Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Hekima ya Kweli
13 Nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Na aoneshe hekima yake kwa mwenendo mzuri, kwa matendo yake yanayofanywa kwa unyenyekevu unaoletwa na hekima. 14 Lakini kama mtakuwa na wivu wenye uchungu na ubinafsi ndani ya mioyo yenu, hamwezi kujivunia hekima yenu; kwamba kujivuna kwenu kungekuwa ni uongo unaoficha ukweli. 15 Hii sio aina ya hekima inayotoka juu mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyotoka kwa Roho wa Mungu bali ni ya kishetani. 16 Kwa sababu pale penye wivu na ubinafsi, basi panakuwepo vurugu na kila aina ya matendo maovu. 17 Lakini hekima inayotoka mbinguni juu kwanza juu ya yote ni safi, kisha ni ya amani ina upole na ina busara. Imejaa rehema na huzaa mavuno ya matendo mema. Haina upendeleo wala unafiki. 18 Wale wenye bidii ya kuleta amani na wanaopanda mbegu zao kwa matendo ya amani, watavuna haki kama mavuno yao.
Jitoe Mwenyewe kwa Mungu
4 Mapigano na magombano yanatokea wapi miongoni mwenu? Je, hayatoki kutoka ndani yenu wenyewe, kutoka katika tamaa zenu za starehe ambazo zinafanya vita siku zote ndani ya miili yenu? 2 Mnataka mambo lakini hamyapati, hivyo mnaua na mnakuwa na wivu juu ya watu wengine. Lakini bado hamwezi kuyafikia mnayoyataka, hivyo mnagombana na kupigana. Nanyi ndugu zangu hampokei mambo mnayoyataka kwa sababu hamumwombi Mungu. 3 Na mnapoomba, lakini hampokei cho chote kwa sababu mnaomba kwa dhamiri mbaya, ili muweze kuvitumia mlivyopatiwa kwa anasa zenu.
7 Kwa hiyo jiwekeni chini ya Mungu. Mpingeni Shetani naye atawakimbia ninyi. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Iosheni mikono yenu ninyi wenye dhambi na kuitakasa mioyo yenu enyi wanafiki!
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)
30 Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31 alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)
33 Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34 Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.
35 Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”
36 Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37 “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”
© 2017 Bible League International