Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
25 Ndugu zangu, ieleweni siri hii ya ukweli. Kweli hii itawasaidia ninyi mjue kuwa hamfahamu kila kitu. Kweli ni hii: Sehemu ya Israeli wamefanywa kuwa wakaidi, lakini hiyo itabadilika wasio Wayahudi, wengi, watakapokuja kwa Mungu. 26 Na hivyo ndivyo Israeli wote watakavyookolewa. Kama Maandiko yanavyosema,
“Mwokozi atakuja kutoka Sayuni;
atauondoa uovu kutoka kwa wazaliwa wa Yakobo.
27 Nami nitalifanya patano hili na watu wale
nitakapoziondoa dhambi zao.”(A)
28 Kwa sasa, Wayahudi wanaokataa kuzipokea Habari Njema wamekuwa adui wa Habari Njema. Hili limetokea kwa manufaa yenu ninyi msio Wayahudi. Lakini bado Wayahudi ni wateule wa Mungu, na anawapenda kwa sababu ya ahadi alizozifanya kwa baba zao. 29 Mungu habadili mawazo yake kuhusu watu anaowaita. Kamwe haamui kuzirudisha baraka alizokwisha kuwapa. 30 Wakati mmoja ninyi pia mlikataa kumtii Mungu. Lakini sasa mmeipokea rehema, kwa sababu Wayahudi walikataa kutii. 31 Na sasa wao ndiyo wanaokataa kutii, kwa sababu Mungu aliwaonesha ninyi rehema zake. Lakini hili limetokea ili nao pia waweze kupokea rehema kutoka kwake. 32 Mungu amemfungia kila mmoja katika gereza la kutokutii. Lakini amefanya hivi ili aweze kuonesha rehema yake kwa wote.
© 2017 Bible League International