitajiwa na wale waliopo duniani. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, haiwezi kufanywa chumvi tena. Haina manufaa yo yote isipokuwa hutupwa nje na kukanyagwa na watu.
14 Ninyi ni nuru inayong'aa ili ulimwengu uweze kuiona. Ni kama mji uliojengwa juu ya kilima unavyoonekana wazi. 15 Watu hawawashi taa na kuificha kwenye chungu. Bali huiweka kwenye kinara cha taa ili nuru iangaze kwa kila mtu. 16 Kwa namna hiyo hiyo mnapaswa kuwa nuru kwa ajili ya watu wengine. Hivyo ishini katika namna ambayo watakapoyaona matendo yenu mema, watamtukuza Baba yenu wa mbinguni.
Yesu Afundisha Kuhusu Sheria ya Musa
17 Msifikiri kwamba nimekuja kuiharibu Sheria ya Musa au mafundisho ya manabii. Sikuja kuyaharibu mafundisho yao bali kuyakamilisha. 18 Ninawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloondolewa katika sheria mpaka mbingu na nchi zitakapopita. Hakuna hata herufi ndogo ama nukta katika Sheria ya Musa itakayotoweka mpaka hapo itakapotimizwa.
19 Kila mtu anapaswa kutii kila amri iliyo katika sheria, hata ile isiyoonekana kuwa ya muhimu. Kila atakayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kuwafundisha wengine kuzivunja atahesabiwa kuwa ni mdogo sana katika ufalme wa Mungu. Lakini kila anayeitii na kuwafundisha wengine kuitii sheria atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. 20 Ninawambia, ni lazima muitii sheria ya Mungu kwa kiwango bora kuliko kile cha walimu wa sheria na Mafarisayo. La sivyo, hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu.
© 2017 Bible League International