Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
29 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo! Ninyi ni wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii, na kuyaheshimu makaburi ya wenye haki waliouawa. 30 Na mnasema, ‘Ikiwa tungeishi nyakati za mababu zetu, tusingewasaidia kuwaua manabii hawa.’ 31 Hivyo mnathibitisha kuwa ninyi ni uzao wa wale waliowaua manabii. 32 Na mtaimalizia dhambi waliyoianza mababu zenu!
33 Enyi nyoka! Ninyi mlio wa uzao wa nyoka wenye sumu kali! Hamtaikwepa adhabu. Mtahukumiwa na kutupwa Jehanamu! 34 Hivyo ninawaambia: Ninawatuma manabii na walimu wenye hekima na wanaojua Maandiko. Lakini mtawaua, mtawatundika baadhi yao kwenye misalaba na kuwapiga wengine katika masinagogi yenu. Mtawafukuza kutoka katika mji mmoja hadi mwingine.
35 Hivyo mtakuwa na hatia kutokana vifo vyote vya watu wema wote waliouawa duniani. Mtakuwa na hatia kwa kumwua mtu wa haki Habili, na mtakuwa na hatia kwa kuuawa kwa Zakaria[a] mwana wa Barakia mliyemwua kati ya Hekalu na madhabahu. Mtakuwa na hatia ya kuwaua watu wote wema walioishi kati ya wakati wa Habili mpaka wakati wa Zakaria. 36 Niaminini ninapowaambia kuwa mambo haya yote yatawapata ninyi watu mnaoishi sasa.
Yesu Awaonya Watu wa Yerusalemu
(Lk 13:34-35)
37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu! Unayewaua manabii. Unawapiga kwa mawe wale ambao Mungu amewatuma kwako. Mara nyingi nimetaka kuwasaidia watu wako. Nimetaka kuwakusanya watu wako kama kuku anavyowakusanya vifaranga wake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu kufanya hivyo. 38 Sasa Hekalu lako litaachwa ukiwa kabisa. 39 Ninakwambia, hautaniona tena mpaka wakati utakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)
© 2017 Bible League International